MASHABIKI wa Simba na Yanga tayari viroho vimeanza kuwadunda, wakati wakiendelea kuhesabu siku kabla ya timu zao kushuka katika pambano la Ligi Kuu Bara litakalopigwa Jumamosi hii ya Aprili 20, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Hili litakuwa pambano la 112 kwa timu hizo kukutana katika Ligi Kuu Bara tangu mwaka 1965, lakini likiwa ni la 14 kwao kukutana ndani ya Aprili na Simba imeshinda mara nne, Yanga mara tatu huku mechi sita zikimalizika bila ya mbabe.
Mwanaspoti linakuletea michezo yote 13 ambayo tayari imeshapigwa ndani ya Aprili tangu 1965 na kuonyesha ni kwa jinsi gani pambano hilo linalosubiriwa kwa hamu litatoa taswira kwa miamba hiyo katika harakati za kuwania ubingwa msimu huu.
Miamba hii ilikutana kwa mara ya kwanza katika pambano hili la Kariakoo dabi na Yanga ilikuwa na morali kubwa baada ya mchezo wao wa mwisho uliopigwa Septemba 5, 1981 kuifunga Simba bao 1-0 lililofungwa na Juma Mkambi ‘Jenerali’.
Kujiamini kwao kuliwabeba, kwani waliendeleza ubabe kwa watani wao kwa kuwafunga tena kwa bao 1-0, lililowekwa kimiani na Rashid Hanzuruni dakika ya pili tu tangu pambano hilo lilipoanza na kupelekea kudumu hadi mwishoni mwa mchezo huo.
Hili ni pambano la pili kwa timu hizi kukutana ndani ya Aprili na Yanga iliendeleza tena ubabe wake kwa kushinda kwa mabao 3-1 ikiwa ni mchezo wa 12 kwa Simba kucheza bila ya kuonja ladha ya ushindi mbele ya watani zao hao wa jadi.
Simba ilikuwa ni ya kwanza kufunga bao dakika ya 14 tu kupitia kwa Kihwelu Mussa kabla ya Yanga kusawazisha dakika ya 21 kupitia kwa Charles Mkwasa kisha Makumbi Juma ‘Homa ya Jiji’ na Omar Hussein ‘Keegan’ kuongeza mengine dakika ya 33 na 84.
Mchezo huu uliisha kwa sare ya bao 1-1 na Simba iliitangulia kupata bao kupitia kwa Edward Chumila dakika ya 25 kisha Yanga kusawazisha dakika tatu baadae lililofungwa na Justin Mtekere na kuzifanya kugawana pointi moja kila mmoja.
Simba na Yanga zikakutana tena katika mechi nyingine ya Aprili, ikipigwa Jumapili, ikiwa ni baada ya miaka minne kupita bila timu hizo kukutana katika mwezi huo.
Katika pambano hilo tamu na la kusisimua, Yanga iliendelea tena ubabe wake kwa watani wao kwa kuifunga Simba bao 1-0, lililofungwa kwa shuti kali na la mbali na aliyekuwa beki wa kushoto wa kikosi hicho, Kenneth Mkapa dakika ya 10.
Mkapa alifunga bao hilo akitokea kuifungia Yanga ugenini dhidi ya Ismailia ya Misri katika mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Miaka mitano baadae miamba hii ikakutana tena Aprili katika mechi iliyoshindwa kutoa mshindi, licha ya Abdallah Msamba ambaye kwa sasa ni marehemu kuandika rekodi katika pambano hilo ambayo haijawahi kufikiwa tena katika Kariakoo Dabi.
Msamba aliyewahi kuichezea Sigara, alifunga bao la mapema zaidi katika dabi iliyowakutanisha miamba hiyo kwa kutupia sekunde ya 56 tu na kuitanguliza Simba kabla ya Yanga kuchomoa dakika ya 16 kupitia kwa nyota, Idelfonce Amlima ‘Chinga Two’.
Baada ya unyonge ndani ya Aprili, Simba ilisahihisha makosa kwenye mchezo huo uliokuwa wa sita kwao kukutana ndani ya mwezi huo.
Tofauti na michezo mitano ya nyuma, safari hii katika mechi hiyo iliyopigwa Jumapili, Simba ilipindua meza na kuinyoosha Yanga kwa mabao 2-1, licha ya Yanga kutangulia kupata bao la uongozi kupitia, Aaron Nyanda aliyelifunga dakika ya 39.
Yanga ilishangilia bao hilo kwa muda wa dakika tano tu, kwani Simba ilichomoa kwa bao lililofungwa na Ally Msigwa hivyo kuufanya mchezo huo kwenda mapumziko kwa bao 1-1 ingawa dakika ya 64 Athuman Machuppa alitupia la pili na la ushindi.
Simba na Yanga zikakutana tena ndani ya Aprili ikiwa ni mchezo wa saba kwao kukutana na ulichezwa baada ya takribani miaka mitatu kupita tangu mara ya mwisho miamba hiyo ilipokutana na hata hivyo mechi hiyo iliisha bila ya kufungana.
Mwaka mmoja tena, Simba na Yanga zikakutana ndani ya Aprili ikiwa ni muda mfupi zaidi kwa timu hizo kukutana ndani ya mwezi huo na mechi hiyo iliyopigwa siku ya Jumapili ilimalizika bila mbabe baada ya sare ya kufungana kwa mabao 2-2.
Simba ndio iliyokuwa ya kwanza kufunga bao kupitia kwa Ramadhani Chombo ‘Redondo’ dakika ya 23 tu ya mchezo na kudumu hadi mapumziko.
Kipindi cha pili kilianza kwa Yanga kusawazisha bao kupitia kwa Mkenya, Ben Mwalala dakika ya 48 na Simba kuongeza la pili kupitia kwa Haruna Moshi ‘Boban’ dakika ya 62 na wakati mashabiki wakiamini mechi imeisha kwa Simba kuibuka na ushindi, Yanga ilisawazisha bao hilo jioni lililofungwa na Jerry Tegete dakika ya 90.
Simba na Yanga zilikutana tena baada ya mwaka mmoja kupita katika ngoma iliyopigwa Jumamosi na Simba kutoka na ushindi mtamu katika pambano hilo la funga nikufunge.
Simba ilipata ushindi wake wa pili dhidi ya Yanga ndani ya Aprili kwa kuifumua mabao 4-3, bao la ushindi likiwekwa kimiani dakika za majeruhi na Mkenya, Hillary Echesa.
Simba ilionyesha dhamira yake ya kutoka na ushindi tangu mapema kwa kupata bao la kuongoza lililofungwa na Uhuru Seleman dakika ya tatu tu ya pambano hilo, kabla ya Yanga kuchomoa mnamo dakika ya 30 kupitia nyota wake, Athuman Idd ‘Chuji’.
Kipindi cha pili Mussa Hassan Mgosi aliifungia Simba bao la pili dakika ya 53, lililosawazishwa na Jerry Tegete dakika ya 69 kabla ya Mgosi kuongeza jingine dakika ya 74 ambalo lilisawazishwa pia na Jerry Tegete kunako dakika ya 89.
Baada ya piga nikupige ndipo zikaongezwa dakika tano za nyongeza na Echesa akaifungia Simba bao la nne na la ushindi hivyo kuwafanya mashabiki wa Yanga kunyong’onyea kwani waliamini mchezo huo tayari umeisha kwa sare ya kufungana mabao 3-3.
Ilipita miaka minne kabla ya kukutana tena ndani ya Aprili, mechi iliyopigwa siku ya Jumamosi na timu hizo kushindwa kutambiana.
Katika pambano hilo la 10 kwa timu hizo ndani ya Aprili, Simba ilitangulia kupata bao kupitia kwa Haruna Chanongo dakika ya 75 ya mchezo huo kabla ya Simon Msuva kuisawazishia Yanga dakika ya 86 na mchezo huo kuisha kwa sare ya kufungana 1-1.
Katika mechi ya 100 kwa watani wa jadi katika Ligi ya Bara tangu 1965, Simba na Yanga zilikutana tena ndani ya Aprili baada ya kupita miaka minne.
Simba ilipata ushindi wake wa tatu dhidi ya Yanga kwa mwezi huo kwa bao lililofungwa na beki, Erasto Nyoni dakika ya 37 akimalizia frii-kiki safi iliyopigwa na Shiza Kichuya na kumparaza kiungo, Rafael Daud na nyota huyo kuweka kimiani.
Miaka minne baadae tangu Simba na Yanga kukutana ndani ya Aprili, zikakutana tena ambapo licha ya kutambiana kama ilivyo kawaida kwa mashabiki wa timu zote mbili ila hakuna aliyeibuka mbabe kwani mchezo huo uliisha kwa suluhu na kutopatikana mbabe.
Yanga ikiwa na matumaini makubwa ya kuibuka na ushindi ilijikuta ikiangukia pua katika mchezo huo baada ya kufungwa 2-0 kwa mabao yaliyowekwa kimiani na Henock Inonga dakika ya pili tu kisha Kibu Denis akafunga la pili kunako dakika ya 32.
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa Oktoba 23, 2022, timu hizi zilifungana bao 1-1 na Simba ilitangulia kupitia kwa nyota wake Mghana, Augustine Okrah dakika ya 15 kisha Stephane Aziz KI akaisawazishia Yanga dakika ya 45.
Kitendawili cha nani mbabe kitateguliwa Jumamosi hii ingawa Yanga inaingia katika mchezo huo ikiwa na morali kubwa hasa baada ya mechi yao ya mwisho iliyopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Novemba 5, 2023 kuifunga Simba kwa mabao 5-1.
Katika mchezo huo wa mwisho mabao ya Yanga yalifungwa na Maxi Nzengeli aliyefunga mawili wakati Kennedy Musonda, Pacome Zouzoua na Stephane Aziz KI wakifunga moja kila mmoja wao huku la Simba la kufutia machozi likifungwa na Kibu Denis.
Nyota wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua anasema licha ya rekodi hiyo ila mchezo baina ya timu hizo zinapokutana huwa hautabiriki.
“Rekodi ni kitu kimoja lakini uwanjani kinachoweza kutokea ni jambo lingine, mechi za aina hii huwa sio za kuzitabiria kwa sababu ya maajabu ambayo yamewahi kutokea huko mwanzoni, Yanga ina nafasi ya kushinda japo lolote linaweza kutokea.”