Tanesco kuajiri 430, wamo mafundi mchundo

Dodoma. Bunge limeelezwa kuwa watumishi 430 wataajiriwa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) katika mwaka 2024/25.

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema hayo leo Ijumaa Aprili 19, 2024 alipojibu swali la mbunge wa Tunduru Kusini, Daimu Mpakate.

Mbunge huyo amehoji ni lini Serikali itaajiri madereva na mafundi ambao wamekuwa vibarua wa muda mrefu kwenye shirika hilo.

Akijibu swali hilo, Kapinga amesema Tanesco imekuwa ikiajiri watumishi wa kada mbalimbali kwa kuzingatia mahitaji ya kiuendeshaji na uwezo wa kibajeti kwa mwaka husika.

Amesema katika ikama na bajeti ya mishahara ya mwaka 2024/25, pamoja na mambo mengine, shirika limetenga fedha kwa ajili ya nafasi 430 za ajira mpya.

Kapinga  amesema ajira hizo ni kwa wahandisi 67, fundi sanifu 135, fundi mchundo 205 na madereva 23. 

Kapinga amesema ujazaji wa nafasi hizi utazingatia sheria na taratibu katika utumishi wa umma.

Katika swali la nyongeza mbunge wa Nanyumbu, Yahaya Mhata amesema katika majimbo ya Tunduru Kusini na Nanyumbu kuna madereva na mafundi sanifu katika ajira za muda kati ya miaka mitano hadi saba.

“Je, wizara iko tayari katika ajira zinazokuja kuwafikiria madereva hawa na mafundi sanifu ambao wapo katika shirika muda mrefu,” amehoji mbunge huyo.

Naibu Waziri Kapinga amesema wizara inathamini mchango wa wafanyakazi vibarua, hususani mafundi na madereva.

“Nataka niwahakikishie kwa kuwa ni wafanyakazi wetu wanafanya kazi kwa jitihada kubwa katika shirika letu, tutahakikisha ajira zinapotoka wanazingatiwa ipasavyo kulingana na sheria na taratibu za utumishi wa umma,” amesema.

Related Posts