Wafugaji Monduli walia bwawa kupasuka, kupoteza maji

Arusha. Wananchi wa jamii ya wafugaji katika kijiji cha Nanja kilichopo wilaya ya Monduli mkoani Arusha, wameiomba Serikali kuharakisha ukarabati wa kuta za bwawa la maji lililopo kijijini hapo, ambalo kuta zake zimevunjika na kusababisha maji mengi kupotea.

Bwawa hilo la kuhifadhia maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na kunyweshea mifugo, liliharibiwa na maji kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.

Akizungumza leo Ijumaa, Aprili 19, 2024, Mwenyekiti wa Kijiji cha Nanja, Yamati Lemomo amesema kupasuka kwa bwawa hilo kunaweza kusababisha athari kubwa kwa wananchi, wanaotegemea maji hayo kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na kunyweshea mifugo.

“Maji mengi yameondoka baada ya bwawa hili kupasuka na athari yake ni kubwa kwani wanalitegemea. Kwa makadirio, karibu watu 50,000 wanalitegemea, Serikali itusaidie ili wananchi wasiumie kwa kukosa maji, japo tunashukuru hakuna madhara ya binadamu yaliyotokea.”

“Wananchi wa Nanja tuna kilio kwani bwawa linategemewa na wafugaji wote, tunajua maji ndiyo uhai, kwa kuwa yameshatoka mengi maana yake maisha ya wafugaji wa Monduli hakuna,” amesema.

Kwa upande wake, Joh Maulid ambaye ni mkazi wa kijiji hicho, amesema wananchi wanahitaji msaada wa haraka kwani hakuna chanzo kingine cha maji katika eneo hilo, hivyo Serikali iharakishe marekebisho hayo.

Akizungumza na wananchi hao baada ya kutembelea na kuona athari zilizojitokeza katika eneo hilo, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amewataka wataalamu wa wizara kuhakikisha wanatumia taaluma zao ipasavyo kuwanusuru wananchi hao kwa kurekebisha bwawa hilo kwa dharura.

Amesema kutokana na bwawa hilo kuwa chanzo kikuu cha maji kwa kata zaidi ya saba wilayani humo, wataalamu hao watashirikiana na viongozi na wananchi katika suala hilo.

“Wataalamu wa Wizara ya Maji msije mkasema hii kazi haiwezekani, sijui gharama, mtafia kwenye kazi, lazima muwaokoe hawa wananchi, nimekwenda kujionea kule, tumeajiri  wataalamu hatujaajiri wababishaji ambao wanalipwa mishahara na Serikali, watumie taaluma zao kuwasaidia wananchi wa Nanja.”

“Katibu Mkuu, Wizara ya Maji ina wataalamu wengi wa mabwawa, kesho asubuhi tukutane hapa watupe utaalamu namna gani tunakwenda kuliziba hili bwawa ili maji haya yasipotee.

Aweso amesema suala hilo ni la dharura, lazima lishughulikiwe kidharura kwani mawe na vifaa vingine vipo na wizara hiyo itatoa fedha kwa ajili ya ukarabati wa bwawa hilo.

Related Posts