Mambo 3 yanaibeba Yanga SC

JUMAMOSI ya wiki hii, inapigwa Kariakoo Dabi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Yanga itakuwa mwenyeji wa Simba ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Bara.

Kuanzia saa 11:00 jioni, ndiyo mchezo huo unatarajiwa kufanyika na kila upande unazihitaji alama tatu ili kujiwekea mazingira mazuri kunako ligi hiyo inayoelekea ukingoni.

Yanga na Simba kila mmoja ameutolea macho mchezo huo, huku wakisema pointi tatu zitakuwa na maana kubwa sana kwa atakayezipata.

Ukiangalia kuelekea mchezo huo, Yanga wanatajwa ndiyo wenye nafasi kubwa ya kushinda kulingana na rekodi zake zilivyo kulinganisha na Simba.

Rekodi hizo ni za Ligi Kuu Bara katika msimu huu na hapa Mwanaspoti linakuchambulia mambo matatu yanayoibeba Yanga kwenye mchezo huo ukizingatia imekuwa na matokeo ya kushtua sana.

Kabla ya kwenda mbali sana, Yanga msimu huu imekuwa ikitoa vipigo vizito kwa wapinzani wake katika michuano yote, jambo linalowafikirisha wengi pengine dozi hiyo itaendelea.

Ndani ya Ligi Kuu Bara pekee, ni mara tano imeibuka na ushindi wa mabao kuanzia manne, miongoni mwa waliokutana na mvua hiyo ya mabao ni Simba katika mchezo uliochezwa Novemba 5, 2023.

Mbali na Ligi Kuu, pia katika Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la FA, pia imegawa sana dozi kitu ambacho kinaitofautisha Yanga na timu zingine linapokuja suala la kusaka matokeo chanya.

Jumla ikiwa ni katika mechi tisa Yanga imegawa dozi ya maana, huku yenyewe ikiwa haijaruhusu kufungwa zaidi ya mabao matatu.

Ni mara moja pekee imepoteza mechi kwa mabao 3-0, ilikuwa Ligi ya Mabingwa Afrika ugenini dhidi ya CAR Belouizdad, huku zingine ikipoteza kwa mabao mawili kushuka chini.

Mechi ambazo Yanga ilifunga mabao mengi Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu walipoishia robo fainali ni; Yanga 5-1 Djibouti Telecom na Yanga 4–0 CR Belouizdad. Ukija katika Kombe la FA, ilikuwa hivi; Yanga 5-1 Hausung na Yanga 5-0 Polisi Tanzania.

Ndani ya Ligi Kuu, mambo yapo hivi; Yanga 5-0 KMC, Yanga 5-0 JKT Tanzania, Simba 1-5 Yanga, Yanga 4-1 Mtibwa na Yanga 5-0 Ihefu.

Yanga ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara na ndiyo mabingwa wa kihistoria wa taji hilo waliloshinda mara 29, Simba yenyewe imelichukua mara 22.

Ally Kamwe ambaye ni Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, amebainisha msimu huu malengo yao ni kutetea mataji yao, hivyo wanazicheza mechi zao kwa ajili ya kufanikisha jambo hilo.

“Sisi ndiyo mabingwa watetezi, tunawaheshimu wapinzani wetu tunaokwenda kucheza nao katika Kariakoo Dabi.

“Wengi wanawaona Simba ni timu dhaifu, lakini sisi tunawaona ni washindani wetu wakubwa, hivyo tutaingia kwa kuwaheshimu.

“Lakini mbali na hayo yote, tunahitaji kufikia malengo yetu ya msimu huu ambayo ni kutetea ubingwa, hatuwezi kutetea ubingwa kama tukidondosha ovyo pointi, lazima tushinde mechi zote zilizo mbele yetu bila ya kuangalia mpinzani gani tunakutana naye,” alisema Kamwe.

Kutokana na ishu hiyo ya njaa ya mafanikio, ndiyo inatoa taswira ya upambanaji kwa wachezaji wa Yanga kila wanaposhuka dimbani.

Ndani ya kikosi cha Yanga, safu yao ya ulinzi inaongoza kwa kuwa na ukuta mgumu sana kupitika, lakini pia ushambuliaji moto unawashwa si kitoto.

Timu hiyo ikiwa imeruhusu mabao 11 katika mechi 21, wakati wapinzani wao Simba, wakiruhusu 19 baada ya mechi 20.

Yanga wapo vizuri katika kucheka na nyavu, wachezaji wake tofauti wana mabao mengi na Stephane Aziz Ki amefunga 14, Maxi Nzengeli (9), Mudathir Yahya (8) na Pacôme Zouzoua (7). Hao ni wale wanaofuatana kwa ukaribu sana.

Yanga katika ishu ya kufunga mabao, ina wastani wa kufunga mabao (3) kila mechi, huku Aziz Ki ndiye kinara, wakati Simba wastani wao wa kufunga bao kila mechi ukiwa ni (2), kinara wao ni Saidi Ntibazonkiza na Clatous Chama ambao kila mmoja anayo 7.

Katika mechi 21 walizocheza Yanga, wameshinda 18, ndiyo timu iliyoshinda mechi nyingi zaidi ya zote zinazoshiriki ligi hiyo. Pia ina sare 1 na kupoteza mbili.

Kwa namna kikosi cha Yanga kilivyo hivi sasa, Kocha Miguel Gamondi ametengeneza kitu kinachowafanya wasiwe wanamtegemea mtu mmoja kuwapa matokeo chanya kwenye mechi zao.

Wakati mwingine anaweza kukosekana mchezaji muhimu wa kikosi cha kwanza, lakini akaibuliwa yule anayekaa benchi sana au asiyepata nafasi kabisa, akaja kuwashangaza.

Tumeshuhudia hiyo kwenye mechi mbili za robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu walipocheza dhidi ya Mamelodi Sundowns ambapo Yanga iliwakosa Pacome Zouzoua, Yao Attohoula na Khalid Aucho.

Licha ya Yanga haikufanikiwa kusonga mbele kwenye michuano hiyo kutokana na kuondolewa kwa penalti 3-2, baada ya mechi zote kumalizika kwa matokeo ya 0-0, lakini hakuna kilichoharibika ndani ya uwanja.

Jonas Mkude alicheza eneo la kiungo mkabaji anapocheza Khalid Aucho na kufanya vizuri akishirikiana na Mudathir Yahya. Kule kwa Yao, alikuwepo Dickson Job ambaye mara nyingi hukucheza beki wa kati, pia ana uwezo wa kucheza beki wa kulia anapocheza Yao.

Kuhusu hilo, aliyewahi kuwa mchezaji na kocha wa Simba, Abdallah Kibadeni, amesema: “Yanga msimu huu wana kikosi kilichokamilika, ukiangalia hivi karibuni wamecheza mechi mbili dhidi ya Mamelodi katika michuano ya kimataifa bila ya wachezaji wao muhimu, lakini kila mmoja ameona nini kilitokea, ndiyo maana nasema Yanga wamekamilika, wana kikosi ambacho akikosekana mtu fulani, inakuwa kama vile hakijatokea kitu.”

Related Posts