Sh900 milioni zaboresha Hospitali ya Wilaya Nachingwea

Nachingwea. Serikali imetoa Sh900 milioni kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya afya katika hospitali kongwe ya Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Fedha hizo zimetumika kwa ajili ya ujenzi wa maabara ya kisasa, kichomea taka ambacho kinatumia umeme na mafuta, jengo la kufulia nguo na la wagonjwa wa nje (OPD).

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Hayo yamebainishwa leo Aprili 19, 2024 wakati kamati ya Jumuiya ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Tanzania (ALAT) ilipotembelea kuona utekelezaji wa miradi ya afya katika wilaya hiyo.

Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Lindi, Andrew Chikongwe ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha hizo ili kuboresha miundombinu ya hospitali hiyo, ambayo baadhi ya majengo yake yameanza kuchakaa.

“Mimi ni mwenyekiti wa halmashauri ya Ruangwa, nitaenda kuwaambia madiwani wangu tuje kujifunza Nachingwea. Nachingwea wamejitahidi sana kwani tumeona maabara ya kisasa yenye hadhi ya nyota tatu.”

“Si jambo la masihara hata kidogo. Ni jambo kubwa kuwahi kutokea, hasa katika ukanda wa kusini, kwa hospitali ya halmashauri kupata hadhi ya nyota tatu,” amesema Chikongwe.

Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk Ramadhan Maige ameeleza kuwa miongoni mwa hospitali zilizopokea fedha kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya hospitali kongwe na imepokea Sh900 milioni.

Dk Maige amesema fedha hizo zimejenga kichomea taka kikubwa ambacho kinatumia umeme na mafuta kufanya kazi na kina uwezo wa kuzuia moshi wenye madhara usitoke nje, zimejenga jengo la kufulia lenye nafasi ya kupokea mashine nne za kufulia na pasi ambayo imeshawekwa na kuanza matumizi.

Ameongeza kuwa kuna jengo kubwa la wagonjwa wa nje lenye nafasi ya kutosha pamoja na maabara ya kisasa yenye maboresho, ukilinganisha na ya awali, kwani ya sasa ina uwezo wa kuchukua vipimo zaidi ya 80.

Dk Maige ameongeza kuwa maabara hiyo inazingatia usiri na nafasi ya kutoa vipimo kwa wakati na weledi kwa kutumia vifaa vya kisasa.

Mmoja wa wagonjwa wanaopatiwa tiba kwenye wa hospitali hiyo, Zainabu Ngombo ameeleza ubora wa huduma zinazotolewa hospitalini hapo kwa sasa  ukilinganisha na miaka ya nyuma.

Amesema kwa sasa huduma zimeboreshwa na hata watoa huduma wanafuata weledi wa kazi zao.

Related Posts