Wafamasia, wataalamu wa maabara watajwa chanzo uuzwaji dawa holela

Mbeya. Serikali imesema bado kuna dawa na vifaa tiba vyenye nembo ya Serikali zinazokamatwa kwenye maduka ya dawa na hospitali na maabara  za watu binafsi zikiuzwa.

Inadaiwa baadhi ya wataalamu wa maabara huagiza vifaa tiba hivyo vyenye nembo ya  Serikali na kuvifungia stoo, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi Aprili 18, 2024 na Mganga Mkuu wa  Mkoa wa Nbeya,  Elizabeth Nyema alipofungua mkutano wa wataalamu wa maabara na wafamasia wa  ngazi ya vituo vya afya wa halmashauri na hospitali.

“Kuna wafamasia na wataalamu wa maabara wenye maduka ya dawa na hospitali binafsi si waaminifu, katika kaguzi mbalimbali dawa na  vifaa tiba vya Serikali vinabainika kwenye  maduka ya dawa na hospitali zao binafsi  kinyume cha utaratibu,” amesema.

Aidha, Dk Nyema amewaagiza wataalamu wote wa maabara wakipokea vifaa tiba na dawa kuziwekea nembo maalumu kwa lengo la kuisaidia Serikali kukabiliana na changamoto hiyo katika kutoa huduma.

“TMDA imetekeleza majukumu yao kwa kupita kwenye maduka kufanya kaguzi, lakini bado kwa upande wa Serikali kuna changamoto, maduka ya wafamasia katika kaguzi wanabainika kuwa na vifaa tiba na dawa za Serikali kinyume cha utaratibu,” amesema.

Baadhi ya wafamasia na wataalamu wa maabara walioshiriki kutoka vituo vya afya na  hosptali katika halmashauri saba za mkoa wa Mbeya .Picha na Hawa Mathias

Kwa upande wake, Meneja wa TMDA, Dk Anitha Mshighati amesema wanaendelea kuimarisha udhibiti katika maeneo ya mipakani, ili kuhakikisha vifaa vinavyozalishwa na kuingizwa nchini viwe vimesajiliwa.

“Lengo ni kuona vifaa tiba vinavyoingizwa  nchini  na kuzalishwa kwenye viwanda kuwa na ubora na ufanisi katika utoaji wa huduma, sambamba na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya kada ya wafamasia na maabara,”amesema.

Meneja wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Dk Anitha Mshighati akieleza lengo la mafunzo hayo

Elizabeth Mashauri, msanifu wa vifaa tiba kutoka Hosptali ya Wilaya ya Kyela, amesema kuna changamoto hiyo kwa baadhi ya wafamasia kuwa na vifaa tiba na dawa za Serikali kinyume cha utaratibu na kutoa siri za kazi ya ukaguzi.

“Zamani TMDA walikuwa wakiwatumia wafamasia kuwapeleka kwenye maduka ya wauzaji wa dawa, lakini kuna vifaa tiba vya Serikali ambavyo muuzaji hana uwezo wa kutumia kutoa huduma kwa wagonjwa,” amesema.

 Aidha, ameomba Serikali kufanya ukaguzi wa mara kwa mara, ili kudhibiti matumizi holela ya vifaa tiba na dawa za Serikali  katika hosptali na maduka binafsi.

Related Posts