Arusha. Mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Olomitu iliyoko Chekereni jijini Arusha, Yusuph Zephania (13) anadaiwa kujinyonga hadi kufa kwa kuogopa adhabu itakayotolewa kwake baada ya kuchelewa shule.
Tukio hilo limetokea jana April 18, 2024 nje ya nyumba katika kamba ya kuanikia nguo iliyokuwa nje.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, SACP Justine Masejo, amesema leo April 19, 2024 amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema mpaka sasa hakuna mtu wanayemshikilia kwa tukio hilo. Mwili umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Rufaa Mount Meru.
Akizungumzia tukio hilo, dada wa marehemu, Flomena Laizer amesema alitoka nyumbani kwao jirani ya nyumba ya baba wa marehemu, ndipo akamuona mtoto huyo akining’inia juu ya kamba akiwa amepiga magoti, huku kamba ikiwa shingoni mwake.
“Nikiwa natoka nyumbani kwetu, kupita hapa njiani jirani na kwa baba mkubwa (baba wa marehemu) ndio nikamuona mdogo wangu akiwa amening’inia kwenye kamba, ameng’ata ulimi. Nilipiga kelele, akaja jirani yetu hapa kujua shida, akakuta mtoto amening’inia akachukua panga lililokuwa jirani akaikata ile kamba,” amesema dada huyo.
Amesema baada ya kamba hiyo kukatwa, mtoto huyo alianguka chini, lakini tayari alikuwa ameshang’ata ulimi na kutoa macho huku akiwa amekakamaa na kupoa.
“Watu walijaa na kumchukua mtoto kumpeleka hospitali kwa vipimo, ili kama hajafa wamsaidie lakini hali ikawa ndivyo sivyo, kwani alishakufa,” amesema.
Baba wa marehemu, Zephania Laizer amesema wakati tukio linatokea alikuwa kijiweni kwake anapopaki bodaboda, ndipo akapigiwa simu na majirani kuwa mwanaye amepata shida, bila kuelezwa tatizo.
“Nikiwa kijiweni niliambiwa mwanangu amepata shida niende nyumbani, nilipofika nikaonyeshwa amekutwa amejinyonga lakini sikujua kama amekufa hadi nilipofika hospitali baadaye,” amesema baba huyo.
Amesema alimuita mama wa mtoto wake kumuuliza kilichotokea hadi mtoto huyo kurudi nyumbani na kufanya tukio hilo.
“Nilimwita mama wa mtoto kwanza kumuuliza ni mtoto yupi amejinyonga? Maana niliondoka asubuhi vijana wangu wote wawili walikuwa wameenda shule, ndipo akaniambia Yusuph alirudi muda wa saa 4 asubuhi akidai amechelewa kufika shule na alipomuona mwalimu aliyemtaja kwa jina moja la Nko akaogopa kuingia na kuamua kurudi nyumbani,” amesema.
“Mke wangu alimshangaa mtoto kurudi nyumbani kisa kumuogopa mwalimu akidai huwa ana adhabu kali, hivyo alimruhusu kuvua nguo za shule kujiandaa na kesho yake kuwahi, lakini wakati anaendelea na shughuli zake nyuma ya nyumba ndio akasikia kelele za dada mtu na kukimbia eneo la tukio na kukuta mtoto amejinyonga”.
Zephani anasema mtoto huyo ambaye kila siku amekuwa mpole na mtulivu, pia alikuwa mbunifu wa vitu mbalimbali nyumbani na hawajawahi kusikia kama ana shida yoyote inayomsumbua moyoni hadi kuchukua hatua hiyo.
Diwani wa viti maalumu Moshono, Veronica Hoseah amesema kama mzazi amesikitishwa na tukio hilo na kuwataka wazazi kuwa karibu na watoto wao kuzungumza nao, ili kufahamu changamoto wanazopitia kabla hawajachukua uamuzi mbaya kama huo.
“Nimeshangaa, mtoto kumuogopa mwalimu hadi kufikia hatua hii ni ngumu kumeza, maana kwanza amepata wapi akili hiyo, labda tuseme ni utandawazi umezidi au ni mapepo. Kikubwa wazazi tuwe karibu na watoto wetu kujua matatizo yao. Si ajabu mtoto alikuwa na tatizo jingine, lakini kwa sababu mzazi hajamuuliza zaidi akaamua kuchukua hatua zake mwenyewe,” amesema diwani huyo.