Dodoma. Waziri George Simbachawene ametumia nukuu za viongozi wa zamani, Alhaji Ali Hassan Mwinyi na Edward Lowassa kuhimiza haki za raia, kujali usawa wa binadamu na fikra za mabadiliko katika jamii.
Simbachawene ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora amesema hayo leo Ijumaa ya Aprili 19, 2024 alipowasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya wizara hiyo kwa mwaka 2024/2025.
Ameliomba Bunge liidhinishe Sh1.101 trilioni, ambazo mchanganuo wake ni Sh922.7 bilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh178.3 bilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Wizara hiyo iko Ofisi ya Rais yenye dhamana ya kufanya maamuzi muhimu kuhusu nchi na inahusika pia na Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ambavyo kwa pamoja vinakuwa nguzo kuu katika uendeshaji wa nchi.
Simbachawene akisoma hotuba ameonyesha umuhimu wa utawala bora kwa kumnukuu Rais wa awamu ya pili hayati Alhaji Ali Hassan Mwinyi kwamba:
“Pamoja na umuhimu wa uvumilivu, ni vyema viongozi wakawa wapenda na watenda haki kwa dhati, wanaojua na kuheshimu kwa vitendo haki za raia, na kujali usawa wa binadamu.”
Simbachawene ameitumia kauli hiyo kueleza mchango wa utumishi wa umma na utawala bora una katika maendeleo ya Taifa.
“Ni dhahiri kuwa mchango endelevu wa watumishi wa umma na uwepo wa utawala bora utaliendeleza Taifa na kuleta ustawi kwa Watanzania,” amesema.
Pia ametumia kauli ya Waziri Mkuu mstaafu, hayati Edward Lowassa kueleza umuhimu wa mabadiliko ya fikra katika utendaji.
“Mabadiliko ni fıkra. Ni kufikiri na kutenda tofauti.” Ni kauli ya Lowassa iliyonukuliwa na Simbachawene kwenye hotuba hiyo ya bajeti.
“Naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako lipokee na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka 2023/24 na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais,” amesema.
Kwa kunukuu kauli za Mwinyi na Lowassa, wizara imejipanga kufuata nasaha hizo kwenye utendaji wao wa kazi.
Simbachawene ametumia kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoitoa Aprili 22, 2021 akilihutubia Bunge la 12 aliposema:
“Tutawapima viongozi na watumishi kwa namna wanavyotimiza majukumu yao, hatutawaonea aibu viongozi na watumishi wazembe, wezi na wabadhirifu wa mali za umma. Tutaendeleza pia juhudi za kupambana na rushwa kwenye utumishi wa umma. Wajibu wa watumishi wa umma ni lazima uendane na haki zao.”
Simbachawene ametumia nukuu hiyo kueleza katika kuendana na wakati, jitihada zaidi zitawekwa kwenye kujenga uwezo na mifumo ya kimenejimenti na utoaji huduma, ikiwemo matumizi sahihi na salama ya fursa zinazopatikana katika utoaji huduma kwa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) ndani ya Serikali.