Unguja. Wakati mbunge kutoka Baraza la Wawakilishi, Suleiman Haroub Suleiman akisema Rais mstaafu wa Zanzibar, Dk Salmin Amour Juma anaishi katika hali ngumu baada ya nyumba yake kukabiliwa na mmomonyoko wa udongo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imetoa ufafanuzi ikisema inawalinda viongozi wake na masilahi yao.
Hata hivyo, SMZ imesema mbunge huyo ameuliza swali ambalo si mahali pake maana Bunge haliwezi kuwa na majibu kwa sababu Dk Salmin hakuwahi kushika nafasi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, hivyo Serikali ya Muungano haina jukumu la kumtunza.
Mbunge Suleiman ameuliza swali bungeni leo Aprili 19, 2024 katika kipindi cha maswali na majibu.
Amesema kuna baadhi ya viongozi ambao waliitumikia Serikali akiwamo Dk Salmin ambaye anaishi katika hali ngumu.
Pia katika swali lake mbunge huyo, amesema kuna baadhi ya maeneo yanahitaji kutunzwa lakini hadi sasa yapo katika hali hatarishi, ikiwemo shule aliyosoma Karume bila kumtaja kama ni Abeid Amani Karume Rais wa Awamu ya Kwanza au Amani Abeid Karume Rais wa awamu ya sita wa SMZ.
Hata hivyo, wakati akijibu swali hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dk Seleman Jafo amesema sheria inagusa maeneo mahususi lakini kwa sababu hayo ni mambo ya Muungano, atayachukua na kuyafanyia kazi kupitia wenzao wa Zanzibar.
Alipotafutwa na gazeti hili kutoa ufafanuzi kuhusu jambo hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu wa Baraza la Wawakilishi, Hamza Hassan Juma amesema SMZ inawalinda viongozi wake na masilahi yao.
Amesema kuna stahiki zao za msingi ambazo zipo kwa mujibu wa sheria, hivyo suala la mmomonyoko wa udongo katika eneo analoishi kiongozi huyo mstaafu lipo zaidi kimazingira.
“Serikali ipo katika utaratibu wa kuangalia namna gani ya kuyahifadhi maeneo yale si tu nyumba ya Dk Salmin pekee lakini nyumba zote ambazo zipo katika ukanda ule hali ni ileile na suala hilo ni la kimazingira,” amesema Waziri Hamza.
Kwa mujibu wa waziri huyo, SMZ ipo katika mpango wa kuhifadhi maeneo hayo kupitia mpango wa mazingira.
“Kwa hiyo si suala lakushughulikiwa nyumba yake tu, ni eneo lote la ukanda ule kuanzia Mazizini hadi Kilimani,” amesema.
Kuhusu uchakavu wa shule aliyosoma Karume, Waziri Hamza amesema hana uhakika na shule hiyo, lakini kwa sasa Serikali inatumia fedha nyingi kujenga shule hadi vijijini.
Amesema kama angeitaja shule hiyo angeweza kutoa ufafanuzi vizuri.
“Shida Mheshimiwa Suleiman masuala ya Baraza la Wawakilishi ameyapeleka bungeni ambako kule hawatakuwa na jawabu la kujibu maswali hayo,” amesema.
Hata hivyo, amesema anafuatilia kwa kina shule hiyo, hivyo atatoa ufafanuzi zaidi baadaye.