MTU WA MPIRA: Hili la Dube ni mtihani mwingine wa soka letu

KUNA vitu vinakera sana. Kuna vitu vinakwaza mno. Unajiuliza mpaka sasa katika dunia ya leo bado tunaishi katika zama za kale.

Ni kama hili tukio la straika wa Azam FC, Prince Dube. Ni jambo la kijinga kulizungumza katika soka la kisasa.

Dube amekimbia kambini pale Azam FC baada ya kutoa barua ya kuomba kuvunjiwa mkataba wake.

Cha ajabu ni kwamba ameomba kuvunjiwa mkataba katikati ya msimu. Nje ya dirisha la usajili. Muda ambao timu ipo katikati ya mashindano mbalimbali.

Nini kimemkuta Dube? Sijui. Ila kuna shida mahali katika soka letu. Kwanini Dube aombe kuvunja mkataba wakati ambao dirisha la usajili lilishafungwa miezi miwili nyuma? Kwanini aombe kuvunja mkataba wakati Azam FC ipo kwenye mbio za ubingwa?

Ni wazi kuwa kuna hila zimefanyika mahali. Kuna watu wamemdanganya Dube ili kuidhoofisha Azam FC. Ushahidi wa kimazingira unaonyesha hivyo.

Nilipenda namna ambavyo Azam FC ililiendea sakata hilo la Dube. Haikugoma maombi yake bali imemtaka atekeleze matakwa ya kuvunja mkataba kama walivyokubaliana.

Hata hivyo, kuvunja mkataba huo ni gharama kubwa. Ni fedha nyingi ambazo Dube hawezi kulipa. Ni fedha nyingi ambazo waliomdanyanga hawataki kulipa. Wanataka kutumia njia za panya.

Na hapa ndipo ujinga wa soka letu unapoanzia. Dube ameshauriwa kwenda kufungua kesi Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupata haki yake. Wamemshauri akane mkataba wa nyongeza aliopewa na Azam FC ambao unamuweka klabuni hapo hadi 2026.

Unawezaje kukana mkataba ambao ulipokea fedha zake? Ni ngumu. Lazima utatakiwa kutoa maelezo kwanini ulipokea fedha hizo. Utatakiwa kutoa maelezo kwanini mshahara wako umeongezeka tofauti na mkataba wako. Ni ushahidi wa wazi.

Kinachoshangaza ni kwamba wapo watu wanashabikia sakata hili kama ni jambo halali. Yaani mchezaji anaweza kuamka muda wowote na kuvunja mkataba na klabu yake nje ya makubaliano. Hapana siyo sawa.

Utaratibu lazima ufuatwe lakini waliomdanganya Dube wametaka jambo liishe kinyemela. Ndio sababu wamekwenda kufungua kesi pale TFF.

Nitashangaa kuona jambo hilo linachukua muda mrefu wakati lipo ndani ya utaratibu. Lipo kimkataba na linamalizika kisheria.

Kesi hii inafanana na ile ya Feisal Salum ‘Fei Toto’ kiasi zikitofautiana kidogo. Fei Toto alitaka kuvunja mkataba wake na Yanga. Akatumia kipengele cha kununua mkataba wake kama walivyoandikishana. Akaweka fedha kwenye akaunti ya Yanga.

Unaweza kusema alikwenda ndani ya utaratibu wa mkataba, lakini maswali ni kwanini alifanya jambo hilo katikati ya msimu? Yaani hata kama Yanga wangepokea pesa hizo wangewezaje kuziba pengo lake wakati amejitoa katika kipindi ambacho sio dirisha la usajili?

Ndicho kilichotokea kwa Dube. Ungeweza kusema alipaswa kuweka fedha anazotakiwa kuwalipa Azam FC kisha akaenda zake. Lakini je, soka la Tanzania linapaswa kuendeshwa hivyo?

Kwamba kwa kuwa mkataba wako una kipengele ambacho unaweza kuuvunja ama kupata matajiri ambao watakupa pesa ya kuuvunja uuvunje wakati wowote unaojisikia hata kama timu yako iko katika kipindi muhimu cha kusaka mataji huku wewe ukiwa mchezaji unayetegemewa tena nje ya dirisha la usajili?

Mfano kabla ya mechi ya Dabi ya Kariakoo jana, wachezaji watatu muhimu wa Simba — Clatous Chama, Henock Inonga na Che Malone wawasilishe barua ya kutaka kuondoka Simba zikiwa zimebaki dakika chache kabla ya mechi kuanza, kwa kuwa tu wamepata tajiri ambaye amewapa pesa za kuvunja mikataba yao basi wakatie katika akaunti ya Simba na kuondoka zao?

Au nyota wa Yanga — Pacome Zouzua, Khalid Aucho na Djigui Diarra wawasilishe barua za kuondoka dakika chache kabla ya mechi dhidi ya Simba kuanza na watie pesa kwenye akaunti ya Yanga na waondoke zao kwa kuwa tu mikataba yao ina kipengele cha kuvunja mkataba kwa kiasi fulani cha pesa?

Ni kama ishu ya Feisal aliyeweka pesa kwenye akaunti ya Yanga nje ya dirisha la usajili wakati timu ikimtegemea katika mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na huku pia timu hiyo ya Wananchi ikifukuzia ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Tukirudi upande wa pili kulikuwa na ulazima gani kwa Dube kutaka kuvunja mkataba wakati ambao hataweza kucheza timu nyingine hadi mwisho wa msimu? Kuna kitu hakipo sawa. Kuna namna Dube hakufikiria vizuri.

Dube angeweza kuvunja mkataba wake na Azam FC mwishoni mwa msimu na kwenda kwenye timu anayoitaka. Mbona jambo lingekuwa jepesi tu. Lakini kuna namna watu fulani wamemdanganya kwa nia ovu ya kuidhoofisha Azam FC sawa na ilivyotokea kwa watu waliotaka kuidhoofisha Yanga wakati ikiwania kuandika historia katika fainali yake ya kwanza ya michuano ya Afrika.

Hata hivyo, kwa namna soka letu linavyokua kwa kasi kesi kama hizi za kina Dube na Fei hazipaswi kuwepo tena. Ni mambo ya zamani. Kila kitu sasa kina utaratibu na ukifuatwa hakuna shida.

Nimeona majuzi Azam FC wametuma ofa kwa Yanga kumtaka Clement Mzize. Azam FC wameanza na dau la Shilingi 400 milioni. Ndivyo ambavyo utaratibu unataka.

Ukimtaka mchezaji wa timu fulani unapeleka ofa na mnafanya mazungumzo. Kama kuna kipengele kinamruhusu kuvunja mkataba wake klabu inalipa pesa na kuuvunja kisha inamsajili. Ndivyo ambavyo PSG walifanya kwa Neymar.

Kama Yanga itakubali ofa ya Mzize, tutashuhudia uhamisho ghali wa mchezaji mzawa kutoka timu moja kwenda nyingine nchini. Ni kama ilivyofanyika kwa Mrisho Ngasa wakati ule. Azam FC walipeleka ofa Yanga na kumnunua. Ndivyo mpira wa kisasa unaendeshwa.

Haya mambo ya kina Dube na Fei ni ubabaishaji ambao hautakiwi kuonekana katika soka letu kwa sasa.

Ni mambo ya ovyo na yanapaswa kukemewa haraka. Tunataka Ligi yetu iwe bora zaidi Afrika, lazima tupunguze ubabaifu huu.

Related Posts