YANGA inashuka kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa saa 11:00 jioni kupambana na watani zao, Simba, huku timu hiyo ikiwa na rekodi bora msimu huu wakati michezo yao ya Ligi Kuu Bara ilipochezeshwa na mwamuzi wa kati, Ahmed Arajiga.
Arajiga kutokea mkoani Manyara ndiye aliyepewa jukumu la kutafsiri sheria 17 za soka baina ya timu hizo, huku rekodi zikionyesha katika michezo yote ya Ligi Kuu Bara aliyosimamia Yanga haijawahi kupoteza wala kutoka sare.
Msimu huu, Arajiga amechezesha michezo minne ya Yanga ambapo mabingwa hao watetezi, wameshinda yote.
Mchezo wa kwanza kwa Arajiga kuichezesha Yanga ulikuwa ni ushindi mnono wa mabao 5-0 dhidi ya JKT Tanzania, mechi iliyopigwa Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Agosti 29, mwaka jana.
Mechi nyingine ilikuwa ya ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Azam FC, Oktoba 23, mwaka jana huku nyota wa timu hiyo, Stephanie Aziz KI akifunga mabao yote matatu yaani ‘Hat-Trick’.
Nyingine ambayo ndiyo ilizua taharuki ni ile ya kichapo cha mabao 5-1 ilichokitoa Yanga kwa watani zao Simba, Novemba 5, mwaka jana huku mchezo huo ukikumbukwa zaidi kwani ndio uliosababisha kutimuliwa kwa aliyekuwa Kocha wa Simba, Mbrazili, Roberto Oliveira ‘Robertinho’.
Mechi ya mwisho na ya nne ambayo Yanga ilichezeshwa na Arajiga na ikashinda ni ile iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijjini Mbeya ambapo ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Tanzania Prisons, Februari 11, mwaka huu.