Zikiwa zimesalia takribani saa nne ili kuchezwa kwa mechi ya Watani wa Jadi Yanga dhidi ya Simba, hali ya Uwanja wa Benjamin Mkapa, imepoa.
Wakati saa zikizidi kusogea na jua likiwa kali katika maeneo ya uwanja, mpaka sasa hali bado si ya kuridhisha kwa upande wa mashabiki.
Rangi zinazoonekana kwa wingi maeneo haya ni kijani na njano zinazowakilishwa na Yanga SC, huku nyekundu na nyeupe zile za Simba SC, zikiwa kwa uchache sana.
Unaweza kusema wenyeji wa mchezo huu ambao ni Yanga wanaonekana kuupania mchezo huu kutokana na wingi wao kuwazidi Simba.
Biashara nazo zinaendelea kufanya kwa uchache, huku maeneo mengi ya vyakula yakionekana kuwa wazi.
Kwa upande wa barabara kutoka maeneo mbalimbali hapa jijini Dar es Salaam zinazoelekea Kwa Mkapa, nazo zimekuwa wazi tangu asubuhi.
Mtanange huo unaosubiriwa kwa hamu kubwa, utachezwa leo Jumamosi ya Aprili 20, majira ya saa 11:00 jioni.
Simba ambao ni wageni, wataingia uwanjani wakiwa na rekodi ya kupoteza mchezo uliopita kwa kufungwa mabao 5-1 dhidi ya Yanga.