Ileje. Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya Ileje mkoani Songwe limemtaka Mkurugezi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Nuru Kindamba ajitathimini katika usimamizi wa fedha za miradi zinazotolewa na Serikali Kuu.
Hayo yamejiri leo Jumamosi Aprili 20, 2024 katika kikao cha Baraza la Madiwani baada ya madiwani hao kubaini miradi mingi ya maendeleo haijakamilika huku fedha zikidaiwa hazitoshi kuitekeleza.
Diwani wa Ndola, Bahati Kyomo amesema mkurugenzi ameshindwa kusimamia fedha zinazoletwa na Serikali Kuu badala yake zinatumika kwa maununuzi yasiyozingatia miongozo inayotolewa.
“Mimi kwenye kata yangu nimeletewa Sh150 milioni kwa ajili ya ujenzi wa vyumba sita vya madarasa na vyoo matundu 12, lakini hakuna kilichokamilika, ukiuliza wanasema tutatenga fedha kwenye mapato ya ndani hali ambayo sio sawa kwa maendeleo ya wilaya yetu,” amesema Kyomo.
Bupe Kalonge, diwani viti maalumu amesema Wilaya ya Ileje imebaki shamba la bibi kutokana na matumizi mabaya ya fedha akitolea mfano Kituo cha Afya Ndola na Itale, ambavyo Serikali ilitoa Sh1 bilioni yaani Sh500 milioni kwa kila kimoja na kuongezewa Sh40 milioni za mapato ya ndani kwa Ndola na Itale kikapatiwa Sh30 milioni, lakini miradi yote hiyo haijakamlika mpaka sasa.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Ubatizo Songa amesema mkurugenzi pamoja na wataalamu wanaosimamia miradi wanashindwa kusimamia vyema fedha kwenye miradi.
“Sisi kama Baraza la Madiwani tutahakisha wataalamu wote watakaokwamisha miradi inayotekelezwa kwa fedha za Serikali na mapato ya ndani, wanachukuliwa hatua,” amesema Songa.
Akijibu hoja hizo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo ambaye pia ni Ofisa Mipango, Amoni Sangana amesema wamepokea maelekezo ya Baraza la Madiwani na watarekebisha kasoro zote zinazojitokeza.
Awali, Mkuu wa Wilaya hiyo, Farida Mgomi aliwaonya watumishi wote wanaokwamisha miradi kwamba watasakwa na hatua za kisheria dhidi yao zitachukuliwa.
“Wataalamu wa wilaya hii mjitathimini kwenye matumizi ya fedha za Serikali ambazo zinashindwa kumaliza miradi ikiwepo ya vituo vya afya Ndola na Itale ambavyo ujenzi wake ulianza mwaka 2022 na haijakamilika, tutahakikisha tunawachukulia hatua wote wanaokwamisha,” amesema Mgomi.