Dabi ya Aziz KI na Chama

UKISIKIA mwisho wa ubishi ndio huu wakati vigogo vya soka nchini, Simba na Yanga zitavaana katika mechi ya marudiano ya Ligi Kuu Bara.

Ndio, kesho kuna Dabi ya Kariakoo itakayopigwa kuanzia saa 11:00 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam huku kila mmoja ikiwa na kumbukumbu ya mechi iliyopita iliyopigwa Novemba 5 mwaka jana na matokeo kuwa mabao 5-1. Yanga ikiibuka na ushindi huo wa kishindo.

Hii ni mechi kubwa kwa Tanzania na Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. 

Lakini siku zote kubwa zinahitaji wachezaji wakubwa kuamua matokeo lakini sio Kariakoo Dabi. Mechi hii ya Watani wa Jadi haijawahi kuwa na mwenyewe. 

Haijalishi ubora wa timu. Haitegemei historia. Haina cha mgeni wala mwenyeji. Unaweza kudhani ni mechi ya Stephen Aziz KI na Clatous Chama, kumbe ni mechi ya Willy Onana! Haina mwenyewe.

Unaweza kudhani ni mechi ya Mudathir Yahya, kumbe ni Jonas Mkude. Kila kitu kinaenda tofauti. Kariakoo Dabi ni mechi kubwa sio tu Tanzania, Afrika inakwenda kuamua matokeo. Tunapaswa kujivunia sana ukubwa wa mechi hii. Ni muda wa kuanza hata kuiuza nchi za jirani.

Kama muziki wa Bongo Fleva unauza Afrika ya Mashariki, umefika wakati ya Dabi ya Kariakoo kuuzwa Afrika. Bila shaka Chama ni moja kati ya wachezaji wenye uwezo mkubwa sana kwenye kikosi cha Simba. Chama akiamka vizuri, ana uwezo wa kuiamua mechi mapema sana. 

Akili ya Mwamba wa Lusaka ina kasi pengine kuliko hata miguu yake. Ni fundi wa mpira haswa. Ni mchezaji wa mechi kubwa. Moja kati ya kumbukumbu nzuri ya Mwamba wa Lusaka kwenye Dabi ya Kariakoo, ni mechi ya Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho wakati huo likijulikana kama Azam Sports Federation Cup ambapo Mnyama alishinda mabao 4-1 pale kwa Mkapa Julai 2020.  

Chama alikuwa Chama. Jose Miquissone alikuwa kwenye kiwango cha lami kabisa. Mechi ya Jumamosi hii, inamtaka Chama kuwa katika ubora wa kuivusha Simba. Chama amekuwa muhanga sana wa mechi hizi na hasa pale timu inapofanya vibaya. 

Amekuwa akipewa lawama na shutuma nyingi sana ambazo hakuna aliyewahi kuzithibitisha. Kama akiamka vizuri, kazini kwa Yanga kutakuwa na kazi.

Stephane Aziz KI ni moja kati ya wauaji wa Jangwani msimu huu. Taja wachezaji wote unaowajua lakini usisahau funguo. Amekuwa na msimu mzuri sana. Amefunga sana. Ameamua sana mechi za Yanga msimu huu.

Ana historia na rekodi nzuri kuelekea Dabi ya Kariakoo. Aliwafunga Simba akiwa na Asec Memosas ya pale  Ivory Coast. Anakwenda katika Dabi ya Kariakoo kama kinara wa mabao wa Ligi Kuu Bara. Amefunga mabao 14 na ameasisti saba.
Hakuna namna unaweza kuizungumza mechi hii bila kutaja jina lake. Aziz Kİ ana kila kitu uwanjani. 

Kila nikikumbuka namna alivyowavuruga Mamelod Sundowns, naona kabisa kazini kwa Simba kutakuwa na kazi. Ni mara chache sana kuona mchezaji mwenye akili, nguvu, ufundi kama Aziz KI! 
Ndiye mtu anayesumbua zaidi wapinzani akitokea kati. 

Sadio Kanoute, Fabrice Ngoma wana kazi sana kumzuia Kİ katikati ya uwanja. Njia ya kwanza ya kuidhibiti Yanga, ni kumzuia kwanza Aziz KI. Kama Simba wanataka Heshima leo Jumamosi, zoezi la kwanza iwe ni kumzuia KI.

Ni kweli Yanga ina wachezaji wengi, lakini ina Aziz KI mmoja tu. Labda ni kwa sababu dabi haina mwenyewe. Labda ni kwa sababu mechi hii haiendeshwi na historia lakini, haiondoi umuhimu wa KI pale Jangwani. Ni kweli wakati mwingine mechi za Dabi ya Kariakoo zimekuwa zikituletea staa mpya nchini. 

Shizza Ramadhani Kichuya, mchezaji wa zamani wa Simba alikuwa na jina kubwa ni kwa sababu tu ya kuwafunga Yanga. Ndivyo inavyokuwa wakati mwingine. Ukute ni mechi inayokwenda kumpa Heshima Jobe! Huenda ni mechi ya Freddy. Dabi ya Kariakoo haitabiriki. Dabi ya Kariakoo haina mwenyewe.

Pale Yanga kuwa pia na watu wengi sana ambao wameibeba timu msimu huu. Huwezi kujua, labda ni mechi ya Mudathir Yahya. Simu zimeita sana msimu huu. 

Ni Kiungo aliyefanya makubwa sana akiwa na Azam FC na Zanzibar Heroes, lakini pengine jina lake litaimbwa zaidi akiwa Yanga msimu huu. Najua alipigana sana msimu uliopita lakini msimu huu amekuja na utofauti. Mudathir anapiga sana simu. Mudathir anafunga sana mabao. 

Hapa ndipo utofauti unapokuja. Mechi ya Jumamosi kila goti litapigwa. Kila silaha itatumika kuleta heshima mjini. Huwezi kujua. Labda ni mechi ya Maxi Nzengeli. Wakati anaanza msimu, matarajio yalikuwa ni makubwa sana kwake lakini, kuna muda ni kama alipotea. 

Ni kama aliyumba kidogo ingawa ukweli utabaki pale pale, kijana kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni fundi na nusu. Ni mchezaji mwenye umbo dogo, lakini mguuni upo. Anajua kukaba. Anajua kufunga. Kasi yake na uharaka wa kufanya maamuzi ni silaha dhidi ya mnyama. 

Tunaweza kumzungumza Chama. Tunaweza kunzungumza KI. Kisha ukweli unabaki kuwa, Dabi ya Kariakoo haina mwenyewe. Hakuna aliyeikodi. Ukienda pale unyamani, kuna mtu anaitwa mgeni rasmi. Kibu Denis. Ni hatari na nusu. Huyu ndiye mchezaji pekee mzawa kwa sasa mwenye muendelezo mzuri wa ubora katika Dabi. 

Mchezaji mwenye kasi na nguvu ambaye kama ataongeza ubora kwenye umaliziaji, Kibu atamlaza mtu na viatu pale kwa Mkapa. Hii mechi haina mwenyewe. Hii mechi imegoma kutabirika. Kama kuna usajili bora waliofanya Simba msimu huu, basi ni Fabrice Ngoma. Huyu ni mtu ni balaa. Fundi wa boli. 

Popote anapoupeleka mpira unatii. Khalid Aucho, Mudathir na Jonas Mkude wanapaswa kuwa kwenye ubora wao vinginevyo, Ngoma atawapoteza. Ana kila kitu cha kuamua mechi ya leo Jumamosi. 
Moja ya matatizo makubwa tuliyonayo kwa sasa ni Waamuzi. 

Natamani kuona mtu akifungwa kihalali. Watu wa Azam Media wanafanya kazi kubwa na nzuri sana, lakini umakini mkubwa sana unahitajika katika Dabi ya Kariakoo.

Tofauti ya mechi hii na nyingine, ni namna inavyobeba Hisia za Watanzania. Kosa moja la Mwamuzi, linaumiza Watanzania zaidi ya Milioni 20! Watu wa televisheni nadhani iko haja ya kuongeza Kamera. Mambo ya Mpira ulivuka au haukuvuka, hayatakiwi kwa Mkapa.

Hii ni Sikukuu ya wapenzi wa soka nchini. Huu ni mtoko wa Simba na Yanga. Tunahitaji kuwa na Waamuzi wa kiwango cha Simba na Yanga. Tunahitaji kuwa na matangazo yenye ubora wa Simba na Yanga. Ufundi wa Chama unapaswa kuonekana vizuri kwa Watanzania. Mashuti ya Aziz KI yanapaswa kumulikwa vizuri na kamera za Azam Tv.

Hii mechi ni fahari ya Tanzania ni vema ikapewa upekee. Vyombo vya ulinzi pale uwanjani, ni vema vikasaidia zaidi watu kuliko kuumiza. Kumekuwa na matumizi ya nguvu mara nyingi sana katika Dabi ya Kariakoo.

Mtu anakwenda kutazama mechi, anarudi kavimba kwa kichapo. Matukio ya kupiga watu na wakati mwingine kuwadhalilisha yanatia doa mechi kubwa ya kiwango hiki. 

Hii mechi ni nembo ya mpira wetu. Tuihudumie kwa heshima kubwa. Kila la heri Watoto wa Jangwani. Kila la heri Mnyama mkali, tukutane kwa Mkapa.

Related Posts

en English sw Swahili