Bukoba. Mbunge wa Bukoba Vijijini (CCM), Jasson Rweikiza amejitolea kujenga ofisi za Chama cha Mapinduzi (CCM) Bukoba Vijijini kwa gharama ya Sh150 milioni.
Taarifa ya ujenzi wa ofisi hizo zilizopatikana wilayani humo, zimethibitishwa na mbunge huyo leo Aprili 21, 2024 wakati akizungumza na Mwananchi Digital kuhusu maendeleo ya mradi huo na ulipofikia hadi sasa.
“Ni kweli CCM Bukoba Vijijini hatukuwa na ofisi za chama, hivyo niliona nianze ujenzi mara moja kwa kugharamia kila kitu ili tuweze kupata ofisi yetu, ujenzi umeanza na umefikia hatua nzuri, tunatarajia kukamilisha mwaka huu.
“Tumetumia gharama kubwa katika kusafiri kila wakati kwenda Bukoba Mjini kufanya vikao na shughuli za chama kiwilaya, sasa itakuwa mwisho,” amesema Rweikiza.
Rweikiza amesema ujenzi wa ofisi hiyo umefikia asilimia 60 na uko hatua ya kuezeka. Katika jengo hilo, amesema kuna ofisi za UVCCM, UWT, Wazazi, ofisi ya mwenyekiti, katibu wa wilaya na Tehama pamoja na ukumbi ambao utakuwa na uwezo wa kuhudumia zaidi ya watu 200 kwa wakati mmoja.
Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa CCM Wilaya Bukoba Vijijini, Deokras Byabato amesema mbunge anajenga ofisi hiyo kwa niaba ya chama kwa sababu ni muhimu kuwa na ofisi ili kuondokana na changamoto ya kutumia ofisi za kuazima.
Amesema ujenzi huo ulianza June 2023 na utakamilika mwishoni mwa mwaka huu.
“Mbunge wetu amejitolea kujenga ofisi ambayo sisi tulimuomba atusaidie kufanya hivyo, kwa sababu tulikuwa tunapata changamoto kwenye shughuli za chama, kwa sasa tunaona changamoto inakwenda kuisha,” amesema Byabato.
Mkazi wa Kijiji Katoju kilichopo Bukoba Vijijini, Philipina Antelius amesema halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Vijijini ilikipatia chama hicho kiwanja chenye na ukubwa wa ekari 10 katika Mtaa wa Bujunangoma, kata ya Kemondo ili kujenga ofisi hizo.