Fahamu njia sahihi ya kuacha pombe kiafya

Dar es Salaam. Ni uchungu kwa ndugu pale mpendwa wao anapoangukia kwenye unywaji wa pombe wa kupindukia.

Mara nyingi hufanya jitihada za kusaidia na wengine kuhangaika kwa waganga wa kienyeji kutafuta dawa ya kukabiliana na hali hiyo.

Wachungaji hufanya maombi huku wengine wakiwekewa dawa za kutapika ili waachane na ulevi.

Hata hivyo, mara nyingi tunaambiwa juhudi hizo hugonga mwamba kwa sababu wengi huwa wanahirisha tu na baadaye hurudi kule kule.

Kutokana na uraibu, inaelezwa kuna waliokatisha masomo, kuachishwa kazi, kufukuzwa shule, kupoteza maisha au kupata ulemavu wa kudumu kutokana na matumizi ya pombe na hapo ndipo jina la pombe ni mwanaharamu au shetani, hutawala.

Mtaalamu mshauri wa masuala ya afya, Festo Ngadaya anasema yapo makundi matatu ya wanywaji wa pombe, mosi watu wanaojiibia kunywa, wanaokunywa kawaida bila kupata madhara na kundi la mwisho ni la watu wenye uraibu.

Anasema kundi la kwanza la wanywaji, wanaweza kuachishwa kupitia hamasa mbalimbali ya kupewa elimu na wanapoacha hakuna madhara watakayopata.

Kundi la pili ni watu wanaohitaji kupewa elimu kwa muda juu ya madhara ya pombe kwa afya yao.

“Kundi la tatu ni la wenye uraibu, hapa yapo mambo magumu ambayo mnywaji hupitia, hivyo huwezi kumuachisha kwa kumtishia, lazima ujenge naye ukaribu na akuamini ili akueleze changamoto aliyonayo ndipo uanze kumshauri apunguze idadi ya chupa anazotumia kila siku na hata kufikia chupa moja,” anasema.

Ngadaya anasema mtu anapofikisha chupa moja anaweza kupitisha siku moja bila kunywa, siku mbili hadi wiki na hatimaye kuacha kabisa akisisitiza uangalizi mkubwa unahitajika.

Naye Dk Rajab Mlaluko anataja njia nyingine ya mtu kuepukana na matumizi ya pombe, ni kuachana na makundi yanayotumia vilevi ili kuepuka vishawishi.

“Kama unatumia pombe kupita kiasi, nenda kwa wataalamu wa afya ya akili kupata msaada wa kisaikolojia na dawa ya kuacha pombe, hatushauri mtu aliyetumia pombe kwa muda mrefu kuacha ghafla bila ushauri wa wataalamu, ni hatari,” anasema Dk Mlaluko.

Mtaalamu wa Saikolojia, Ramadhani Masenga anasema kuacha pombe si jambo rahisi kwa sababu ubongo hupenda kushika vitu ambavyo imevizoea, hivyo mtu anayetaka kuacha lazima akubali kupitia maumivu.

“Lazima ukubali kuachana na aina ya marafiki ulionao sababu aina ya watu waliokuzunguka wana mchango mkubwa wa ulevi ulionao,” anaeleza na kufafanua kuwa mtu anapokuwa na watu wapya waliomzunguka ubongo hutengeneza seli mpya za kufikiria na kutenda.

Pili, anasema lazima mtu anayeacha pombe atafute mbadala wa faraja yake.

“Mtu anapokunywa pombe kuna faraja anaipata, sasa anapoacha ni kitu gani kitamfanya ajisikie vizuri, lazima ajihusishe na marafiki ambao atakuwa nao kwenye vitu vya kumjenga, mfano mazoezi, kusoma au kufanya shughuli itakayomfanya asitafute pombe,” anaeleza.

Anasisitiza kuwa ubongo wenye upweke ni nyumba ya ibilisi hivyo mtu anayetaka kuacha pombe anapokaa peke yake atarudia kutumia vile vitu alivyoacha.

Hii ni kutokana na sumu iliyojitengeneza mwilini ikitokana na pombe ambayo humsukuma mtu kuwa na uhitaji mkubwa wa kunywa, ndio maana anasisitiza kuamua kuacha pombe kuambatane na kujishughulisha.

“Kama mtu amekuwa mraibu wa kupindukia kwa maana kwamba pombe anazokunywa ni chupa nane na kuendelea ni lazima aanze kupunguza kidogo kidogo akijua msukumo wowote anaoupata wa kurudia pombe ni jambo la kawaida na anapaswa aishinde,” anaeleza.

Masenga anasema mtu anayeacha kunywa pombe lazima atambue kuwa anaacha kwa sababu ya afya yake, heshima na thamani yake.

“Binadamu lazima awe na uwezo wa kuongoza hisia zake unaposhindwa kudhibiti hisia zako unakuwa mtumwa,” anaeleza.

Akielezea utegemezi wa pombe kiakili, daktari wa magonjwa ya akili Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mbeya Dk Raymond Mgeni anasema mtu anapokuwa mraibu maana yake matumizi ya pombe yanaingilia shughuli zake za kila siku hivyo hawezi kufanya kazi bila kutumia.

Kutokana na hali hiyo, Dk Mgeni anasema mfumo wa maamuzi wa mtu huathirika, kupitia migogoro ya kifamilia na hata kufukuzwa kazi. “Mtu anapokuwa mraibu anapata magonjwa ya akili kiwemo maruerue, utendaji wake kuwa na mashaka, kuvua nguo, kujisaidia na hata kuchanganyikiwa,” anasema Dk Mgeni.

Dk Mgeni anasema mtu anaanza kunywa pombe kutokana na uchungu anaoupitia, starehe au majaribio kwenye maisha akitolea mfano vijana balehe na mtu huanza kunywa kidogo kidogo mpaka mwili kutengeneza utegemezi.

Anasisitiza kuwa uraibu mmoja unatengeneza mwingine ambapo mtu anayekunywa pombe ataanza kuvuta sigara, shisha, bangi na hatimaye dawa za kulevya.

Dk Ernest Winchislaus kutoka Idara ya mafunzo na utafiti wa magonjwa ya ndani Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya anasema pombe inaathiri vibaya ini na kusababisha magonjwa kupungua kwa uwezo wa ini kufanya kazi, mafuta kujikusanya kwenye ini na uvimbe wa ini.

“Magonjwa haya yanaweza kusababisha uharibifu mkubwa wa ini na kuhatarisha maisha ini linaposhindwa kufanya kazi yake ya kuchuja sumu mbalimbali mwilini,” anasema.

Anasema unywaji wa pombe kupita kiasi husababisha ongezeko la shinikizo la damu na kiharusi, kupanuka kwa mishipa ya damu, ambayo inaweza kusababisha matatizo ya moyo.

Shida nyingine anayoitaja Dk Winchislaus ni saratani ambayo anasisitiza upo ushahidi unaoonyesha matumizi ya pombe kupita kiasi huhusiana na hatari ya kuendeleza aina tofauti za saratani kama vile ya koo, ini, matumbo na matiti.

Akinukuu Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) Dk Winchislaus anasema kiasi Kilichopendekezwa cha matumizi ya pombe ni tofauti kwa wanaume na wanawake.

“Kwa wanaume, inapendekezwa kunywa hadi uniti kwa siku, wakati kwa wanawake ni unit moja tu. Unit moja ya pombe ina takriban mililita 14 ya pombe ngumu, sawa na glasi moja ya divai, kikombe kimoja cha bia au shoti,” anasema Dk Winchislaus.

Aisha Juma (27) mkazi wa Tabata Dar es Salaam tayari amekatisha masomo ya Chuo Kikuu kutokana na unywaji wa pombe.

“Nilianza kunywa pombe mwaka wa kwanza nikiwa Chuo Kikuu mwaka 2018 na huko nilihudhuria klabu na kumbi mbalimbali za starehe, nilikuwa na kundi sogozi la what’sApp kujumuisha marafiki zangu ambao wote tunalewa,” anasimulia.

Upatikanaji wa fedha kwake haukuwa mgumu kutokana na fedha ya mkopo wa masomo. Urafiki wake na pombe ulimfanya kuacha kula ili mradi fedha hizo azielekeze kwenye vinywaji vikali ambavyo vilikatisha ndoto ya elimu yake.

“Niliacha chuo sababu nilitumia muda mwingi kulewa sikuwa na uwezo wa kuamka mapema asubuhi, ninapoamka jioni rafiki zangu wananipigia na kunielekeza ni wapi tukutane kuendeleza unywaji,” anasema.

Aisha anasema hakuna mwanafamilia aliyejua ulevi wake bali kuanguka kimasomo, walimtaka aendelee lakini hakuafiki, baadaye alikosa fedha za pombe na ndipo marafiki walimtenga. Alipiga mnada samani za ndani na kwenda kuishi kwa rafiki naye alimchoka.

Anasema alijaribu njia zote bila mafanikio na baadaye ilibidi arudi nyumbani.

Mchungaji Elieth Mtaita wa Mkoa wa Kilimanjaro anasema suala la unywaji wa pombe ni tatizo kubwa linalotokana kukosa malezi pamoja na ujinga wa mtu.

“Tatizo ambalo sisi viongozi wa dini tunakutana nalo mara kwa mara ni watu kupandikizwa roho ambayo humfanya mtu kujiona mahitaji yake pekee ni pombe,” anasema.

Anasema jamii inapaswa kuanza kusimamia malezi ya watoto kikamilifu na hata kupitia masomo ya sayansi ni muhimu elimu ya madhara ya pombe ikatolewa mapema.

Related Posts