Kauli ya ‘tutawapoteza’ ya kigogo UVCCM moto

Mwanza/Kagera. Kauli ya Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Faris Buruhan ya kulitaka Jeshi la Polisi kutowatafuta vijana wanaotukana viongozi mtandaoni pindi watakapokuwa wamepotezwa, imezuia mjadala baada ya watu kuanza kukumbushia waliopotea kusipojulikana.

Aprili 16, 2024, akizungumza na viongozi pamoja na vijana wakati wa ziara yake katika mji mdogo wa Rulenge Ngara mkoani Kagera, Buruhan alisema:“Kama kuna mtu anadhani anao uhuru wa kukaa mtandaoni na kisimu chake anashinda asubuhi kutwa nzima anatukana viongozi, Jeshi la Polisi hawa tukiwapoteza msiwatafute.”

Hata hivyo, jana jioni Jumatano, Aprili 17, 2024 baada ya Buruhan kutoa kauli hiyo na kusambaa kwa kasi mitandaoni na kuibua mijadala mikali, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi akiwa kwenye mkutano wa hadhara jijini Mbeya alikosoa kauli hiyo akisema:

“Leo akiinuka kijana wa CCM kwa mfano, akasema wapinzani wetu wakifanya hivi na hivi lazima tuwapoteze, huyu ni kijana wetu lakini kasema jambo la kijinga tutalipinga na lazima tuone ni lakijinga kwa sababu mwisho wa siku nchi hii ni yetu sote.”

Licha ya Dk Nchimbi kuipinga kauli hiyo, kumekuwa na hisia ya kauli za chuki zinazotolewa na CCM, huku pia kukiwa na kumbukumbu za watu waliopotea na wengine kudaiwa kutekwa katika mazingira ya kutatanisha.

Mwananchi Digital limemtafuta Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kujua hatua alizozichukua dhidi ya kauli hiyo amesema ameona kipande hicho cha video kinachomuonesha Buruhan akitoa kauli hiyo akidai wanafanyia kazi.

“Nimeiona, nashukuru wewe si wa kwanza kunitumia na tunaifanyia kazi,” alisema Jaji Mtungi

Miongoni mwa watu waliopotea ndani ya kipindi cha miaka 10 iliyopita ni pamoja na aliyekuwa Diwani wa Kibondo, Simon Kangoye aliyetoweka mwaka 2017, Mwandishi wa Mwananchi, Azory Gwanda aliyechukuliwa na watu wasiojulikana mwaka 2017 pamoja na aliyekuwa mkuu wa Idara ya Sera na Utafiti wa Chadema, Ben Saanane aliyetoweka mwaka 2017.

Mwaka 2023 matukio ya watu kutoweka kwenye mazingira ya kutatanisha yalijirudia likiwamo tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara, Mussa Mziba (37) aliyekuwa akimiliki Kampuni ya Mziba Empire Investment Ltd yenye ofisi zake Mikocheni, Dar es Salaam.

Pia, Desemba 28, 2023 ndugu wawili mkoani Singida, Juma Iddi (45) na Haruna Iddi (50) waliotoweka, saa 10 jioni katika maeneo tofauti ya Mwenge na Mghanga, mjini Singida huku, Charles Wetinyi akidaiwa kukamatwa na watu waliojitambulisha kuwa polisi, eneo la Mugumu wilayani Serengeti Mkoa wa Mara Oktoba 23, 2023.

Wengine ni aliyekuwa mfanyabiashara na fundi simu eneo la Kariakoo Dar es Salaam, Innocent Elias Liveti (34) aliyetoweka Desemba Mosi, 2023.

Wengine ni vijana waliokuwa mafundi simu Kariakoo Dar es Salaam, Tawfiq Mohamed, Self Swala, Edwin Kunambi, Hemed Abass na Rajabu Mdoe, waliotoweka Desemba 2021 baada ya kukamatwa na watu waliodhaniwa kuwa ni polisi na kupelekwa kusikojulikana.

Buruhan azungumzia kauli yake

Leo, Mwananchi Digital ilimtafuta Buruhan juu ya kauli yake kuibua mijadala na kukemewa na Dk Nchimbi aliyesema:“Sisi umoja wa vijana wa UVCCM ndiyo jumuiya pekee ambayo ina watu wanaojifunza uongozi na kila siku tunaamini katika kukosea na kuanza upya.”

Amesema amepokea maelekezo ya Katibu Mkuu Dk Nchimbi yawe hasi au chanya.

“Kiongozi mkuu wa chama, akishakuwa amelitolea ufafanuzi wa kukemea haijalishi ulipatia au ulikosea sisi uwa tunatii na kupokea maelekezo ya kuendelea na kazi.

Akifafanua kauli yake, Buruhan amesema kupoteza mtu kunaweza kukawa na tafsiri pana sana.

“Mtu anaweza kupotezwa kisiasa, mtu anaweza akapotezwa kwenye uongozi kwa hiyo hiyo tafsiri pana na ukienda kuangalia kupoteza kuna maana gani ni kitu cha kawaida ambacho kina tafsiri nyingi sana siyo jambo ambalo unaweza kusema ni kubwa.

“Jambo watu wanatakiwa kulijua nilikuwa katika kukemea matumizi mabaya ya mitandao, kukemea lugha mbaya za matusi kwa viongozi wetu, kuonyesha kwamba sisi kama umoja wa vijana hatukubaliani na kauli hizo,” alisema.

Sheikh Ponda, ACT-Wazalendo

Katika ukurasa wake wa X (zamani Twitter) wa Katibu Mkuu wa Shura ya Maimamu, Sheikh Ponda Issa leo Alhamisi ameweka picha ya mwenyekiti huyo wa vijana Kagera pamoja na watu mbalimbali waliopotea wakiwemo Azory Gwanda, Ben Sanane.

Picha hizi zimeambatana na ujumbe ameuandika: “Toka 2013-2024, watu wanatekwa na kupotezwa. 2023, Shura ya Maimamu ilitoa ripoti ya uchunguzi. Katika ripoti hiyo jumla raia 236, wametekwa na kupotezwa. Kauli ya CCM “hawa tukiwapoteza msiwatafute” inawafanya watuhumiwa Na.1. Kama Taifa linajali uhai wa raia Dola ichukue hatua.”

Kauli hiyo imeiibua Ngome ya ACT-Wazalendo na kulitaka Jeshi la Polisi limchukulie hatua kali mwenyekiti huyo wa UVCCM.

“Ngome ya vijana tunaichukulia kauli hii kama tishio na tangazo la vita dhidi ya wakosoaji wa Serikali na wa viongozi wa umma jambo ambalo Jeshi la Polisi na Watanzania hasa vijana hatupaswi kulifumbia macho hata kidogo,” amesema Philbert Macheyeki, Katibu Mwenezi Ngome ya Vijana wa chama hicho.

Kupitia taarifa kwa umma ya Macheyeki imesema kauli hiyo inahatarisha amani na inakwenda kinyume na Sheria na Katiba ya Jamuhuri ya Muungano ibara ya 14 na 18 zinazotoa haki na uhuru wa kuishi na kutoa maoni bila kubughudhiwa.

“Kutokana na kauli za vitisho zilizotolewa na kiongozi huyo wa UVCCM Mkoa wa Kagera; Ngome ya vijana tunalitaka Jeshi la Polisi kumkamata mara moja na kumfikisha katika vyombo vya dola ili sheria ichukue mkondo wake kwani kumuacha aendelee kuwa mtaani tafsiri yake Serikali na chama chake kinaunga mkono kauli zake za vitisho na uvunjifu wa amani alizozitoa hadharani,” amesema.

Pili, ngome hiyo ya vijana ilimsihi Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ni mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi kutoa maelekezo kwa Katibu Mkuu wa CCM: “Kumchukulia hatua za kinidhamu Faris Buruhan ili iwe fundisho kwa vijana wengine wa chama hicho ambao wamekuwa wakitoa kauli za vitisho, kutugawa na kuhatarisha amani ya nchi.”

Kufuatia kauli hiyo, Kamanda wa Polisi mkoani kagera, Blasius Chatanda japokuwa hajaiona video hiyo inayosambaa mtandaoni, lakini suala la kutoa elimu linaweza kufanywa na mtu yeyote ilimradi lifanyike kwa nia njema.

“Pia, sisi kama jeshi tunafanya kazi kwa mujibu wa sheria, mtu akizungumza jambo kimsingi halipo kisheria lina muelekeo wa kijinai tunachukua hatua dhidi yake, lakini likiwa na muelekeo wa kimadai tunachuka hatua maana yake tutamshauri muhusika afungue mashauri ya madai mahakamani

“Kwa mfano, linaweza kuwa jinai kwa sababu mtu katumia lugha ya matusi au vitisho,” amesema Chatanda.

Akizungumzia kauli hiyo, Ofisa wa sheria katika Chemba ya mawakili Rwela iliyopo mkoani Mbeya, Hendrick Bundala amesema licha ya Katiba kutoa uhuru wa kuzungumza lakini imemnyima kuongea huko kusiwe kunaingilia uhuru wa mtu mwingine.

“Kwanza kikatiba kuanzia ibara ya 11 hadi ya 15 inaruhusu Mtanzania yeyote na inampa uhuru wa kuongea isipokuwa maongezi yake yasiwe yanaingiliana na uhuru wa mtu mwingine, kama mtu amekosa vipo vyombo vya sheria na polisi ndio wenye mamlaka ya kufanya uchunguzi wa mhusika kwa kumhoji,” amesema.

Kwa upande wake, mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Lenin Kasoga amesema kauli ya mwenyekiti huyo wa UVCCM ni ya kichochezi na kwamba kama ingetolewa na kada wa upinzani ingekuwaje?

“Sidhani kwamba hiyo amri imetoka juu nadhani ni mambo yake tu mwenyewe haiwezi kuwa imetoka kwa Dk Nchimbi au kwa viongozi wengine. Kauli kama hizo ni kauli za uchochezi sasa akiongea hizo na watu wa Chadema watasemaje,” amehoji Kasoga.

“Nchi hii tangu uongozi wa Mwalimu Nyerere imejengwa na misingi ya amani, utulivu na sio kwamba waonevu hawapo wapo na wanapokuwepo watu hawasemi, kuna vijana ambao wanataka kufanya uonevu…huo sasa ndio ulevi wa madaraka na ubinafsi.”

Naye mchambuzi wa Masuala ya Kisiasa na Kijamii mkoani Mwanza, Richard Mshilimu amesema viongozi lazima wakubaliane kuwa kiongozi sio kuzungumza kila kitu. 

“Kuna wakati lazima tukubaliane kuwa kiongozi au kupata nafasi kwenye chama cha siasa sio kwamba unaweza kuzungumza kila kitu, ni lazima kuwe na mipaka.

“Kauli ya kiongozi huyu kutoka kwenye jumuiya yenye nguvu inaleta tafsiri ya kwamba hata wakubwa wake wanajua anachozungumza na hii inaleta ukakasi kidogo kuhusu hizi kauli,” amesema Mshilimu.  

Buruhan si kiongozi wa kwanza wa UVCCM kutoa kauli za vitisho kama hizo. Mwaka 2019 Katibu wa UVCCM Kata ya Sandali wilayani Temeke jijini Dar es Salaam, Mrisho Kamba alilitaka Jeshi la Polisi kuwaacha ili wawapige wanaomkosoa Rais (hayati John Magufuli).

“Katika kitu ambacho vijana tunaumia, ni mambo ya polisi. Tunawaona wapinzani wanamtukana Mheshimiwa Rais. wanambeza mheshimiwa Rais, lakini pia tuna uwezo wa kuwapiga, tunaogopa polisi.  

 “Mimi nikuombe kamwambie mheshimiwa Rais, maaskari watuache, mtu akimbeza mheshimiwa Rais, tunatakiwa tumpige, mtu akimbeza Rais tunatakiwa tumburuze, mtu akimkashifu mheshimiwa Rais sisi tunatakiwa tumkatekate. Hayo mambo ya polisi, sisi watuache tumsifie mheshimiwa Rais kazi anayofanya ni kubwa.”

Kauli nyingine iliwahi kutolewa na mwanaharakati anayetambulika kwa jina la Cyprian Musiba ambaye Mei 30, 2019 alinukuliwa kwenye mtandao wa Youtube akiwaonya  wanaomkosoa Rais kwenye mitandao ya jamii.  

 “Hii nchi ukipotea wewe, milioni 54 (idadi ya Watanzania) wakawa salama hamna tatizo, hata kwenye vitabu vya dini imeandikwa. Wale wote waliokuwa wanaleta shida, hata ukisoma Biblia, Q’uran imo. Toa wawili kafara 100 wapone. Sasa kuweni makini kumtukana Rais, ni kiongozi mkubwa kweli,” alisema Musiba.

Kauli nyingine iliwahi kutolewa na aliyekuwa Mwenyekiti wa UVCCM, Kheri James ambaye sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Iringa, alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara mkoani Arusha akisema, “wewe unashindana na watu unawaambia, safari hii wasiponitangaza kitaeleweka, nakwambai safari hii, safari hii, hiii! Wajaze upepo, endelea kuwajaza upepo. Wala hatutumii nguvu kubwa, ni sindano pyuu!” alisema James.

Related Posts