Dar/Mara. Biashara ya usafirishaji abiria kwa kutumia pikipiki maarufu kama bodaboda imegeuka ajira kubwa nchini ikiwa na mambo mengi ndani yake.
Wapo wenye pikipiki zao wenyewe, wapo wanazikodi na kurejesha hesabu kwa tajiri (mmiliki) kila siku na wapo wenye mikataba, kwamba baada ya kurejesha fedha za mmiliki pikipiki inabaki mali yao.
Utaratibu huu wa mkataba, ambao uliaminika ndiyo salama zaidi kwa wamiliki, hivi sasa nao unakabiliwa na changamoto kadhaa, kila upande wa mkataba ukiulalamikia mwingine.
Wakati madereva wakilalamika kwamba mikataba inayoingiwa ni ya kinyonyaji, wamiliki wa pikipiki nao wanalalama kuhusu usumbufu na kuikukwa kwa masharti ya mkataba unaofanywa na wanaopewa pikipiki.
Wamiliki wa bodaboda wanasema baadhi ya madereva si wastaarabu katika utunzaji wa vyombo hivyo vya moto, na hawana uaminifu katika uwasilishaji wa mapato.
Ni kutokana na hayo, baadhi ya madereva wanalalama kunyang’anywa pikipiki wanapokaribia kumaliza mikataba hivyo.
Mikataba inayosainiwa katika serikali za mitaa au vijiji, mmiliki humkabidhi dereva pikipiki kwa ajili ya kufanya biashara ya usafirishaji kwa sharti la kuwasilisha mapato ya kila wiki kwa muda wa mwaka mmoja au miezi 16, kisha bodaboda inakuwa mali yake.
Hata hivyo, hali ya kutupiana lawama kati ya pande hizo mbili, imeibua hoja ya kukosekana ajira nchini, inayotajwa kuwa sababu ya vijana wengi kuishia kwenye shughuli ya bodaboda, licha ya changamoto zilizopo.
Malalamiko ya bodaboda yaliibuliwa mkoani Mara katika ziara ya Makamu Mwenyekiti wa CCM -Bara, Abdulrahman Kinana.
Joseph Chege mbele ya Kinana anasema wamewasilisha malalamiko kwa halmashauri lakini hakuna ufumbuzi uliopatikana.
Anasema kila wiki hutakiwa kuwasilisha kwa mmiliki Sh70,000 ambazo zitapelekwa kwa miezi 16, sawa na Sh4.48 milioni.
Kiasi hicho anasema hakilingani na bei ya pikipiki dukani ambayo ni Sh2 milioni.
“Ukifanya kazi kwa muda huo chombo kinakuwa kimechoka hata ukifika wakati wa wewe kukimiliki hakikupi faida tena,” anasema Chege.
Dereva mwingine aliyelalamikia hilo ni Shadrack Mwita aliyesema matajiri wengi hununua pikipiki kwa shughuli hiyo, hasa wanapoona vijana wanahitimu vyuo na kurudi mitaani.
“Hapa Bunda ukitaka kuendesha pikipiki, mkataba kwa wiki Sh70,000 unatakiwa kutoa ndani ya miezi 16, pamoja na ugumu huo unaweza ukakuta umepambana umebakiza miezi miwili umepata changamoto anafuta mkataba na kukunyang’anya chombo chake,” anasema.
Hilo la mikataba kusitishwa pia lilizungumzwa na Wambura Marwa.
Mwenyekiti wa Bodaboda Mkoa wa Dar es Salaam, Michael Massawe anasema mikataba wanayopewa imeegemea upande wa wamiliki na kumnyima haki dereva.
Katika mikataba hiyo, Massawe anasema kuna vipengele vinavyomuadhibu dereva ikiwemo kunyang’anywa pikipiki iwapo atakosea, lakini hakuna kinachomwadhibu mmiliki atakapotenda kosa.
“Maana yake dereva tu kwa sababu hana kitu ndiye anayeonekana atakosea, lakini mkataba hautambui kuna wakati mmiliki anaweza kukosea,” anasema.
Mazingira hayo, anasema ndiyo yanayorahisisha wamiliki kuwanyang’anya pikipiki madereva hasa pale wanapokaribia kumaliza mikataba.
Anasema hata baadhi ya wamiliki hawana ustaarabu, kwani hutuma watu kumnyang’anya dereva pikipiki ambao huwapiga kabla ya kuchukua chombo hicho.
Massawe amependekeza utaratibu wa kibenki kufanyika wakati wa ukopeshaji na malipo kwa biashara ya usafirishaji wa bodaboda.
Anasema mkoani Dar es Salaam unafanyika utaratibu huo na takribani vijana 3,000 wamekopeshwa pikipiki kwa mfumo huo.
“Tunachotamani ni Serikali iingilie kati na kuamua kuwakopesha vijana pikipiki kupitia benki, hii itasaidia kwa sababu kule hakutakuwa na mikataba ya kinyonyaji,” anasema.
Abdul Msonga, mmoja wa wamiliki wa bodaboda aliyewahi kufanya biashara hiyo ya usafirishaji, anasema madereva wengi hawana leseni na wanapokamatwa hukimbia na kuziacha pikipiki kwa askari wa usalama barabarani.
“Iliwahi kunitokea, mwenye pikipiki yangu amekamatwa na askari, amekimbia akaiacha, ilibidi niifuate na kugharimia faini ya makosa yake, nikamnyang’anya,” anasema.
Pia anasema wamekuwa wakilimbikiza fedha za makusanyo kwa kutowasilisha kwa mmiliki au benki kwa mujibu wa makubaliano ya mkataba.
“Mimi na dereva wangu masharti ya mkataba yalikuwa akishindwa kuwasilisha mapato kwa wiki mbili nachukua pikipiki yangu. Pamoja na masharti hayo, dereva alikuwa anapitisha hadi mwezi bila kuniletea kiasi chochote cha fedha, ulifika wakati, muda wa mkataba umeisha lakini bado namdai fedha za miezi minne, ilibidi nimnyang’anye,” anasema.
Mmiliki mwingine, Benson Msaky anasema baada ya kumkabidhi kijana pikipiki kutoka dukani, dereva aliuza baadhi ya vifaa ikiwamo betri na shokapu, kisha akanunua vifaa vya zamani na kuvifunga.
“Pikipiki ilianza kusumbua kila siku. Nilipofuatilia nikabaini ameuza vifaa halisi amenunua vingine,” anasema.
Anasema dereva mwingine alitoa kazi kwa watu wengine ambao walikuwa wakimpelekea fedha ndipo naye awasilishe kwake.
“Sio tatizo kwa kuwa mimi ninachotaka ni fedha, lakini shida inakuja kwenye utunzaji, hawa anaowapa hawatunzi chombo na wanabeba mizigo hata inayozidi uwezo wa pikipiki, ndani ya miezi miwili pikipiki inachoka mno,” anasema.
Wamiliki wakisema hayo, kiongozi wa bodaboda Massawe anasema madereva wengi huwa wanahakikisha usalama wa vyombo hivyo kwa kuwa wanafahamu ndiyo maisha yao ya baadaye.
“Unakuta bodaboda au bajaji inakaribia kumaliza mkataba inaonekana vizuri kama imetoka jana dukani,” anasema.
Kuhusu uaminifu wa kuwasilisha fedha kwa wamiliki, anasema hutokea dharura ikiwemo dereva kuugua au kupatwa na tatizo lolote.
“Mkataba hauelezi chochote kuhusu dereva atakapoumwa, mmiliki anataka apelekewe fedha hata kama unaumwa, ndiyo maana tunasema mikataba ni mibaya,” anasema.
Mmoja wa wenyeviti wa Serikali za Mitaa, Salama Kiwanda anasema ukiukwaji wa masharti ya mikataba ni moja ya kesi wanazosuluhisha kila mara kati ya madereva na wamiliki wa pikipiki.
Salama, mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Vigaeni mkoani Mtwara, anasema kinachosababisha hali hiyo ni kukosekana uaminifu miongoni mwa madereva.
“Hivi majuzi tumesuluhisha kesi ililetwa hapa, dereva amemaliza mkataba lakini bado anadaiwa Sh400,000 hakuwa amelipa kwa bosi wake, ikabidi tufanye busara ya kumpa muda wa ziada amalizie,” anasema.
“Tulipomuuliza tumpe muda gani mwenyewe akaahidi wiki moja, tukaona kama ameshindwa kulipa kwa mwaka, ndani ya wiki atawezaje? Ilibidi tumuombee muda zaidi,” anasema.
Pamoja na hayo, Massawe anasema vijana wengi wenye umri wa miaka 18 hadi 35 walioshindwa kuendelea shule na wahitimu wasio na ajira, wamekimbilia ajira hiyo yenye kina aina ya karaha.
Profesa wa uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Abel Kinyondo anasema kumekosekana mbadala wa kazi ndiyo maana vijana wanaishia kufanya shughuli hiyo isiyo na staha.
Suala la vijana kung’ang’ana na kazi hiyo kutokana na uhaba wa ajira, linashabihiana na kilichowahi kuelezwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Godbless Lema, aliyesema shughuli hiyo si kazi inayopaswa kufanywa bali ni laana.
“Hakuna kazi imeangamiza vijana kama kazi ya bodaboda, halafu mnasema tusiseme ukweli eti kwa sababu mna kura, mimi siishi kwa ubunge, nataka nitetee watu,” alisema Lema.
Lema aliitaka Serikali itafute mbinu ya kuwaondoa vijana kwenye ajira aliyoiita ya ‘kukimbiza upepo.’
“Hiyo si kazi ya maana na inazidisha umasikini na umasikini ni laana,” alisema Lema.
Mtaalamu wa uchumi, Profesa Samuel Wangwe anasema ni muhimu Serikali ikaingilia kati kutengeneza usawa katika mikataba hiyo ili pande zote zinufaike.
Hata hivyo, alitilia shaka suala la bodaboda ya Sh2 milioni kuingiza faida ya Sh5 milioni, akisema ni kubwa isiyolingana na uzalishaji halisi wa chombo husika.
“Haiwezekani ununue chambo kwa Sh2 milioni halafu umpatie mtu aendeshe na utengeneze faida mara mbili zaidi ni faida kubwa mnoo, ilitakiwa Serikali isaidie kuingia makubaliano ili wapate hata faida ya Sh1.6 milioni ili na wanaofanya kazi nao wafaidike,” anasema.
Akizungumza katika ziara mkoani Mara kuhusu malalamiko ya bodaboda hao, Kinana aliahidi kuzungumza na wabunge ili watengeneze utaratibu mzuri kuhusu hilo.
“Vijana wana hoja, nimekubaliana nanyi, nitaenda kuongea na wabunge wote kuhusu suala hili ili kutengeneza utaratibu mzuri wa kuwakopesha vijana pikipiki na kukabiliana na watu wanaowanyonya,” alisema.
Hata hivyo, alisema wanaofanya hivyo ni wachache wanaotaka kujinufaisha, akisisitiza haiwezekani pikipiki ya Sh2 milioni ikaingize Sh5 milioni.