Vita iko hapa Kariakoo Dabi

MECHI za watani wa jadi huweza kuamuliwa na uwezo binafsi wa washambuliaji, viungo na mara chache mabeki, lakini mbinu za kocha zinaweza pia kuwa nguzo ya timu kupata matokeo iliyokusudia.

Mara kadhaa ustadi binafsi wa wachezaji kama Emmanuel Okwi, Dua Said, Omary Hussein ‘Keegan’, Abeid Mziba ‘Tekero’, Abdallah Kibadeni ‘King Mputa’, Amissi Tambwe, Mohamed Hussein ‘Mmachinga’, Madaraka Seleman ‘Mzee wa Kiminyio’ na Jerry Tegete umekuwa ukiamua mechi za watani wa jadi katika mazingira ambayo wengi hawakutarajia.

Shuti la mbali la Okwi alilopiga katika dakika ya 52 ya mechi ya Ligi Kuu ya Bara ya mwaka 2015, lilitosha kuamua matokeo ya mechi hiyo iliyoonekana kuelekea kuwa sare. Kipa Ally Mustapha ‘Barthez’ hakutegemea kuwa Okwi angejikunjua na kuachia shuti la mbali akiwa kulia mwa uwanja. Alipostuka, mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uganda alikuwa ameshaachia shuti hilo na kumkuta Barthez akiwa amesogea mbele kidogo ya mstari wa lango na hivyo kushindwa kuzuia mpira.

Hali kadhalika, mechi baina ya watani hao iliyoonekana kuelekea kumalizika kwa sare, iligeuka ghafla katika dakika ya 75 ya mechi hiyo ya Oktoba 2011 na Simba kujikuta wakilala kwa bao 1-0. Mshambuliaji wa kimataifa wa Zambia, Davies Mwape alipenyezewa pasi safi, lakini akaonekana amebanwa na beki wa Simba. Hata hivyo, mshambuliaji huyo mwenye umbile la miraba minne, alilazimisha kuingia eneo la goli na huku mabeki wakihofia kumchezea vibaya, walijikuta wakimruhusu kufunga bao pekee na la ushindi kwa Yanga.

Mjini Mbeya, Yanga walikuwa wakijiandaa kushangilia ushindi wa bao 1-0, lakini George Masatu akazima furaha yao katika dakika ya 89. Yanga walicheza faulo nje kidogo ya eneo la penalti na kabla ya friikiki kupigwa, refa akanyoosha mkono juu kuonyesha kuwa mpira haukutakiwa kupigwa moja kwa moja golini. Lakini beki huyo mahiri wa kati akapiga shuti moja kwa moja lililojaa wavuni kuipa Simba sare muhimu katika mechi ya mwisho ya Ligi Kuu.

Katika msimu ambao ulikuwa mgumu kwa Yanga mwaka 2018 baada ya mfadhili na Mwenyekiti Yusuf Manji kujiweka kando, ilionekana kama vigogo hao wa Jangwani wangepata kipigo kikubwa mbele ya Simba iliyoanza msimu kwa kishindo, ikishinda mechi zake zote za kwanza.

Lakini mbinu za kocha Mwinyi Zahera na ustadi wa kipa Beno Kakolanya ziliiepusha Yanga katika uwezekano wa kupata kipigo cha aibu. Huku Simba wakitawala umiliki kwa zaidi ya asilimia 70, Yanga waliwasubiri golini wakiepuka kucheza rafu, huku wakiwazonga washambuliaji wa Simba wasiweze kutulia kutumia nafasi za wazi walizopata.

Hayo yanaweza kutokea wakati watani hao wa jadi watakapokutana tena kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, kesho  Jumamosi kumalizia kipande chao cha mkate walichotengewa msimu huu baada ya Yanga kuibuka na ushindi mkubwa wa mabao 5-1 katika mchezo wa kwanza, ushindi ambao Yanga iliusubiri kwa muda mrefu.

Simba haijawa kwenye mwenendo mzuri katika mechi za karibuni, kwa mara ya kwanza ikifungwa nyumbani na ugenini na Al Ahly ya Misri na kutolewa tena katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa na baadaye kuondolewa Kombe la Shirikisho kwa penalti na Mashujaa ya Kigoma kabla ya kulazimisha sare ya bao 1-1 na Singida Black Stars (zamani Ihefu).

Lakini hilo halitawafanya kuingia mchezoni wakiwa vichwa chini kwa kuwa wanajua kuwa wachezaji kama Kibu Dennis, Sadio Kanoute, Cloutus Chama, Ayoub Lakred na Henock Inonga wanaoweza kufanya lolote wakati wowote ama kuinusuru timu na kipigo au kuipa ushindi.

Yanga inaonekana kwenye mwenendo mzuri, ikitoka kupata ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Singida Fountain Gate, huku ikiwa imeonyesha nidhamu ya hali ya juu kimbinu katika mechi mbili dhidi ya Mamelodi Sundowns ambazo ilisadikiwa awali kuwa vigogo hao wa Afrika Kusini wangeweza kupata ushindi mnono, hasa katika mechi ya marudiano.

Kocha Miguel Gamondi ndiye mtu wa kwanza anayeweza kuamua matokeo kutokana na mbinu zake alizoonyesha katika mechi tofauti, huku Stephane Aziz Ki, Clement Mzize, Kennedy Musonda, Maxi Nzengeli na Pacome Zouzoua wakiwa na uwezo wa kuamua mechi uwanjani.

Kiungo wa zamani wa kimataifa wa Mali amekuwa akichezeshwa nafasi tofauti katika kiungo. Anapocheza kama kiungo wa nyuma hutumia nguvu sana anapoenda kupokonya mipira na huishia kupata kadi. Lakini katika siku za hivi karibuni amekuwa akisaidia mashambulizi na ingawa msimu huu amefunga mabao mawili tu, hujiweka katika nafasi nzuri za kufunga kutokana na ujanja wa kutoroka mabeki. Urefu wake humuwezesha kucheza mipira ya juu ya krosi na ari yake ya kupambana humuwezesha kuifikia mipira ambayo hakutarajiwa. Ni mmoja wa wachezaji waliokosa mabao ambayo yangeiwezesha Simba angalau kushinda mechi ya nyumbani dhidi ya Al Ahly. Lakini mabao huja wakati wowote kwa mchezaji anayefungua, kutoroka mabeki na kupambana kufikia mipira ya juu ya kona na krosi.

Ni huzuni kwake kwamba hadi sasa amefunga bao moja tu msimu huu licha ya jitihada kubwa anazofanya za kumiliki mipira kusubiri wenzake, kupokonya mipira na hata kulisha wenzake. Ameifunga Yanga katika mechi mbili mfululizo zilizopita, la kwanza likiwa la shuti kali kutoka nje ya eneo la penalti lililoipa Simba ushindi wa mabao 2-0 msimu uliopita na la pili likiwa la kichwa aliposawazisha katika mechi ambayo timu yake ililala mabao 5-1.

Ni mshambuliaji mwenye nguvu, kasi, mhangaikaji na mwenye mashuti. Pengine ndiye pekee ambaye mashabiki wa Simba wanamkubali katika safu ya ushambuliaji. Hutokea upande wa kulia na pamoja na kutegemea kutumia mguu wa kushoto, bado ana uwezo wa kutumia vizuri mguu wa kulia.

Alianza msimu wa kwanza Simba kwa kufunga mabao manane, lakini akapoteza nuru msimu uliofuata alipomudu kufunga mabao mawili tu, huku akilaumiwa na mashabiki kwa kushindwa kuzifumania nyavu na zikiwa zimesalia mechi 10 kwa Simba, hadi sasa ana bao moja. Lakini hiyo haimuondolei uwezekano kuwa anaweza kuamua mechi ya watani Jumamosi. Kasi yake, nguvu zake katika kugombea mpira dhidi ya mabeki na ukunjufu wa moyo wake katika kutoa pasi za mwisho kwa wenzake vinaweza kuwa vitu vitakavyomuwezesha kuamua mchezo.

Hakuna shabiki wa soka ambaye anaweza kudhihaki uwezo wake wa kuamua matokeo. Akili kubwa anayotumia kugawa mipira mbele ya lango, utulivu wake katika mazingira magumu, mipira mizuri ya adhabu anayotuma kwa wenzake na shabaha yake katika mipira ya adhabu huweza kubadili matokeo wakati wowote. Bado hajaweza kuitungua Yanga katika mechi za Ligi Kuu, lakini alikuwa chachu ya ushindi wa mabao 4-1 ambao Simba iliupata kwa Yanga katika Kombe la Shirikisho misimu minne iliyopita.

Beki wa kimataifa wa Jamhuri ya Congo ambaye amekuwa nguzo kuu katikati mwa ukuta wa Simba. Ana uwezo wa kujiunga na safu ya ushambuliaji wakati Simba inapokwenda mbele, uwezo mkubwa wa kucheza mipira ya juu wakati wa krosi au kona. Ameshaingia katika karatasi ya wafungaji wa mechi za watani wa jadi alipofunga bao la kichwa.

Ingawa bado hajafanikiwa, lakini ni hatari pia kwa mashuti ya mbali anayopiga bila ya kutarajiwa. Inonga pia anaweza kuamua matokeo kwa kuzuia washambuliaji kumfikia kipa wake Ayoub Lakred kirahisi kutokana na uwezo wake wa kuwahi mipira, kujinyoosha kufuata mipira ya chini na kuokoa mipira ya juu kutokana na kimo chake kizuri.

Kama Simba itazidiwa sana kwenye kiungo, itabidi ihamishie matumaini yake katika kujilinda na kama mabeki wake Shomary Kapombe, Inonga, Che Malone na Mohamed ‘Tshabalala’ Hussein watakuwa wakitoa nafasi kwa wapinzani, basi kipa wa zamani wa FAR Rabbat ya Morocco atakuwa ndio tegemeo. Atakuwa akicheza mechi ya kwanza ya watani wa jadi.

Ingawa alianza kwa mashabiki kumdhihaki, kipa huyo raia wa Morocco ameonyesha ustadi mkubwa golini, hasa washambuliaji wanapobakia naye. Kocha Benchikha amekuwa akimuamini katika mechi za kimataifa na hakuna shaka ndiye atayesimama katikati ya milingoti miwili Jumamosi hii kudhibiti mashuti ya mbali ya Aziz Ki, mipira ya kichwa ya Musonda, Joseph Guede na Mzize.

Mshambuliaji wa kimataifa wa Burkina Faso ambaye amekoleza moto unaomfanywa asakwe na klabu kubwa za Afrika. Msimu uliopita alimaliza akiwa amefunga mabao manane na tayari msimu huu ana mabao 14 huku zikiwa zimesalia mechi tisa kwake. Shuti lake ambalo lingeweza kuhesabiwa kuwa goli katika mechi dhidi ya Mamelodi Sundowns limezua gumzo kubwa barani Afrika. Na kuonyesha kuwa hakubahatisha, mshambuliaji huyo wa zamani wa Asec Mimosas alionyesha ustadi huo dhidi ya Singida Fountain Gate.

Wakiwa wanakimbia sambamba na Mzize aliyekuwa na mpira, Aziz Ki alinyoosha mikono kumtaka mshambuliaji ampasie na ilifanyika hivyo. Bila ya kutuliza Aziz Ki aliachia shuti kutoka umbali wa takriban mita 30 kufunga bao la pili kwa Yanga.

Mbali na uwezo wa kufunga kwa mashuti ya mbali, Aziz Ki ana uwezo mkubwa wa kupiga pasi za mwisho au muhimu kwa wenzake wanaokimbia kutoka pembeni na pia kufunga mabao ya frii-kiki. Hutumia vizuri kasi ya Mzize na Nzengeli kutoa ama pasi za mwisho au muhimu kuelekea golini. Ndiye aliyekuwa nguzo kuu ya ushindi wa mabao 5-1 katika mechi ya kwanza, mwenyewe akifunga bao moja.

Anazidi kugeuka kuwa kipenzi cha mashabiki wa Yanga kadi anavyojituma uwanjani na tabia yake ya kutokuwa mchoyo mbele ya goli. Katika mechi dhidi ya Fountain Gate, alitoa pasi mbili za mwisho na katika mechi ya ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Simba, alitengeneza mabao mawili yaliyofungwa na Aziz Ki na Nzengeli.

Anakuwa bora kadri siku zinavyokwenda na uwezo wake wa kuamua mechi kwa kufunga au kutoa pasi za mwisho unazidi kukua.

Ni mshambuliaji wa kati lakini mara nyingi hutokea upande wa kushoto, akianzisha mashambulizi na baadaye kwenda kusubiri mipira mbele ya lango. Bao lake dhidi ya Mtibwa Sugar, alipopokea pasi akiwa amelipa mgongo lango, lakini akageuka haraka na kufunga kwa mguu wa kushoto, lilionyesha kiwango chake cha unyumbufu anapokuwa kwenye mazingira magumu golini.

Ni mwibiaji mzuri wa mipira ya krosi kutokana na urefu wake na ndiye aliyewatanguliza Yanga katika mechi iliyopita dhidi ya Simba alipounganisha krosi ya Yao Kouassi. Ni msumbufu kwa mabeki, mhangaikaji na mwenye uwezo mzuri wa kurudi nyuma kuungana na wenzake kuanzisha mashambulizi. Alikuwa msaada mkubwa kwa Fiston Mayele ambaye alikuwa mfungaji hodari wa Yanga.

Hadi sasa kiungo huyo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amefunga mabao manane na huenda kasi yake imepunguzwa na majukumu tofauti ambayo Gamondi amekuwa akimpa katika siku za hivi karibuni. Ana uwezo mkubwa wa kugeuka na mipira anapotaka kuwashtukiza wapinzani kwa shambulio na mara nyingi ni mchezaji anayepiga pasi za mbele,.

Kasi yake huiwezesha Yanga kusonga mbele haraka na hivyo kuwazidi wapinzani kwa idadi ya watu golini kwao. Imani yake kuwa mbele ndiko muhimu, huiwezesha timu kutengeneza nafasi na akili yake ya kufuatilia pasi zake humuwezesha kufunga kwa kuipata mipira iliyookolewa. Alifunga mabao mawili katika mechi iliyopita, la kwanza likitokana na pasi safi aliyotanguliziwa na Aziz Ki na la pili likitokana na shambulizi aliloanzisha kutoka upande wa kushoto na kufuatilia mpira hadi ulipopigwa na Mzize na kumkuta mbele ya lango huku kipa Aishi Manula akishindwa kuzuia krosi hiyo ya chini.

Hatazamiwi sana kuanza baada ya kupata majeraha katika mechi ya Ligi Kuu, lakini iwapo atapangwa, mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Ivory Coast anaweza kuwa chachu ya ushindi. Ana uwezo wa kuibeba timu pale anapoona imebanwa kwenye nusu yao kutokana na ustadi wake wa kukimbia na mpira. Ana uwezo mkubwa wa kufunga kutoka nje ya boksi na ni mchezeshaji mzuri wa wenzake anapotaka timu itembee kwenda mbele. Ndiye aliyeanzisha wimbi la mabao katika mechi ya mwisho baina ya timu hizo, akianza na mpira kulia mwa uwanja na kumzidi mbio Kanoute kabla ya kupiga krosi kwa Musonda aliyechelewa na mpira uliookolewa ukamfikia Kouassi ambaye aliurudisha kwa Musonda aliyefunga kwa kichwa.

Pacome aliibeba Yanga katika mechi za makundi za Ligi ya Mabingwa, hasa dhidi ya CR Belouizdad na ndiye aliyefunga bao la Yanga dhidi ya Al Ahly.

Rekodi za wachezaji hao zinaweza kuwa muhimu wakati Simba na Yanga zitakapokutana kesho katika mechi ya pili ya Ligi Kuu, lakini ‘dabi’ hiyo yaweza kuamuliwa na wachezaji wengine ambao huibuka na kung’ara siku ya mechi kama Mudathir Yahya ambaye ameibukia kufunga mabao muhimu siku za karibuni au uzoefu na ukongwe wa wachezaji kama Mzamiru Yassin ambaye ana uwezo mkubwa wa kuhamisha mpira kutoka upande mmoja na upambanaji wake.

Related Posts