Dk Mwinyi awapa mbinu wahandisi utekelezaji miradi mikubwa

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema ili wahandisi wazawa wapewe miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali hawana budi kuungana kupata mitaji mikubwa.

 Hata hivyo, amesema Serikali zote mbili zinaendelea kushirikisha taaluma ya uhandisi katika shughuli mbalimbali, ikiwamo kuweka mazingira yanayowawezesha kujiajiri.

Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Aprili 20, 2024 alipozindua taasisi ya wasanifu, wahandisi na wakadiriaji majenzi (IAESZ) kisiwani Unguja.

Amesema si wakati wote Serikali inakuwa na fedha inapotekeleza miradi, bali kampuni zinalazimika kujenga kisha hulipwa kwa awamu.

“Mwendelee kujenga uwezo na ikibidi muungane, ili kuleta ufanisi na kuweza kukopeshwa fedha kwenye taasisi za fedha kutekelza miradi maana si wakati wote Serikali inakuwa na fedha, unaweza kuambiwa jenga mradi fulani kisha utalipwa fedha zako polepole,” amesema Dk Mwinyi.

Amesema Serikali zote mbili, ya Zanzibar na ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinafanya jitihada kushirikisha taaluma hizo katika shughuli mbalimbali, ikiwemo kuweka mazingira yanayowawezesha kujiajiri.

Rais wa Zanzibar,  Dk Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza mwakilishi wa Kampuni ya PADDCO, Afla Abdalla Mrusi wakati akitembelea maonyesho ya wahandisi, kabla ya uzinduzi wa Taasisi ya Wasanifu, Wahandisi na Wakadiriaji uliofanyika leo Aprili 20,2024. Kushoto kwa Rais ni Waziri wa Ujenzi,Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Dk Khalid Mohamed Salum na (kulia) Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Ayoub Mohammed Mahmoud

Amesema wanahamasisha utambuzi wa fursa kupitia rasilimali zilizopo nchini, kurejesha stadi za ujuzi, elimu ya uanagenzi vyuoni na kutenga bajeti kwa ajili ya kufanikisha utafiti na bunifu mbalimbali.

“Tunajua tunahitaji kushirikiana, ili kufanikisha dhamira ya maendeleo endelevu hususani katika fani hizi kutokana na umuhimu wake kwa ustawi wa nchi yetu,” amesema.

Amesema fani za wasanifu, wahandisi na wakadiriaji zinabeba dhima ya shughuli mama katika harakati za kujenga, kuimarisha na kuendeleza uchumi wa nchi, hivyo wanazipa mazingatio makubwa.

Amesema Tanzania ni nchi inayoendelea, ambayo imefikia katika uchumi wa kati kutokana na kuwa na miradi inayochangia zaidi pato la Taifa na nyuma yake wakiwapo wenye fani hizo.

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza akimsikiliza mwanafunzi wa Chuo cha Karume Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume Zanzibar akitoa maelezo ya ufundi wa utengenezaji wa mashine za ndege,  alipotembelea maonyesho ya wahandisi katika hafla hiyo.

“Tunaamini tayari tunao wakandarasi wazuri na washauri elekezi mahiri wazawa, wenye uwezo mkubwa wa kufanyakazi hizi za uhandisi kwa weledi,” amesema.

“Miradi mbalimbali mliyoitekeleza kwa ufanisi mkubwa ni kielelezo kinachotufanya tuwaamini,” amesema.

Rais wa IAESZ, Abdul Samad Mattar amesema taasisi hiyo inalenga kuwa na wanachama wengi zaidi Zanzibar wanakotarajiwa kufikia 500 na Tanznaia Bara 200. Kwa sasa wapo 152.

Amesema taasisi hiyo inawajengea uwezo wataalamu kuwa washindani katika kupata miradi mingi ya maendeleo.

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk Khalid Salum Muhamed amesema kuna mabadiliko makubwa na ujenzi mkubwa wa miradi kupitia kwa wataalamu hao.

Amesema wanaendelea kuboresha sera na sheria, ili kuhakikisha taaluma hiyo inaendelea kufanya vizuri katika ujenzi wa miradi.

Related Posts