DAWASA NA BONDE LA WAMI WAUNDA VIKUNDI RAFIKI VYA MAZINGIRA KULINDA MTO RUVU. – MWANAHARAKATI MZALENDO

 

 

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam DAWASA kwa kushirikiana na Bonde la Wami Ruvu wameunda na kuanzisha vikundi rafiki vya Mazingira vitakavyosaidia kulinda Mto Ruvu ikiwa ni sehemu ya ulinzi na utunzaji wa vyanzo vya maji.

Akizungumza wakati wa Mkutano wa kutambulisha vikundi hivyo kwa ngazi ya Mkoa na Wilaya Mkoa Pwani, Mwakilishi wa Afisa Mtendaji Mkuu DAWASA ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha udhibiti ubora, Mhandisi Christian Christopher ameeleza kuwa lengo la kuunda vikundi mazingira ni kuhakikisha vyanzo vya maji hasa mto Ruvu ambao ni tegemeo la Wakazi wa Mikoa ya Dar na Pwani katika upatikanaji wa maji vinalindwa na kuwa na matumizi sahihi.

“Lengo ni kuunda Vikundi Mazingira rafiki wa Mto ruvu ni kuhakikisha wanasimamia utunzaji wa mto kandokando ya Mto na kuhakikisha wananchi wanafanya shughuli zao bila kuathiri vyanzo vya maji na kuahidi Mamlaka kuwa bega kwa bega na vikundi hivyo kuhakikisha vinatekeleza majukumu yake kikamilifu” ameeleza Mhandisi Christopher

 

 

 

 

Mhandisi Christopher ameongeza kuwa utunzaji wa vyanzo vya maji husaidia kuepusha jamii na majanga makubwa kama vile uharibifu wa Mazingira yanayopeleka ukame hivyo uwepo wa vikundi ni jambo lenye tija kubwa katika sekta ya Maji Nchini.

Ndugu Innocent Paul kutoka Bonde la Wami Ruvu ameeleza ni muhimu kutunza mto Ruvu, Ili kuepuka changamoto za upungufu wa maji katika Mkoa wa Dar es salaam na Pwani zinaweza kusababishwa na uharibifu wa Mazingira hasa katika vyanzo vya maji.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Mtambani katika Wilaya ya Bagamoyo, Bi Mwajuma Denge amepongeza uanzishwaji wa vikundi hivi na kusisitiza kuwa vitaleta manufaa kiuchumi kwa wananchi, zaidi akiwahakikishia wajumbe wa vikundi hivi kuwa mchakato wa kuvisajili utakua wa haraka ili viweze kufanya kazi vyema.

Pamoja na uundaji wa vikundi hivi, elimu juu ya uendeshaji wa vikundi rafiki vya kimazingira imetolewa kutoka kwa wageni kikundi cha UWAMAKIZI kutoka Mkoani Tanga kwa kueleza faida nyingi zinazopatikana katika vikundi hivi.

Jumla ya vikundi rafiki 36 vya Mazingira vimeundwa kutoka katika Vijiji 12 vya Vikuruti, Mihande bomu, Kitemvu, Kibwende, Kongo, Yombo, Chasimba, Misweduka, Miswe chini, Mbwawa shule, Mkoleni, na Ruvu kwa dosa vilivyopo katika kata nne za Yombo, Mbwawa, Mtambani na Malandizi katika Mkoa wa Pwani.

 

 

 

 

 

 

 

 

Related Posts