Wanazuoni, wataalamu waeleza faida, changamoto na maadui wa Muungano

Unguja. Wakati Tanzania ikielekea kuadhimishwa miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, zimetajwa changamoto, faida na maadui wa Muungano huo ulioasisiwa mwaka 1964.

 Miongoni mwa faida za Muungano ni kupanua maeneo ya kiuchumi, heshima kimataifa, amani, umoja na masuala ya ulinzi na usalama katika mataifa hayo mawili.

Changamoto kubwa ni kutoundwa tume ya akaunti ya pamoja, jambo ambalo linatajwa kuonekana upande mmoja kuendelea kupata misaada na mikopo kutokana na utashi wa mtu badala ya sheria.

Hayo yamebainika jana katika kongamano la tathmini ya miaka 60 ya Muungano lililoandaliwa na Mchambuzi Media na Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (Suza), Maruhubi Unguja.

Mwanasiasa mkongwe Hamad Rashid amesema licha ya changamoto nyingi kupatiwa ufumbuzi, suala la akaunti ya pamoja bado linasumbua, kwani bila kuwapo tume hiyo, yapo mambo ambayo yanaendeela kutolewa kama hisani.

“Iwapo likipatiwa ufumbuzi litaondoa changamoto nyingi, kwani ndiyo suala zima la mgawanyo wa mapato, masuala ya misaada na mikopo na ndiyo hayo yanatakiwa kila mtu ajue kanuni yake ni ipi badala ya kutegemea utashi wa mtu,” amesema Hamad.

“Kuna kipindi fulani utashi hautakuwapo misaada haitapatikana, lakini kama kuna sheria na chombo maalumu cha kusimamia jambo hilo kila kiongozi anayekuja atasimamia misingi hiyo,” amesema.

Amesema Sheikh Abeid Amani Karume na Mwalimu Julius Nyerere walikuwa na ndoto zao, zipo ambazo zinaendelezwa na nyingine zimefifia.

Amesema viongozi hao katika kuunganisha mataifa hayo walitamani kuona wanasayansi wengi wanasoma na kuja kubadilisha Taifa lao, lakini kwa sasa ndoto hizo zipo kinadharia.

Kuhusu masuala ya rushwa na maadili, viongozi hao walichukia vitu hivyo, lakini kwa sasa kuna maadili yameporomoka na rushwa inatawala.

Amesema ndoto nyingine walitamani baada ya kuwakimbiza wakoloni nchi iendeshwe kwa Kiswahili, jambo ambalo ndoto hiyo inaendelea mpaka sasa.

Balozi Amina Salum Ali

Balozi Amina Salum Ali amesema Muungano utaendelea kudumu kwa kuendelea kusema ukweli na uwazi, ili kila mtu ajue ulipotokea na umuhimu wake.

Kuhusu akaunti ya pamoja, amesema jambo hilo wanamatumaini litakwisha hivi karibuni, kwani viongozi wameshaonyesha dhamira ya kulishghulikia.

Balozi Amina amesema Muungano uliundwa kwa dhamira njema na fikra hizo zinapaswa kuendelea, kwani kuna matunda ya Muungano hata kama mengine hayaonekani, lakini yapo hata kwa hisia.

“Kuaminika na kupendwa katika dunia ni kutokana na Muungano wetu upo sahihi hata wananchi wanakuwa wasikivu na kuongea kwa uwazi Tanznaia inaendela kusifika pote,” amesema Amina.

Mwanasiasa mkongwe nchini, Dk Harrison Mwakyembe amesema baada ya kuungana viongozi hao walijitahidi kujenga Zanzibar mpya, ili kuondoa mtazamo ambao ulijengwa kwamba huenda kukawa na matatizo makubwa zaidi ya walipokuwa wakitawaliwa na wakoloni.

Kutokana na hilo ndipo walitafuta mbinu za kuondoa jambo hilo na kuwafanya wananchi waondokane na umasikini, hivyo Karume alianza kugawa ardhi bure ekari tatu kwa kila mmoja.

Amesema wakati anauawa mwaka 1972 tayari alikuwa ameshagawa ekari 24,000 za ardhi.

Kisha aliamua kutoa elimu bure, wakati nchi hizo zinaungana Zanzibar ilikuwa na asilimia 11.7 ya elimu na kupanda hadi asilimia 61 na kuanza kutoa matibabu bure.

Baada ya hapo alianza kujenga makazi bora na kuanzisha malipo kwa ajili ya wazee kupewa fedha za kujikimu.

Amesema mambo aliyoyafanya Karume kwa kipindi cha miaka minane hayakuwahi kufanyika sehemu yoyote duniani.

Amesema baada ya Muungano kulifungua milango Wazanzibari kwenda Tanzania Bara na kufanya shughuli zao, kuoa na kuolewa bila ubaguzi na maeneo yote bila ubaguzi.

Dk Harrison Mwakyembe

Dk Mwakyembe amesema viongozi hao waliona shauku kubwa ya Muungano ukiendelea kuimarisha maendeleo zaidi ilivyokuwa na ndiyo maana walikuwa wakifanya jitihada nyingi kuhakikisha wanashirikiana kupiga hatua.

Baada ya Muungano, amesema kuna watu walidhani ndiyo mwisho wa Zanzibar maana itamezwa katika Muungano, hivyo waasisi wa Muungano walifanya kila jitihada kuhakikisha hilo halitokei na walifanikiwa.

Kutokana na hilo, suala la Zanzibar lilipewa kipaumbele na viongozi hao kuhakikisha inainuka na kufika mbali.

“Mzee Karume (Abeid Amani Karume) alizunguka kwa kiasi kikubwa kutoa elimu kuhusu umuhimu wa Muungano,” amesema.

Amesema kilichosababisha Muungano utokee kwa haraka kulikuwa na hatari katika masuala ya usalama.

Dk Mwakyembe ambaye kitaaluma ni mwanasheria amesema bado upo uwezekano wa kurekebisha muundo wa Muungano iwapo ikionekana kuna haja ya kufanya hivyo.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar Salaam (UDSM), Dk Idd Mandi amesema hati ya Muungano ni waraka muhimu, ni katiba ya tatu baada ya Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Amesema zipo faida nyingi za Muungano ikiwa ni pamoja na kuleta umoja, lakini katika suala la uchumi umepanua eneo kubwa la kibiashara.

“Biashara zinapanuka kwa sababu kunakuwa na eneo kubwa, mnachangia rasimali zilizopo na Muungano unaleta udugu,” amesema.

Kuhusu kuwapo madai ya kuwa na Serikali tatu, Dk Mandi amesema zinaweza kuongeza gharama na changamoto za Muungano.

Amesema kumekuwapo na ubishani kuhusu haki za Zanzibar katika Muungano, Zanzibar kutokuwa na haki ya kukopa fedha nje ya nchi, bandari na masuala ya kugawana mapato.

Katika Tume ya Jaji Kisanga mwaka 1998 asilimia 6.5 ndiyo walitaka Serikali moja, asilimia 4.3 walitaka Serikali tatu na asilimia 88.87 walitaka Serikali mbili.

Mtaalamu wa siasa na uongozi wa umma, Dk Richard Mbunda ametaja masuala ya usiasa, utaifa na udumavu kiuchumi kuwa tishio kwa Muungano.

“Kuna usiasishaji wa kero za Muungano, wanasiasa wakiona kero fulani wanataka kuzitumia kama njia ya kuhusianisha Muungano na kero hizo,” amesema.

Dk Mbunda ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amesema kutokana na umaskini na masuala ya kiuchumi vinapoibuka vinataka kuhusianishwa na masuala ya Muungano, hivyo kuendeleza hoja ambazo hazina uhalisia.

Kuhusu utaifa, amesema limekuwa likisumbua watu wengi na kuanza kuona kila upande una mambo yake.

Hata hivyo, amesema jambo hilo huenda Rais Samia Suluhu Hassan akalimaliza na ameonyesha njia ya kuliendea.

“Sifikirii siku za karibuni Wazanzibari waendelee kulalamikia uwepo wa Muungano, kwani Rais Samia amefifisha hilo jambo,” amesema.

Kuhusu watu wanaolalamikia Muungano, amesema watu hao wanapaswa kukaribishwa kwenye hoja waeleweshwe na kuwapo na mifumo rasmi itakayosimamia mambo hayo.

Dk Mbunda amesema vijana wengi hawaelewi masuala ya Muungano, hivyo lazima historia zifundishwe shuleni.

Makamu Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Zanzibar (Suza), Professa Moh’d Makame Haji amesema Muungano ni maridhiano kwa hiyo kama kuna kitu hakipo sawa, lazima kifanyiwe kazi ili kuishi katika maono ya waasisi wa Muungano.

Related Posts