Mabalozi wa Tanzania nje wanolewa chuo cha uongozi

Kibaha. Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika mataifa mbalimbali duniani wamekutana mjini Kibaha, mkoani Pwani kwa warsha maalumu inayolenga kuwakumbusha majukumu yao na matarajio ya Serikali kwenye maeneo yao ya kazi.

Warsha hiyo iliyoandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, imeanza leo Aprili 21, 2024 katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere mjini Kibaha na itamalizika Aprili 24, 2024, ikiwashirikisha mabalozi na watendaji waandamizi wa wizara.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Jamruary Makamba akizungumza katika warsha ya mabalozi wa Tanzania nje ya nchi na maofisa waandamzi wa wizara kwenye Chuo cha Uongozi cha Nyerere Kibaha mkoani pwani leo Aprili 21, 2024.

Akizungumza kwenye warsha hiyo, Waziri wa wizara hiyo, January Makamba amesisitiza umuhimu wa kuwa na mfumo wa kuwajibishana ambao utasaidia kuhamasisha utendaji kazi na kuongeza ufanisi katika wizara.

Amezungumzia pia umuhimu wa kuendelea kulinda heshima na hadhi ya nchi kwenye mataifa wanakofanya kazi.

Katika kufanikisha hilo, amesema kunapaswa kuwa na mazingira bora ya utendaji kazi na vitendea kazi vinavyohitajika.

“Serikali itahakikisha inaboresha mazingira ya kazi ili nchi iendelee kulinda heshima yake iliyojengwa kwa muda mrefu na viongozi waliopita,” amesema Makamba.

Wakati huohuo, amewapongeza mabalozi kwa kazi nzuri wanayofanya licha ya changamoto wanazokabiliana nazo.

Makamba amesema tangu ateuliwe kuwa Waziri wa Mambo ya Nje kwa muda wa miezi saba sasa, amebaini kuna uwezekano wa kufanya mambo makubwa zaidi, ndiyo maana ameitisha warsha hiyo.

Amesema lengo la warsha hiyo inayoshirikisha maofisa wengine wa wizara hiyo ni kubainisha changamoto, kuzitafutia ufumbuzi na kuweka mpango wa utekelezaji wenye tija kwa masilahi ya Taifa.

Makamba amewataka washiriki wa warsha hiyo ambao ni makatibu wakuu, naibu makatibu wakuu, mabalozi, wakuu wa utawala balozini, wakurugenzi na wakurugenzi wasaidizi wa wizara yake, kujadili kwa upana maeneo hayo ili wizara iweze kufikia malengo iliyowekewa na Serikali.

Amewataka kuboresha mawasiliano ndani ya wizara, baina ya wizara na taasisi nyingine na wadau wake.

“Hakuna namna wizara ambayo majukumu yake ni uratibu ikafikia ufanisi unaohitajika bila kuwa na mfumo madhubuti wa mawasiliano,” amesema Makamba.

Eneo lingine umuhimu la kufanyia kazi, amesema ni wizara kuweka mfumo madhubuti wa kufuatilia utekelezaji wa matukio, ambayo imekuwa ikiyaratibu, tena kwa ufanisi mkubwa.

Matukio hayo ni masuala yanayoafikiwa katika ziara za viongozi, mikutano, makongamano ambayo yana faida kubwa kwa nchi.

“Kuna umuhimu kwa wizara kuweka mfumo wa kuwaongezea maarifa, weledi na ujuzi maofisa wetu, hususani katika uandishi na kuzungumza. Nchi yetu inasifika na kutangazika kutokana na umahiri wa wanadiplomasia wake, jambo ambalo limekuwa ni kama urithi wetu, hivyo lazima tulitekeleze kwa kuwapatia watumishi ujuzi unaohitajika,” amesema.

Ufanisi balozi za Tanzania

Katika mahojiano na Mwananchi, Machi 20, 2024, Waziri Makamba alieleza kwamba ufanisi wa balozi za Tanzania duniani ni mchanganyiko, zipo zinazofanya vizuri na zinazohitaji kuimarisha utendaji wake.

Akirejea kauli ya Rais Samia, wakati akizindua kamati aliyoiunda kufutilia utendaji wa wizara,  alisema: 

“Yale maelezo yake pamoja na matokeo ya kamati aliyoiunda kwa ajili ya kutathmini kazi ya wizara tunayapokea na tunayafanyia kazi, tunayachakata na matokeo yake ni kwamba Aprili, kuanzia tarehe 20, tumewaita mabalozi wote 46 na konseli kuu tano duniani, tutakaa sehemu huko Kibaha kwenye shule ya uongozi kwa siku nne kujadili utendaji wa kila ubalozi,” alisema Makamba.

Alisisitiza watakapowaita wangewapa KPI (vipimo vya utendaji) ambazo zimetokana na uchambuzi wa fursa na changamoto na mazingira yaliyopo katika kila balozi.

“Tunaona hiyo ni njia bora zaidi kuliko kufanya ya jumla kwa sababu vituo vinatofautiana. Balozi wetu Malawi, huwezi kumpa performance indicators (vipimo vya utendaji) vinavyofanana na vya balozi wetu wa Beijing.

“Kwa hiyo, kazi ambayo tumeifanya ni kuchambua mazingira mahususi ya kila nchi, kila ubalozi ili tuweze kutoa vipimo tofauti kwa kila balozi,” alisema.

Related Posts