Dar es Salaam. Chakula ni muhimu kwa afya njema na kuna misingi inatakiwa kufuatwa ili kuepukana na madhara yatakayosababishwa baada ya kula chakula.
Wataalamu wanaelezea mambo saba ya kuzingatia baada ya kula chakula ili kuepuka muingiliano wa virutubisho vinavyopatikana kwenye chakula na changamoto zinazoweza kusababisha maradhi.
Daktari wa binadamu, Erick Shayo anasema Watanzania hawana utamaduni wa kula na kusubiri ili chakula kifanyiwe mmeng’enyo, badala yake hula au kunywa vitu vinavyoingilia mmeng’enyo huo au kuvuta tumbaku.
Dk Shayo anasema wapo vijana na wazee ambao starehe yao ni uvutaji wa sigara au shisha na wanafanya hivyo baada ya kula, wakishushia kama kinywaji ambacho kinawapa burudani.
“Dhahiri kuwa sigara ina madhara kiafya kwa ujumla hivyo watu wanashauriwa kuacha kutumia lakini inaelezwa kuwa madhara yake huongezeka pale inapotumika mara baada ya kula chakula,” anasema Dk Shayo.
Anasema utafiti wa kimaabara unaonesha kuwa uvutaji wa sigara moja baada ya kula ni sawa na mtu aliyevuta sigara 10 hivyo hatari ya kupata saratani huongezeka.
Wapo watu baada ya kula wanakwenda kulala ambapo anasema hili ni kosa kiafya kwani inakuwa ngumu chakula kilicholiwa kusagika sawasawa na inaweza kusababisha vidonda vya tumbo na magonjwa mengine ya kuambukiza kwenye utumbo mdogo.
Dk Shayo anasema hilo linatengenezwa kwa watoto kwa kuwahimiza kula, kuoga na kwenda kulala ili waweze kupumzika lakini wanatengenezewa madhara makubwa ya kiafya bila kujua.
“Kuruhusu hili ndipo tunakutana na matokeo ya watoto kutokewa na chakula kwenye pua, kupaliwa na wakati mwingine kutapika kwa sababu hakupewa muda wa kusubiri chakula kimeng’enywe,” anasema.
Pia, anasema ni rahisi kupata kiungulia kutokana na tindikali ya tumboni kuhama kwa njia isiyo sahihi na kulazimisha kurudi kwenye umio, ili kuzuia hali hii inatakiwa kulala saa tatu baada ya kula.
Anasema kiafya haishauriwi kula matunda baada ya mlo, kwani ulaji huo hufanya tumbo kujaa hewa na matokeo yake kusababisha gesi tumboni.
Usahihi ni kula matunda saa moja au mbili kabla au baada ya kula chakula, ambapo kula matunda muda mfupi mara baada ya kula chakula ni kosa ambalo linafanywa na watu wengi na huonekana ni sawa.
Kumekuwa na tabia kwa baadhi ya watu kunywa chai baada ya kula chakula, iwe mchana au usiku hivyo haitakiwi kunywa chai kwa mujibu wa utafiti kwani majani ya chai yana kiwango kikubwa cha tindikali ‘acid’.
Hata hivyo majani hayohayo yana kemikali kadhaa ambazo huingilia ufyonzwaji wa madini muhimu na virutubishi vilivyopo katika chakula, kama ilivyo kafein inayopatikana katika soda za cola.
“Mtu anapokunywa chai, tindikali hiyo hufanya protini iliyo kwenye chakula kilicholiwa kuwa kigumu na kutosagika haraka tumboni na matokeo yake ni kukosa choo kwa siku kadhaa,” anasema Dk Shao.
Anasema endapo mtu amevaa nguo ya kuvalia mkanda hapashwi kufungua baada ya kula kwani ni jambo la hatari kwa mustakabali wa afya.
Baada ya kula haitakiwi kulegeza mkanda wa suruali, hivyo inapaswa kuachwa kama ulivyokuwa hapo awali kwani kufanya hivyo kunaweza kusababisha utumbo kujikunja na kuziba.
“Kuna vitu vinaweza kuzuilika ili kuepukana na madhara makubwa ambayo yanaweza kugharimu maisha kwa sababu ya kutokuzingata vitu vidogo vidogo ambavyo vinatolewa maelekezo na wataalamu wa afya,” anasema Dk Shayo.
Inaeleza kuwa mtu anapooga baada ya kula mtiririko wa damu huongezeka zaidi sehemu za mikono,miguu na mwili na kusababisha damu kupungua kwa sehemu za tumboni.
Hivyo damu inapopungua tumboni maana yake ni kudhoofika kwa mfumo wa usagaji chakula tumboni.
“Mwili unahitaji nishati na mtiririko mzuri wa damu kwenye tumbo kwa usagaji chakula mzuri. Kuoga mara baada ya kula kunaweza kutatiza mchakato wa mwili kwenye mtiririko wa damu kwenye viungo ili kudhibiti halijoto,”
Hivyo anashauri kusubiri angalau kwa saa moja baada ya mlo kabla ya kuoga.
Anasema utafiti unaonesha kuwa kurandaranda mara baada ya kula husababisha mfumo wa usagaji wa chakula kukosa uwezo wa kunyonya virutubisho vilivyomo kwenye chakula, vinavyoliwa badala yake inatakiwa kutulia sehemu moja.
“Tunajua watu wanakazi nyingi za kufanya, hivyo hawana muda wa kupoteza kwa wale wanaojishughulisha mchana na ni ngumu kufuata eneo hili kwa sababu hana muda, lakini anaweza kufanya hivi wakati wa usiku,” anasema.
Hata hivyo wananchi wengi bado hawana uelewa wa kutosha, kama asemavyo Hans Mashaka mkazi wa Tabata.
“Naamini kama madhara yanatokea baadae yanaweza kunikuta, kwa sababu nikishakula sikai sehemu moja na wakati mwingine nikimaliza naendelea na kazi zangu kutokana na muda,” anasema Hans.
Mboni Kasani anasema, “Familia zetu zinahitaji kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja, tumeshakuwa na utaratibu wa kula na kuingia kuoga, unalala.”
Nassoro Razack anasema imekuwa ni mazoea kwake kuvuta sigara, “Nikimaliza kula chochote lazima nivute sigara hiyo inakuwa kama maji kwangu na ninajihisi vizuri.”