Njombe. Wananchi wa Kata ya Makowo, Halmashauri ya Mji wa Njombe, wamepatiwa gari la kubeba wagonjwa litakalowapunguzia changamoto ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya.
Akikabidhi gari hilo leo Jumamosi Aprili 20, 2024 Mbunge wa Njombe Mjini, Deo Mwanyika amesema mwaka 2021 aliomba hospitali hiyo ipatiwe vifaa tiba, wahudumu wa afya na gari la kubeba wagonjwa.
Amesema anafurahi kuona maombi yake yote yametimizwa baada ya awali kupatiwa vifaa tiba na wahudumu wa afya na leo wamekabidhiwa gari la wagonjwa kwa kituo hicho cha afya kinachowahudumia wananchi wa Kata ya Makowo na maeneo ya jirani.
Amesema wagonjwa wengi hupatiwa rufaa ya kwenda kutibiwa katika Hospitali ya Kibena na ile ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe.
“Ndugu zangu tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais (Samia Suluhu Hassan) amefanya makubwa katika jimbo letu la Njombe na kata hii ya Makowo, leo hii tumeshuhudia mambo makubwa matatu, ikiwemo ahadi ambayo mimi niliitoa ya kupatiwa gari la kubeba wagonjwa,” amesema Mwanyika.
Amewataka wananchi na watumishi wa kituo hicho cha afya kulitunza gari hilo ili lifanye kazi iliyokusudiwa ya kubeba wagonjwa.
Mganga mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Njombe, Jabir Juma amesema inapotokea dharura ambayo kwa hali ya kawaida katika kituo ambacho huduma fulani haiwezi kutolewa, wananchi hupata shida ya usafiri wa kuwapeleka eneo lingine kupata huduma inayohitajika.
Amesema zahanati zinazozunguka Kata ya Makowo zitafaidika na rufaa kwa wagonjwa wanaohitaji huduma katika kituo cha afya cha Makowo.
“Kwa hiyo wananchi hawatohangaika tena na kugharamia gharama za magari ya kawaida, ambulance hii itatoa huduma kwenye maeneo mengi na ni bure,” amesema Juma.
Baadhi ya wananchi wa Kata ya Makowo akiwemo Valentina Mlelwa amesema gari hilo litawasaidia kuepuka gharama ya kukodi magari binafsi kwa ajili ya kuwapeleka wagonjwa hospitali nyingine.
“Ujio wa gari hili ni jambo kubwa sana kwetu mwanzo wenye magari madogo ndiyo tulikuwa tukikodi kwa gharama kubwa mpaka kufika kwenye vituo vyetu vya afya,” amesema Mlelwa.