MABALOZI WA TANZANIA WAJIFINGIA KIBAHA, KUTAFAKARI NA KUJIPANGA UPYA

Mabalozi wanaowakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali duniani na Wakuu wao wa utawala wamejifungia katika Chuo cha Uongozi Cha Mwalimu Julius Nyerere mjini Kibaha kwa siku 4 kuanzia tarehe 20 hadi 24 Aprili 2024.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) ametaja sababu za kujifungia huko kuwa ni pamoja na kukutana kama familia ya wanadiplomasia wa zamani na wa sasa ili kubadilishana uzoefu wa namna bora ya kutekeleza Sera ya Mambo ya Nje ambayo imejikita katika diplomasia ya uchumi.

Mhe. Makamba alisema kazi ya diplomasia ni moja ya kazi muhimu duniani na kupitia kazi hiyo Tanzania imejitangaza na kusikika, hasa kupitia misimamo yake na umahiri wa wanadiplomasia iliyokuwa nao.

Hivyo, vikao hivyo ni muhimu kwa ajili ya kupata mwendelezo huo, kwani vinatoa fursa ya kutafakari upya na kupanga mikakati ya namna bora zaidi ya kutekeleza majukumu ya Wizara hiyo ambayo ni moja ya nguzo muhimu ya ukuaji wa uchumi nchini.

Alisema mfumo wa kikao hicho ambao ni tofauti kabisa na mifumo ya vikao vilivyofanyika miaka ya nyuma ni kwamba wanadiplomasia watapewa fursa ya kubadilishana kinaga ubaga changamoto wanazokabiliana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao, kutafakari kwa pamoja namna bora ya kuzitafutia ufumbuzi na baadaye kuweka mpango kazi wa utekelezaji.

Aliwahakikishia kuwa Serikali itajitahidi kutoa nyenzo ilizo nazo ili kazi hiyo muhimu iweze kutekelezwa na kuleta matokeo chanya yanayotarajiwa.

“Tutafakari majukumu yetu, masuala mahususi ya kuzingatia pamoja na kutathimini nyenzo zetu za utekelezaji ili wote tuwe katika uelewa na mwelekeo mmoja wa kufanikisha malengo ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mama yetu, Mwana diplomasia namba moja, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan”. Mhe. Makamba alisema.


Warsha hiyo ya Mabalozi inajumuisha pia Makatibu na Naibu Makatibu Wakuu wa Wizara wakiongozwa na Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, Wakurugenzi, Wakurugenzi Wasaidizi, Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara na baadhi ya wadau wanaoshirikiana kwa karibu na Wizara katika utekelezaji wa majukumu ya Diplomasia.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na Mabalozi kuelekea warsha inayotarajiwa kuanza tarehe 21 Aprili 2024 mjini Kibaha, Pwani
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb) akizungumza kwenye kikao kazi kuelekea warsha ya Mabalozi inayotarajiwa kuanza tarehe 21 Aprili 2024 mjini Kibaha, Pwani
Sehemu ya Mabalozi wakifurahia jambo wakati Waziri Makamba akizungumza kwenye kikao cha maandalizi kuelekea warsha ya Mabalozi inayotarajiwa kuanza tarehe 21 Aprili 2024 mjini Kibaha, Pwani

Mwenyekiti wa Umoja wa Mabalozi Wastaafu Mhe. Balozi Aziz Ponary Mlima akizungumza kwenye kikao cha maandalizi kuelekea warsha ya Mabalozi inayotarajiwa kuanza tarehe 21 Aprili 2024 mjini Kibaha, Pwani

Related Posts