Mafuriko yafunga shule nne Kyela, Sh35 milioni kusaidia waathirika

Mbeya. Serikali imezifunga shule nne zilizoko katika Kata ya Katumba Songwe wilayani Kyela Mkoa wa Mbeya kutokana na kuzingirwa na maji ya mafuriko.

  Maji hayo mpaka sasa yamezingira pia makazi ya watu na leo Jumamosi Aprili 20, 2024 Serikali imepeleka msaada wa fedha taslimu Sh35 milioni zitakazowasaidia waathirika.

Mafuriko hayo yaliyoanza Machi, mwaka huu,   mbali ya kuzingira makazi ya wananchi, pia yameharibu mashamba ya mpunga, mihogo, kakao na migomba.

Awali akizungumza baada ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera kufikisha salamu za Rais Samia Suluhu Hassan kwa wananchi wa kijiji cha Mwaya, Mbunge wa Kyela, Ally Mlaghila amesema eneo hilo huwa linakumbwa na mafuriko kila mwaka, lakini ya mwaka huu yamekuja kivingine.

Mlaghila amesema uharibifu wa mashamba uliofanyika unaashiria mwakani kutakuwa na uhaba mkubwa wa chakula katika vijiji hivyo.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera akiwajulia hali waathirika wa mafuriko waliohifadhiwa katika kambi ya  Mwaya Wilaya ya Kyela baada ya kupelekea salama za Rais Samia Suluhu Hassan

“Hili bonde lote tumepita ni maeneo ya mashamba ya mpunga na kakao, mihogo, yamezama kabisa kwenye tope na mashamba mengine yameja maji, hali ni mbaya,” amesema mbunge huyo.

Naye Ofisa Mtendaji wa kata ya Mwaya, Venusta Mpogole amesema vijiji 10 vimezingirwa na maji na kwa sasa wanaendelea kufanya tathimini ya mashamba na kaya 82 wamezinusuru kwa kuzihifadhi katika vituo maalumu.

“Madhara mengine yaliyojitokeza ni pamoja na shule nne kufungwa,” amesema mtendaji huyo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, Patrick Mwalunenge ameishauri Serikali ili kuwanusuru wananchi na adha hiyo, itenge maeneo mengine kwa ajili ya wananchi hao kuhamia huko.

Hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Kyela kutafuta maeneo salama ya wazi yapimwe na wayagawe kwa wanachi hao.

“Ndugu zangu kwanza niwape pole nimefika nimejionea hali ilivyo, Rais Samia Suluhu Hassan amenituma kuleta mkono wa pole Sh 35 milioni ambazo zimetumika kununua mahitaji mbalimbali muhimu,” amesema.

Homera amesema Serikali iko bega kwa bega na waathika wote mpaka watakapopata ufumbuzi wa changamoto na kuhakikisha wako  sehemu salama.

Mwathirika wa mafuriko, Elizabeth Kasingira ameishukuru Serikali kwa msaada wa mahitaji na kutenga eneo salama kwa ajili ya kuwahamishia.

“Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kutukumbuka ,ingawa hofu yetu kubwa ni uwepo wa baa la njaa kutokana na mafuriko kufanya uharibifu wa mazao. Tunaomba Serikali isituache itushike mkono, wengi tulikuwa tukitegemea kilimo kuendesha maisha ya kila siku” amesema.

Related Posts