NIONAVYO: Kombe la Dunia la klabu ni vita mpya ya pesa

TANZANIA, Afrika Kusini na labda Afrika nzima mitandao imejaa mjadala wa uamuzi wa kutia shaka wa refa wa mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika uliozikutanisha Young Africans au Yanga na Mamelodi Sundowns au Masandawana ya Pretoria, Afrika Kusini.

Kutolewa kwa Yanga ni kilio kwa wapenzi wa Yanga, lakini ni kicheko kwa watunzaji wa fedha na zaidi wawekezaji wa klabu ya Mamelodi Sundowns.

Wakati mashabiki wa Yanga wakiomboleza kukosa nafasi ya kuwatambia wenzao wa Simba kwa kuwaacha wakishindwa kuvuka robo fainali kwa uongozi wa Mamelodi sifa ni jambo la pili, lakini fedha inayokuja kutokana na kuendelea kuwemo katika mashindano hayo, na itokee Mungu bariki washinde ndiyo ndoto wanayotamani itimie leo.

Nafasi ya kushiriki Kombe la Dunia la Klabu na kuzoa mabilioni yanayokuja na nafasi hiyo ndiyo kila kitu kwa taifa hilo la manjano na samawati.

Mwamko mkubwa ulikuja Kombe la Dunia la Klabu au Club World Cup kama linavyoitwa na waandaaji wake yaani Fifa linakuja kivingine na klabu zitakazotia mguu Marekani mwakani 2025 kwa kiasi kikubwa zitakuwa zimeuaga umaskini.

Kombe la Dunia la Klabu ni wazo lililoibuka hata kabla ya wazo la mashindano makubwa ya Kombe la Dunia la Mataifa ambalo lilikuja kuchezwa kwa mara ya kwanza mwaka 1930.

Mawazo ya kuwa na Kombe la Dunia la Klabu yanarudi nyuma mpaka huko England na Scotland miaka ya 1880. Mwamko mkubwa ulikuja miaka ya 1950 wakati klabu za Amerika Kusini na Ulaya zilipochuana kupata bingwa ambaye alionekana kuwa bingwa wa dunia.

Mfano wa shindano lililokuwa kubwa ni mchezo uliowakutanisha Palmeiras ya Brazil na Juventus ya Italia uliofanyika katika uwanja wa Maracana, Brazil na kuvuta mashabiki wanaofikia laki mbili.

Mchezo huo wa mwaka 1951 uliojulikana pia kama Kombe la Rio, Copa de Rio, uliweka historia kwa Palmeiras kutawazwa mabingwa na wao kujiita mabingwa wa dunia.

Yote kwa yote, bingwa huyo wa dunia hakutambuliwa na Fifa ambao walisema hiyo ilikuwa ni mechi ya kimataifa ya kirafiki.

Kwa muda mrefu mashindano ya dunia ya klabu na mashindano ya mabara yalishindwa kufanikiwa kwa kutotambuliwa na Fifa iliyoona kama ni mashindano ya mabara mawili wakati Fifa ilikuwa na mashirikisho mengine zaidi ya Uefa na CONMEBOL.Kwa upande wa mwingine Fifa iliwaona Ulaya au UEFA kama ndio kikwazo kwani Ulaya walikuwa wanaiona dunia ya mpira kama iliyo na Ulaya na Amerika  Kusini tu na hivyo kuzuia ushiriki wa mabara mengine.

Miaka kati ya 1960-1970 Fifa ilianza kulipigia debe sana wazo la kuwa na klabu bingwa ya dunia, lakini siku zote kikwazo ilikuwa UEFA. Kwa hiyo pamoja na Fifa kuyaacha mashindano ya Ulaya na Marekani ya Kusini yaendelee, lakini haikupenda kutia mkono wake sana kwa tahadhari ya kutoonekana kuunga mkono mashindano yanayohusisha sehemu ndogo tu ya wanachama wake.

Ilipofika mwaka 2017, Rais wa Fifa, Gianni Infantino alitangaza kuwatambua rasmi mabingwa wa klabu bingwa ya dunia kuwa mabingwa rasmi wa dunia kama walivyo mabingwa wa mataifa.

Ushiriki wa Fifa ulitia hamasa hasa kwa timu za Afrika na Asia ambazo pamoja na kuwakilishwa na timu moja, lakini bado ilikuwa ni hatua moja mbele. Hatimaye Desemba, 2010 klabu ya kwanza isiyotoka Ulaya au Amerika ikafanikiwa kutinga fainali. Hiyo ilikuwa ni TP Mazembe ya Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo. Bahati mbaya ikapoteza fainali kwa Inter Milan ya Italia kwa mabao matatu ya Pandev, Eto’o na Biabiany.

Mwaka 2013 Raja Cassablanca ikaingia fainali na kama ilivyokuwa TP Mazembe,ikaishia kupigwa na mabingwa wa Ujerumani, Bayern Munich ya Pep Guadiola kwa mabao mawili ya David Alaba na Tony Kroos.

Mwaka 2022 Fifa ikatangaza mfumo mpya wa timu 32 kutoka katika mashirikisho yote yaliyo chini yake. Mashindaano ya kwanza kwa mfumo huo yanakwenda kufanyika Marekani 2025 ikiwa ni mwaka mmoja kabla ya fainali za Kombe la Dunia la Marekani ya Kaskazini 2026.

Kulikuwa na maneno mengi hasa kutoka katika klabu za Ulaya wakilalamikia kuchoka kwa wachezaji hasa kutokana na mashindano hayo kupangwa kwenye kipindi cha kiangazi muda ambao ligi zinakuwa zinatamatika. Hata hivyo, wanasema penye udhia penyeza rupia kelele hizo zimezimwa na kifurushi cha fedha kilichoahidiwa na Fifa kwa klabu 32 zitakazoshiriki. Kwanza klabu zitagawana Euro bilioni mbili kwa kila klabu shiriki kulamba karibu Euro milioni 50 sawa takriban Sh140 bilioni. Kuna zawadi za ushindi zinazofikia Euro 2.5 bilioni ambapo bingwa wa dunia atanyakua kiasi cha Euro 100 milioni ikiwa ni takriban Sh280 bilioni. Tayari Fifa na mabara husika wamekwishaweka utaratibu wa kufuzu kwa ajili ya mashindano hayo. Ulaya na Amerika Kusini watakuwa na klabu 12 na sita mtawalia. Kumbuka Ulaya na Amerika Kusini wana historia ndefu kama waanzilishi wa mashindano haya. Lakini pia ikumbukwe haya ni mabara ambayo yametoa mabingwa mara nyingi katika mashindano yaliyotangulia na mpira wao unaonekana kuwa juu kwa viwango kwa kulinganisha na mabara kama Asia, Afrika na Amerika  Kaskazini ambao wana nafasi nne kila mmoja isipokuwa Amerika Kaskazini watakuwa na nafasi moja ya ziada hivyo kuwa na timu tano kama wenyeji. Mpaka sasa timu mbili zinazoiwakilisha Afrika zimeshatangazwa yaani mabingwa wawili waliopita Wydad Cassablanca ya Morocco na Al Ahly ya Cairo, Misri. Zimebaki nafasi mbili za kupiganiwa ambapo klabu mbili zinazokaribia kabisa kutwaa nafasi hizo ni Mamelodi na Esperance ya Tunisia.

Timu hizo mbili zina pointi nyingi kuliko wanaofuatia na bado zimo kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambamo zinaweza kuongeza alama na pia atakayechukua ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika atakuwa na nafasi ya kwenda Marekani moja kwa moja.

Unaweza kuona jinsi kutolewa kwa Mamelodi na Yanga ungekuwa msiba mkubwa kifedha kwao.

Kwa hatua waliyofikia sasa ni kama wanaelekea kwenda Marekani wakiwa na kibunda chao cha Euro 50 milioni. Bingwa hajapatikana na mashindano yanaendelea, lakini ni wazi kwamba sasa Mamelodi wanachagizwa na fedha za Kombe la Dunia la Klabu kuliko hata ubingwa wenyewe wa Ligi ya Mabingwa. Kama klabu iliyotumia fedha nyingi labda kuzidi klabu zote Afrika katika kipindi cha karibuni zinatakiwa kurudi pesa zilizowanunua kina Marcelo Allende, Ronwen Williams na nyota wengine toka pande nne za dunia waliowagharimu Masandawana na familia ya Motsepe mamilioni ya Rand.

Kwa sababu ya pesa, Mamelodi wanataka kusalia kwenye mbio za Ligi ya Mabingwa ije mvua liwake jua.

Mwandishi wa makala hii ni katibu mkuu mstaafu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Unaweza kumtumia maoni yako kupitia simu yake hapo juu.

Related Posts