Eti tusiwachape watoto wakikosea, tuwafanyeje?

Dar es Salaam. Mwaka jana nilipata bahati ya kutembelea sehemu zaidi ya tatu ambazo wazazi na walezi hawaruhusiwi kupiga watoto wao viboko. Na ninaposema hawaruhusiwi namaanisha hawaruhusiwi kwelikweli, sio ile ya tangazo tu, kwamba inakuja serikali au uongozi unatangaza kuwa hauruhisiwi kumchapa viboko mtoto, kisha wakimaliza kutangaza na kuondoka huku nyuma wazazi wanaweza kuendelea kuwacharaza watoto wao kama kawaida na hakuna kitu watafanywa.

Hizi sehemu nilizoenda, mzazi au mlezi akimgusa mtoto ujue hiyo ni kesi, mtoto ana uwezo wa kwenda kumripoti mzazi wake, na mzazi akawajibishwa. Na sio tu mpaka mtoto akaripoti, hata majirani na watu wengine wanaweza kuripoti pia.

Lakini nikiwa huko, moja ya kitu nilichogundua ni kwamba watoto wa maeneo hayo hawana adabu hata kidogo. Wanaweza kufanya mambo ya ajabu tena mbele ya macho ya watu wazima. Kitu ambacho sijapata kukishuhudia sana kwenye jamii ambazo watoto wanachapwa viboko.

Na hapa sina maana kwamba bila viboko watoto hawawezi kuwa na adabu, hapana. Ila ukweli ni kwamba, kucharaza viboko watoto imekuwa ndiyo njia pekee ya miaka yote ambayo sisi Watanzania tumekuwa tukiitumia. Babu yangu alichapwa na baba yake, babu yangu akamcharaza viboko baba yangu na mimi pia nilipofanya upumbavu sikusalimika mikononi mwa baba yangu, alinicharaza. Mwalimu wangu alipokuwa mwanafunzi alichapwa na mwalimu wake, na yeye alipokuwa mwalimu alituchapa sisi wanafunzi wake tulipokosea.

Kwa hiyo kwa miaka yote tumejifunza kwamba linapokuja suala la kumuadabisha mtoto, njia inayofanya kazi zaidi ni kumcharaza viboko. Na ndiyo maana hata kuna kipindi adhabu ya viboko ilipotaka kuondolewa mashuleni mgongano mkubwa ulitokea, wengine walisema ziendelee kuwepo kwa sababu zinasaidia kuwanyoosha watoto, wengine wakasema zisiwepo kwani ni sehemu ya ukatili kwa watoto na zinawakosesha amani ya kujifunza.

Ukiangalia vizuri suala la kutochapa watoto ni kama geni hapa kwetu na limeanzia kwa wenzetu wa magharibi, ambao wao kwao mtoto hachapwi hata afanye nini. Siipingi, ni njia nzuri, lakini nadhani mtindo uliotumika kuiingiza sehemu kama Tanzania haukuwa sahihi.

Kwa wenzetu, mtoto hachapwi lakini bado akikosea unaweza ukawa unaendelea kumpa adhabu nyingine kama vile kumzuia asifanye vitu anavyovipenda, mfano kwenda nje kucheza na wenzake, kuangalia TV, kucheza gemu na vitu vingine. Lakini pia kumfanyisha vitu asivyovipenda kama vile kazi za nyumbani, kulala mchana na kadhalika. Na kweli, hizi nji zinasaidia sana kumnyoosha mtoto, tena inawezekana zinamnyoosha mtoto kuliko viboko, lakini tatizo ni kwamba, waliokuja kutuambia tusiwachape watoto wetu hawatuambia kuhusu hizi njia.

Na hii sio kwenye viboko tu, imekuwa ikifanyika kwenye tamaduni nyingi ambazo tunakatazwa kuendelea kuzifanya. Unaambiwa usifanye kitu fulani. Lakini kumbuka, watu hawakuwa wakifanya kitu hicho bila sababu, wamekuwa wakikifanya kwa kuwa kuna faida wanayopata. Sasa unapokuja kuwazuia, inabidi uwaonyeshe mbadala wa nini wafanye ili waendelee kupata faida ile ile.

Mwishowe, tumeacha kuwacharaza viboko watoto wetu kwa kuogopa kuwajibishwa, lakini wanapofanya makosa hatujui tuwafanye nini. Tunawaacha na matokeo yake ndiyo tunapata watoto jeuri, viburi na wasiokuwa na utu na tabia za kufurahisha hata kidogo, mtoto anaweza kufanya tukio la ajabu mbele ya wageni wako na baba ukashindwa kufanya chochote kwa kuhofia kuwajibishwa.

Waliokuja kuzuia tusiwachape watoto wetu walitakiwa watupe darasa lililokamilika kuhusu namna ya kumuadhibu mtoto bila viboko.

Related Posts