Dodoma. Mbunge wa Viti Maalumu Janeth Mahawanga amehoji iwapo Serikali haioni umuhimu wa kuwatafutia maeneo wanawake wenye watoto wadogo wajasiriamali wanaofanya biashara zao pembezoni mwa barabara wakati wakisubiri kuwatengea maeneo husika.
Akiuliza maswali ya nyongeza bungeni leo Ijumaa Aprili 19, 2024, Janeth pia amehoji lini Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kitatengeneza programu mahususi kwa ajili ya wajasiriamali wadogo.
Amependekeza programu hiyo iwalenge wajasiriamali ambao ni wanufaika wa mikopo ya Serikali ili fedha wanazokopeshwa zirudi kwa kuwekezwa sehemu sahihi.
Akijibu swali hilo kwa niaba ya Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Mipango na Uwezeshaji, Profesa Kitila Mkumbo, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe amesema wamekuwa wakihamasisha wakinamama na wengine ambao hawana maeneo ya kufanyia shughuli zao, waweze kufanya biashara katika maeneo ambayo ni salama.
“Lakini pia ni sahihi kulingana na ubora hasa kwenye chakula. Kituo cha Uwekezaji kinatoa vivutio maalumu hasa vikilenga wafanyabiashara wanawake na vijana,” amesema.
Amesema ndio maana kupitia programu ya kuwezesha wakinamama na vijana, Rais Samia Suluhu Hassan amekuja mpango huo kupitia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri nchini.
Amesema mpango huo utakua ni kichocheo ili wanawake wapate fursa kwenye biashara zao.
Katika swali la msingi Janeth amehoji ni lini Serikali itaanzisha utekelezaji wa mpango wake wa kuanzisha vituo vya masuala ya uwekezaji na masoko kwa wanawake kwa kila kata.
Akijibu swali hilo Kigahe amesema Serikali kupitia Mamlaka ya Maeneo Maalumu ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA), imetenga maeneo kwa ajili ya kuanzisha kanda maalumu za kiuchumi katika mikoa mbalimbali nchini.
Amesema lengo kuu la kuanzisha maeneo haya ni kuhamasisha uwekezaji wa viwanda vya kuongeza thamani mazao mbalimbali yanayozalishwa nchini, kukuza mauzo ya nje ya bidhaa za viwandani na pia kuzalisha bidhaa zinazoagizwa nje kwa soko la ndani.
Amesema ili kuendeleza maeneo hayo kuna sehemu zitatengwa kwa ajili ya wajasiriamali wadogo na wa kati (SME’s), wakiwemo wanawake na vijana ili waweze kuanzisha viwanda vya kuchakata na kutengeneza bidhaa mbalimbali kwa ajili ya soko la ndani na nje.
Aidha, amesema maeneo haya yatatumika kama ‘incubator’ (atamizi) ili kukuza wajasiriamali wadogo.