Sheria ya Magereza yatajwa chanzo cha manyanyaso kwa wafungwa

Dar/Morogoro. Kauli iliyotolewa na Mkuu wa Jeshi la Magereza, Kamishna Jenerali, Mzee Nyamka kuhusu unyanyasaji wa wafungwa magerezani, imewaibua wadau wa haki za binadamu wakitaka Serikali iwajibike kuchukua hatua za haraka kwa kuwa mambo hayo yameshalalamikiwa sana.

Wadau hao wakiwamo wanasheria, wameikosoa Sheria ya Magereza ya mwaka 1967 kuwa imepitwa na wakati na ndiyo chanzo cha mateso kwa wafungwa.

Akizungumza jana Aprili 20, 2024 mjini Morogoro wakati akifunga mafunzo ya uongozi daraja la kwanza ngazi ya Sajenti kwa askari wa magereza wa mkoa huo, Nyamka alisema kumekuwa na malalamiko kuwa baadhi ya askari na maofisa wanawapiga wafungwa na kuwasababishia majeraha makubwa na hata vifo wakiwa ndani ya magereza.

Alikemea askari na maofisa hao akisema hataki kuona Jeshi analoliongoza linasababisha ulemavu na mauti kwa wafungwa.

Kauli ya Nyamka imetolewa wakati ripoti ya Tume ya Haki Jinai ilishaeleza hali mbaya iliyoko magerezani na kupendekeza hatua zichukuliwe.

Juhudi za kumpata Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni na Naibu wake, Daniel Sillo kuzungumzia suala hilo hazikufanikiwa baada ya simu zao kuita bila kupokewa. Hata walipotumiwa ujumbe wa maneno (sms) haukujibiwa.

Wakati Mkuu wa Magereza akikemea matukio hayo, wanasheria waliozungumza na Mwananchi wamekosoa Sheria ya Magereza ya mwaka 1967 wakisema ndiyo chanzo cha manyanyaso hayo.

Wakili Mpale Mpoki aliyewawakilisha Joseph Mbilinyi (Sugu) na Peter Msigwa katika kesi ya kupinga sheria hiyo namba 13 ya mwaka 2021, amesema walipinga manyanyaso hayo, lakini Magereza waliyakanusha.

“Namshangaa Mkuu wa Magereza kuja leo kueleza manyanyaso, wakati kwenye kesi yetu walikuja wakapinga. Tulieleza manyanyaso yote yanayoendelea magerezani yakiwamo ya kuvuliwa nguo wakati wa kupekuliwa, wakakanusha,” amesema Mpoki.

Amesema katika kesi waliyofungua Mahakama Kuu Masjala Kuu ya Dar es Salaam walishindwa.

Mpoki amesema Sheria ya Magereza ya mwaka 1967 na kanuni zake vimepitwa na lakini ndiyo chanzo cha manyanyaso kwa wafungwa.

“Sheria hiyo ni ya zamani, ilitungwa wakati ambao hatukuwa na Tamko la Haki za Binadamu katika Katiba yetu, hivyo imeshapitwa na wakati kwa kuwa haiendani na Katiba,” amesema.

Hoja hiyo inaungwa mkono na Wakili Samwel Banza wa Morogoro, aliyesema sheria hiyo inatoa kinga isiyo na kikomo kwa maofisa wa magereza kufanya wanavyotaka.

“Sheria ya Magereza ya mwaka 1967 inampa mamlaka ofisa wao kutumia nguvu kupita kiasi, huku ikimtaka mfungwa kuheshimu sheria za magereza,” amesema.

Wakili Banza amesema, “Ipo haja kwa mamlaka zinazohusika na urekebishwaji wa sera na sheria nchini kuhakikisha sheria hii ya magereza ya mwaka 1967 inabadilishwa.”

Hata hivyo,  Wakili Alhaji Majogoro anayefanya shughuli zake jijini Mwanza, amesema mfungwa akishafikishwa magereza huwa ni mali ya gereza, hivyo jeshi hilo lina wajibu wa kumtunza na kumfundisha ili asirudie makosa kwenye jamii anayoishi na si kumpiga na kumsababishia kifo na wakati mwingine ulemavu wa kudumu.

“Suala la mfungwa kupigwa maofisa wa jeshi hilo hadi kufariki dunia halikubaliki na ni kinyume cha haki za mfungwa, maana licha ya kufungwa bado ana haki ya kuishi kama walivyo wananchi wengine,” amesema.

Kwa upande wake, Peter Madeleka, wakili na mwanaharakati wa haki za raia, naye amesema sheria hiyo inahitaji marekebisho ili kuwapa haki wafungwa.

Amesema sheria hiyo inatoa utaratibu wa kuwatunza mahabusu lakini maofisa wa magereza hawaufuati.

“Sheria inasema kila mfungwa apewe godoro lake na vifaa vyake, lakini wafungwa wanajazwa sehemu moja, wanateswa. Mimi ni shahidi nilikuwa huko,” amesema.

“Kwanza sheria inatakiwa iwape wafungwa haki ya kujamiiana na wenza wao, tunapeleka kesi mahakamani ili Mahakama itamke hivyo,” amesema.

“Kuna haki za wafungwa kulipwa wakifanya kazi nje ya gereza, lakini hawalipwi. Kwenye nchi nyingine, wafungwa wakifanya kazi wanahifadhiwa fedha kwenye akaunti na wanapotoka ndipo zinakuwa mtaji wa kuanzia maisha,” amesema.

Uchunguzi wa kifo gerezani

Akizungumzia utaratibu wa kuchunguza kifo kilichotokea gerezani, Wakili John Seka amesema Magereza wanapaswa kumjulisha Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai ambaye naye ataijulisha Mahakama ili iteue korona wa kuchunguza kifo hicho.

“Kuna sheria ya uchunguzi wa vifo visivyo vya kawaida, ambayo bahati mbaya siku hizi haitumiki, lakini sheria hiyo inataka Mahakama iteue korona wa kuchunguza kifo, maana Polisi na Magereza hawatakiwi kujichunguza,” amesema.

Kauli ya mkuu wa Magereza imezungumziwa pia na Nyanda Shuli, Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, kuwa mateso kwa wafungwa ni kinyume cha sheria za nchi na mikataba ya haki za binadamu ya kimataifa ambayo Tanzania imeridhia.

“Nikiri kwamba matukio ya kupigwa, kujeruhiwa kwa wafungwa wakiwa gerezani ni jambo baya linalohitaji kuchunguzwa. Kutesa ni kinyume cha sheria zetu na Katiba,” amesema alipozungumza na Mwananchi leo.

“Ikiwa ni mahabusu, sheria inasema asipewe adhabu kabla hajakutwa na kosa, hata kwa waliofungwa, hakuna sheria iliyotamka adhabu ya mateso,” amesema.

Amesema tume hiyo imepewa dhamana kwa mujibu wa Katiba na sheria kutembelea na kukagua magereza, vituo vya polisi na maeneo mengine ya vizuizi vyote kulingana na mikataba ya kimataifa iliyoridhiwa na nchi.

“Tunakagua kuona kama maeneo hayo yana viwango vya kuweka binadamu?”

Hata hivyo, amesema mifano iliyotajwa na Mkuu wa Magereza hawajaipata, lakini watafuatilia kujua kwa undani kwa nini matukio hayo yametokea magerezani.

“Hilo ni suala linalopaswa kukemewa na tumeona tayari Mkuu wa Magereza amekemea, ni jambo baya, japo na sisi hatujalipata, lakini tutafuatilia,” amesema.

Matikio hayo yametoka kitindi ambacho Ripoti ya Tume ya Haki Jinai iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan na kutolewa Julai 16, 2023, ikiwa imependekeza kufanyika mabadiliko kwa Jeshi la Magereza.

Mapendekezo hayo yalitokana na maoni kutoka kwa wadau na wananchi kuhusu matumizi ya nguvu, ukaguzi unaotweza utu, msongamano wa wafungwa, mahabusu na wazuiliwa na uchakavu wa miundombinu ya magereza.

Tume ilisema hakuna mabadiliko chanya ya wahalifu wanaomaliza kutumikia vifungo vyao kama ilivyotarajiwa, na hali hiyo inasababisha Jeshi la Magereza kulalamikiwa kwa ukiukwaji wa haki za binadamu.

Tume ilipendekeza kuwa jina la Jeshi la Magereza lifanyiwe marekebisho ya kisheria, kifikra na kimiundo kutoka kuwa sehemu ya kutoa huduma ya kuhifadhi wafungwa na kutoa huduma ya urekebishaji.

Pia ilipendekeza mitalaa ya mafunzo ya askari magereza irekebishwe ili iendane na mabadiliko ya kutimiza majukumu ya urekebishaji ipasavyo

Related Posts