Mwisho wa tambo kwa mashabiki wa Yanga na Simba ambao kila mmoja anavutia ushindi upande wake ni Jumamosi kwenye uwanja wa Benjamini Mkapa ambapo hii itakuwa ni nafasi kwa Mnyama kulipiza kisasi cha mzunguko wa kwanza au Wananchi kuendeleza ubabe katika mchezo huo wa dabi.
Tofauti na ilivyokuwa katika mchezo wa mzunguko wa kwanza, Simba na Yanga zinakutana safari hii huku kila mmoja akiwa na maumivu ya kutolewa kwao katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, pamoja na hayo wekundu wa Msimbazi pia walitolewa na Mashujaa katika kombe la Shirikisho (FA) kwa mikwaju ya penalti (6-5) baada ya sare ya bao 1-1.
Ni kweli kuwa Simba haijashinda katika michezo yake minne iliyopita, wametoa sare moja dhidi ya Ihefu na kupoteza tatu dhidi ya Al Ahly nyumbani (1-0) na ugenini (2-0) na Mashujaa (p6-5) katika mashindano yote huku Yanga ikishinda mechi mbili dhidi ya Singida BS (3-0), Dodoma Jiji (2-0) na kutoa suluhu moja dhidi ya Mamelod nyumbani na kupoteza kwa penalti ugenini (3-2) baada ya kutoka tena suluhu katika dakika 90 za Afrika Kusini.
Pamoja na yote hayo huku kila mmoja akiongea lake kuhusu dabi hawa hapa wachezaji ambao wanaweza kunogesha utamu wa mchezo huo kwa kuongeza wigo wa machaguo katika vikosi vyao vya kwanza.
Hapa tunaongelea wachezaji ambao hakuna ambaye pengine anawapigia hesabu kuanza katika mchezo huo lakini makocha wa timu hizo,Migue Gamondi kwa Yanga na Abdelhak Benchikha wanaweza kutushangaza kwa kufanya mabadiliko ‘rotation’ ambayo mara nyingi hujikita katika mpango wa kimbinu.
AUGUSTINE OKRAH
Sio aina ya wachezaji ambao wanaimbwa sana katika kikosi cha Yanga lakini kila ambapo amekuwa akipata nafasi amekuwa akionyesha utofauti, kiasi na maarifa aliyonayo vinaweza kumfanya Gamondi kufikiria kuanza naye au kumuingiza kipindi cha pili kwa ajili ya kuongeza nguvu.
Kasi aliyonayo Okrah kwa mpango wa kutaka timu ishambulie zaidi kupitia pembeni tena kwa kustukiza, anaweza kuwa na madhara kiasi cha kuwafanya mabeki wa pembeni wa Simba, Shomary Kapombe au Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ kushindwa kuwa huru na kupandisha nao mashambulizi.
MZAMIRU YASSIN
Mara nyingi amekuwa akitumika kama mbadala baada ya kuchemka kwa mmoja kati ya Babacar Sarr, Fabrice Ngoma au Sadio Kanoute, kiungo huyo punda ambaye alikuwa chaguo la kwanza mbele ya Robertinho anaweza kuwa mmoja wa wachezaji kwa Simba ambaye lolote linaweza kutokea.
Kwanini? kufanya makosa kwa Sarr ambayo yamekuwa yakiigharimu Simba hivi karibuni kunaweza kumfanya Benchikha kutafuta mbinu mbadala ya kufauta ustawi katika eneo lake la kiungo cha chini ambalo kwa sasa lionekana kuwa dhaifu.
KIBWANA SHOMARY
Hivi karibu imekuwa ikimbidi kocha wa Yanga, Miguel Gamondi kumtumia beki wake wa kati Dickson Job upande wa kulia kutokana na kusumbuliwa na majeraha kwa wachezaji wake wawili, Kouassi Attohoula Yao na Kibwana Shomary.
Yao haonekani kuwa tayari kwa mchezo wa dabi kutokana na aina ya majeraha ambayo aliyapata lakini kwa Kibwana anaonekana kuwa tayari na ndo maana alikuwa sehemu ya mchezo dhidi ya Singida BS japo hakuanza.
ISRAEL MWENDA
Kama kocha wa Simba,Abdelhak Benchikha atahitaji uzoefu basi anaweza kuanza na Shomary Kapombe lakini akihitaji nishati ya mchezaji ambaye anaweza kukimbia muda wote wa mchezo katika kuzui basi anaweza kutushangaza kwa kuanza na Israel Mwenda ambaye ni mzuri zaidi katika kulinda.
Mwenda anaifanya Simba kuwa na machaguo zaidi katika upande wa beki ya kulia, licha ya kuwa na uwezo pia wa kucheza kushoto.
PACOME ZOUZOUA
Hajaonekana katika michezo minne iliyopita kwa Yanga katika mashindano yote, ni miongoni mwa wachezaji hatari mno katika safu ya ushambuliaji ya Wananchi kukosekana kwake kumetokana na majeraha ambayo aliyapata katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam FC, Machi 17.
Zouzoua anaweza kuongeza makali katika safu ya ushambuliaji ya Yanga ambayo imefunga mabao matano katika michezo miwili iliyopita.
PA OMARY JOBE
Kocha wa Simba, Abdelhak Benchikha anaweza kufikiria kufanya mabadiliko katika eneo lake la mwisho la ushambuliaji ambalo hivi karibuni alitumika zaidi Freddy Michael ‘Funga Funga’ ambaye alishindwa kuonyesha makali yake miongoni mwa wachezaji ambao wanaweza kuachiwa msala ni pamoja Pa Omar Jobe.