Benchikha na msala wa 5-1 za Yanga SC

Ilikuwa Novemba 5, 2023 uwanja wa Benjamin Mkapa ambapo Yanga iliichapa Simba mabao 5-1 kwenye mechi ya ligi na kupelekea kufutwa kazi kwa aliyekuwa kocha mkuu wa wekundu wa Msimbazi, Roberto Oliveira ‘Robertinho’.

Ni mechi iliyokuwa na hisia mbili tofauti. Furaha kwa wageni Yanga. Huzuni kwa kwa wenyeji Simba. Iliichukua Yanga dakika tatu kuandika bao la kuongoza kupitia kwa Kennedy Musonda aliyefunga kwa kichwa kabla ya Kibu Denis kuisawazishia Simba kwa bao la kichwa pia dakika ya tisa na dakika 45 za kwanza kumalizika kwa sare pale kwa Mkapa huku kila shabiki akipiga hesabu za kushinda mechi hiyo baada ya kuonekana kubalansi.

Kipindi cha pili Yanga ikarejea mchezoni na kufunga bao la pili dakika ya 63 kupitia kwa Maxi Nzengeli kisha dakika ya 73 Stephane Aziz Ki akaweka kamba ya tatu na dakika ya 77 Maxi akapiga tena bao la nne kisha Pacome Zouzoua akagongelea msumari wa mwisho dakika ya 87 kwa mkwaju wa Penalti na ubao wa matokeo kusomeka 1-5.

Huo ndio ulikuwa mwisho wa enzi za Robertinho ndani ya Simba na baadae timu hiyo akapewa Mualgeria Abdelhack Benchikha akiwa ametoka kushinda kombe la Caf Super Cup akiwa na US Alger.

Zama mpya za Benchikha zikaanzia huku zikiandamwa na vitimbwi vya hapa na pale ikiwemo timu kutocheza soka la kufurahisha sambamba na kushindwa kuvuka robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Pamoja na yote hayo lakini hii ya Jumamosi itakuwa Dabi ya kwanza kwa Benchikha katika aridhi hii ya Nyerere pale atakapoivaa Yanga iliyochini ya Muargentina Miguel Gamondi aliyemfukuzisha kazi Robertinho baada ya kumchapa mabao 5-1.

Ni muda wa Benchikha kufuta unyonge wa Simba kwa Yanga msimu huu akiwa na kikosi ambacho kwa asilimia kubwa kiliicheza mechi ya 5-1, Novemba mwaka jana.

Benchikha katika kikosi chake kunaonekana kuwa na mabadiliko machache ukilinganisha na namna alivyokuwa akipanga timu Mbrazili Robertinho.

MFUMO
Makocha wote wawili hao mfumo wanaopendelea kutumia ni 4-2-3-1 ambapo mabeki huwa wanne, viungo wachini wawili na watatu juu kisha mshambuliaji mmoja.

Robertinho akiwa Simba alipendelea kuwatumia wachezaji Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Che Malone Fondoh, Henock Inonga, Fabrice Ngoma, Sadio Kanoute, Jean Baleke, Saidi Ntibanzokiza, Clatous Chama na Kibu Denis na hao ndio walianza wakati Simba inakufa 5-1 mbele ya Yanga.
Hata hivyo Benchikha tangu ametua Simba naye ameonekana kupendelea zaidi kutumia mfumo huo.

Tofauti ni mabadiliko ya baadhi ya wachezaji ambapo kwenye eneo la kiungo ameongezeka Babacar Sarr na kuondoka Jean Baleke eneo ambalo hadi leo Benchikha hajapata mchezaji maalumu wa kudumu na mara nyingi huwatumia Kibu, Saido, Freddy Michael au Pa Omar Jobe kucheza hapo licha ya kuwa hakuna mwenye uhakika wa namba ya kudumu eneo hilo.

Utofauti mwingine Benchika kuna muda amekuwa akifanya mabadiliko ya kikosi lakini pia ni mwepesi kubadili wachezaji na aina ya uchezaji (mfumo), wakati mechi ikiendelea.

Wachezaji kama Ayoub Lakred na Ally Salim eneo la kipa wamekuwa wakibadilishana huku kwa mabeki, Kennedy Juma, Israel Mwenda, Hussein Kazi na David Kameta wote wakipata nafasi japo kwa muda mfupi vilevile kwa viungo Mzamiru Yassin, Ladack Chasambi, Willy Onana sawa na washambuliaji Jobe na Freddy nao hupata nafasi ndani ya kikosi cha Benchikha.

Kiufupi Simba ile iliyopigwa tano na Yanga ina mabadiliko ya wastani wa wachezaji watatu tu na hii mpya ya Benchikha kwa maana ya kipa kutoka Manula hadi Salim au Lakred, kiungo Sarr aliyeingia na Baleke aliyeondoka ambaye pengo lake bado liko wazi pale Msimbazi.

MORALI
Licha ya Benchikha kuanza vyema maisha ndani ya Simba kwa kuibadili timu hiyo kucheza kwa Morali ya juu na wachezaji kujituma zaidi lakini katika mechi za hivi karibuni inaonekana hali imerejea kuwa vile vile alivyoiacha Robertinho.

Ukirejea mechi ya mwisho ya Simba dhidi ya Ihefu baadhi ya wachezaji wanaonekana kucheza kwa morali ya chini. Willy Onana ni mfano wa hilo huku Saido na Chama nao wakilalamikiwa kwa kushindwa kujituma zaidi.

Huenda kutokana na ukubwa wa Dabi wachezaji wanaweza kuiheshimu mechi hiyo na kujituma kwani inaushindani mkubwa, historia na rekodi ambazo wengi wao wanatakiwa kuweka lakini nje ya hapo Simba inaonekana kupoa zaidi hususani kwenye mechi za mashindano ya ndani kuliko hata alivyoiacha Robertinho.

Hyo ni mitihani mikubwa miwili inayomkabili Benchikha ambapo kama ataishinda atajitengenezea heshima na ufalme mpya ndani ya kikosi hicho cha Wanamsimbazi.

Beki wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa alisema; “Makocha wengi mbinu zao hazitofautiani sana, kinachobeba zaidi ni namna wachezaji wanazielewa na kuzifanyia kazi.

 Lakini kwakuwa hii ni mechi ya Dabi bado kila timu inaweza kushinda na lolote linaweza kutokea hivyo kufungwa 5-1 kwa Simba kwenye mechi ya kwanza sio kigezo kwamba huu ni muda wao kulipiza au kufungwa tena mabao mengi,” alisema Pawasa.

Mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Saidi Maulidi ‘SMG’ alisema “Kama wachezaji hawako tayari kupokea wanachopewa na kufanyia kazi pia kujiongeza utawalaumu tu makocha.

Binafsi naona kocha aliyeondoka Simba (Robertinho), alikuwa mzuri sawa na huyu (Benchikha) wa sasa kikubwa ni wachezaji kutimiza wajibu wao kwa ufasaha,” alisema SMG.

Kocha wa Dodoma Jiji, Mkenya Francis Baraza alisema: “Tunatofautiana unaweza kuwa unapendelea mfumo flani lakini usiutumie kutokana na kukosa wachezaji wanaofiti hapo hivyo kuwalinganisha makocha tena wa timu moja huwa inahitaji vitu vingi lakini jambo la kwanza kwa kila mwalimu ni kutaka kutimiza malengo tu,” alisema Baraza. Nini maoni yako kuhusiana na mechi hii ya watani wa jadi Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Mkapa.

Related Posts