Dar es Salaam. Uwezeshwaji katika nyanja na fursa mbalimbali kwa watoto wa kike umeshuhudiwa kwa kiasi kikubwa katika zama hizi ambapo kuna namna mtoto wa kiume anasahaulika, wadau mbalimbali wameibuka wakitaja athari zake, huku wakitaka mtoto wa kiume pia akumbukwe na kuwekewa nguvu kama ilivyo kwa mtoto wa kike.
Hata hivyo, katika maisha, hususan Afrika mtoto wa kike hukuzwa akijua kuwa mtoto wa kiume ndiye aliyejuu, hivyo kunakuwa na heshima na uelewa juu ya maisha yao ya baadaye, lakini hivi sasa mtoto wa kike anakua akifunzwa kuwa yuko sawa na mtoto wa kiume.
Si kwamba kuna shida kwa mtoto wa kike kukua akiamini yuko sawa na yule wa kiume, lakini kinachoonekana sasa ni nguvu kubwa ya uwezeshaji kuwekezwa kwa mtoto wa kike na kumsahau mtoto wa kiume, hali ambayo imeanza kuleta athari kubwa kwenye jamii.
Hivi karibuni mwanasiasa mkongwe, Gertrude Mongella alivunja ukimya katika hilo akitaka jamii iwekeze pia kwa watoto wa kiume kwa kuwa hali ilivyo sasa inaonekana wazi wamesahaulika.
Mama Mongella anaongeza kuwa vijana wa kiume wanawake ndiyo mama zao na jambo hilo analichukulia kwa uzito, hivyo nguvu kubwa pia inahitajika katika kuwawezesha vijana wa kiume.
“Vijana wa kiume tutawapoteza na ikifikia mahali tukawapoteza, basi hata hawa watoto wa kike tunaohangaika nao watapata shida kwa sababu wataolewa na wanaume wasiojielewa,” anasema.
Mama Mongela si mwanasiasa wa kwanza kulisema hili. Desemba 2023 mbunge wa jimbo la Kongwa, Job Ndugai naye alipaza sauti akionyesha wasiwasi wake kwa jamii kumpa kisogo mtoto wa kiume kwenye suala la malezi.
“Naona kama nguvu kubwa ipo kwa mtoto wa kike, hawa wa kiume tumewaacha ndiyo tunashuhudia machokoraa, panya road, wameangukia kwenye dawa za kulevya, kwa kifupi sisi kama jamii tumewaacha.
Tunashuhudia vijana hawana uelekeo mzuri wa maisha, hii inapaswa kutushtua kama wanajamii na tuchukue hatua. Juhudi za kumuinua mtoto wa kike ziendelee, lakini tusimsahau huyu mwingine,” anasema Ndugai.
Mwanaharakati wa haki za wanawake, Glory Olomi anasema anachokiona uwezeshwaji usiwe wa ulinganifu na wanaume, lazima itambulike mwanamke ana nafasi yake, vivyohivyo mwanamume pia.
“Nafikiria katika kizazi kijacho inawezekana zikatokea harakati za kuwainua tena wanaume, kwa kuwa kwa sasa wanawake wanazaliwa wanakutana na milango na nafasi zao zikipambaniwa zaidi.
“Lazima kuwe na uzani sawa, ila tukitaka kuwasha mishumaa ya wanawake huku tunazima ya wanaume au kuwabeza hatutatengeneza usawa,” anasema Olomi.
Olomi anaongeza kwamba lazima kuwe na uangalifu pamoja na kutafuta usawa, kumwinua mwanamke kunapaswa kumuinua yeye kama yeye na si kumlinganisha.
Musa Mlela, ambaye ni mkazi wa Mwanza anasema ukiitafakari kwa uzuri ajenda ya kumuinua mtoto wa kike unaiona ina ukakasi ndani yake kwa sababu kuna namna ya kumdidimiza mtoto wa kiume.
“Sababu nguvu imeelekezwa kwa watoto wa kike na siyo tu hapa nyumbani Tanzania au Afrika pekee, bali ni duniani kote. Wanamlinda, wanampa kipaumbele na wanamtafutia nafasi zaidi ukilinganisha na mtoto wa kiume.
“Imeanza miaka mingi nyuma (shuleni, jeshini na kwenye taasisi mbalimbali), mtoto wa kiume anapoteza nafasi yake mapema sana punde tu baada ya kushindanishwa na msichana na hapa hakuna uwezo, bali ni usichana wake ndio unaompa nafasi,” ameelezea.
Akitaja madhara yake, Mlela anasema kuanzia ngazi ya familia mpaka kwenye jamii, akitolea mfano uwepo wa wazazi wa kike (single mothers) wengi kuliko miaka ya nyuma.
Anasema watoto wanapata malezi ya upande mmoja sababu kuna namna ajenda inawaaminisha wazazi hao wanaweza hata kuishi, kulea na kuongoza bila uwepo wa mwanamume.
Anaeleza kwamba vyama vya kuwainua wanawake vinaanzishwa kila kukicha na ukijaribu kuhoji unaambiwa unadidimiza juhudi za mtoto wa kike. Anasema leo mtoto wa kiume yupo hatarini kuliko wakati wowote huko nyuma, akitolea mfano nyumbani, shuleni na hata kazini.
Mwarobaini wa hali hii ni jamii na dunia kwa ujumla kuamua kuishi kwa kufuata misingi ya haki na kuepuka upendeleo bila kujali tofauti za kijinsia.
Akitaja athari zake, Mwanasaikolojia Charles Nduku anasema jambo la kwanza ni mtoto wa kiume kujihisi athaminiwi na kukosa kujiamini kwa sababu anakuwa anaona wenzake wanapewa zaidi kipaumbele.
“Ataweza hata kujichukia, mfano kuangalia kwenye harusi anayepewa elimu ni mtoto wa kike, kwani watoto wa kiume wanayoelimu ya kuishi kwenye ndoa? Jibu ni hapana, hivyo lazima kuwe na usawa kama uwezeshwaji na elimu wote wapewe.
“Unajua shida inapoanzia ni kudhani mtoto wa kiume tayari anaweza kila kitu ambapo mwisho wa siku mtoto wa kiume akaanza kuona hakuna usawa akaanza kuwachukia, akiwaona ni watu wa kupewa msaada siku zote,” anasema Nduku.
Anaongeza kuwa kwa upande wa mahusiano ya kimapenzi mwanamke kama anawezeshwa kwa kuambiwa anaweza mwenyewe basi anaweza kujiona anaweza na ikamuondolea fikra za utegemezi kwa mwanamume.
Mwanasaikolojia Bernadette Odunga anasema kitendo cha mwanamke kupewa kipaumbele kwenye nafasi mbalimbali za kijamii na mwanamume kusahaulika kisaikolojia inaweza kumuathiri na kumfanya kujisikia vibaya na kupata msongo wa mawazo.
Pia, Mwanasaikolojia Modester Kimonga anasema suala la kusahaulika kwa mtoto wa kiume maana yake taarifa zake zinakuwa hazifiki, jambo ambalo linaweza kuwanyong’onyeza.
“Piga hesabu miaka kumi inayokuja kama kila kitu atawekewa mtoto wa kike na kusahaulika kwa mwanaume, mawazo yake tutayakosa. Hivyo tunapaswa kuwekeza nguvu pande zote ili kupata matokeo bora,” anabainisha Kimonga.
Athari iliyopo mtoto wa kiume hata akifanya jambo ambalo lina matokeo kwenye jamii halifiki, kwa kuwa nguvu na masikio yote yapo kwa mtoto wa kike na kumfanya mtoto wa kiume akajiingiza kwenye mambo yasiyofaa kwa kuwa anasahaulika hata kwenye malezi.
Anasema hali hii inamnyong’onyeza mtoto wa kiume, huku akitaja jambo la kufanyika alisema wote wanahitaji nguvu ili mwisho wa siku kupata vijana wenye uzalishaji.
Hata hivyo, mwanaharakati Rebeca Gyumi, anasema msingi wa kumwezesha mtoto wa kike umejielekeza kwenye kuangalia jitihada zinazowekezwa kwake kama jitihada za kibaguzi. Lakini jitihada za kumwezesha kupata fursa zaidi zinapaswa kuangaliwa kwa jicho la tofauti.
Rebeca anasema kuna changamoto nyingi anazopitia mtoto wa kike, ndiyo maana kuna jitihada mahususi za kumuangalia mtoto huyo. Pia, kwa maono yake mtoto wa kiume yupo tayari katika fursa mbalimbali.
“Fursa mbalimbali mtoto wa kiume tayari yupo, mfano hata kwenye ushiriki wa siasa. Si kwamba mtoto wa kiume anahitaji juhudi kumwezesha, lakini kwa watoto wa kike inahitajika jitihada kwa sababu tayari kuna tamaduni za kijinsia, zitakazomfanya mtoto wa kike aanze kujiuliza maswali ajiingize au la,” anasema Rebeca.