Arusha. Zaidi ya waumini 200 wa Kanisa la Kilutheri Afrika Mashariki (KKAM) wamefanya ibada nje ya nyumba ya mtu baada ya kukuta kanisa lao limefungwa na kuzungushiwa mabati kutokana na mgogoro wa ardhi.
Eneo la kanisa hilo lilizungushiwa mabati wiki iliyopita na mtu anayetajwa kuwa mmiliki wa eneo hilo, baada ya kushinda kesi kuhusu madai ya kuvamiwa eneo la familia yake na kuendelezwa bila kibali cha familia.
Katika shauri hilo, Askofu wa Kanisa hilo la KKAM, Philemon Mollel maarufu kama Monaban ndiye aliyedaiwa kuvamia eneo hilo na kujenga kanisa lililokuwa linatumiwa na waumini hao.
Wakizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili Aprili 21, 2024, waumini hao wamesema uhuru wa kuabudu umeporwa na watu wanaodai eneo hilo ni lao, na wamemwomba Rais Samia Suluhu Hassan aingilie kati mgogoro huo.
“Huu mgogoro sisi hatujawahi kuusikia zaidi ya juzi kukuta eneo la kanisa limezungushiwa mabati na kufuli kubwa kila pembe, hivyo vipindi vya ibada na mafundisho vimekwama,” amesema Magreth Ayubu, muumini wa kanisa hilo.
Ametumia nafasi hiyo kumwomba Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda na Rais Samia Suluhu kuwasaidia kupata eneo mbadala kwa ajili ya kuendesha ibada wakati mgogoro huo ukitafutiwa ufumbuzi zaidi.
“Tunaomba viongozi wetu watusaidie hasa Rais wetu Mama Samia aone hilo jambo ni la Kimungu zaidi, atupatie eneo lingine la kusalia kwani tunataabika na watoto tunaowalea kiroho wanateseka. Pia, vipindi vya maombi kwa usalama wa Taifa letu navyo vinakwama,” amesema Magreth.
Mchungaji wa kanisa hilo, Emmanuel Mollel amesema baada ya kukosa pa kusalia na waumini wamefika, wameamua kufanya ibada nje ya nyumba ya mmoja wa viongozi wa kanisa hilo.
“Ibada ni kila kitu kwenye huu ulimwengu, hivyo baada ya kukuta kanisa limefungwa na bahati mbaya waumini wote hawakupata taarifa, tumelazimika kufanya ibada hapa nje tukiendelea na maombi kwa viongozi wetu wa Serikali waangalie jambo hili upya lakini pia kutupatia eneo mbadala la kusalia,” amesema Mchungaji Emmanuel.
Akizungumzia suala hilo, Askofu Monaban amesema hali hiyo imetokea baada ya Mahakama kumpatia ushindi aliyemshtaki kwa madai alivamia eneo hilo.
“Eneo hilo nilinunua mwaka 2009 kwa Jimmy Titus Mollel, ambaye alikuwa msimamizi wa mirathi ya mali ya baba yake, Titus Mollel. Alidai wamekubaliana na familia anayoisimamia kuuza,” amesema Monahan.
Amesema eneo hilo la kanisa, kiwanja namba 31, kikiwa pamoja na viwanja namba 29, 30 na 32 vyote kwa pamoja, vina ukubwa wa ekari mbili alivyonunua jumla ya Sh360 milioni.
“Haya maeneo mimi sijavamia, bali nilinunua kihalali na nimewekeza kituo cha mafuta, sehemu ya kuoshea magari, kanisa na supamaketi, vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya Sh2.5 bilion, nashangaa Mahakama ikitoa hukumu ya kuamuru nirudishe ardhi ya watu bila kujali hata nimewekeza na nirudishiwe fedha zangu,” amesema Monaban.
Amesema anatarajia kukataa rufaa dhidi ya shauri hilo, hivyo kuwataka watu wanaotaka kununua maeneo hayo wasikubali kwani bado kuna mgogoro.
Kwa upande wake, mmoja wa wanafamilia wanaodai eneo lao kuvamiwa, William Mollel amesema wameamua kuzuia shughuli zozote kuendelea katika eneo lao lililovamiwa.
“Baba yetu alituchia hili eneo sisi familia yake, na Monaban alikuja kumrubuni aliyekuwa msimamizi wetu wa mirathi akadai amenunua. Hii ni Mali ya familia huwezi kununua kwa mtu mmoja, hivyo amfuate aliyempa hela arudishiwe hela zake lakini kwa sasa tumeshakua na tumekuja kumiliki mali zetu wenyewe,” amesema William.