Ulinzi Yawachezesha Kwata Wapinzani Katika Darts

Bingwa wa mchezo wa vishale (Darts) wanawake Scholastica Kaizer kutoka wa timu ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (Ulinzi Sports Club) akionesha utaalamu wake wakati wa michuano ya Kombe la Mei Mosi Taifa 2024 inayoendelea Jijini Arusha.

Na Mwandishi Wetu, Arusha

WACHEZAJI Omary Mmbaga na Scholastica Kaizer wa timu ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (Ulinzi Sports Club) wameibuka mabingwa wa mchezo wa vishale (darts) wa michuano ya Kombe la Mei Mosi Taifa 2024, uliofanyika Jijini Arusha.

Wachezaji hao wazoefu wamekuwa mabingwa wa kwanza katika mashindano hayo baada ya mchezo huo kuingizwa rasmi na kuchezwa kwa mara ya kwanza katika michuano hii,

Aidha, Mmbaga ni mzoefu wa mchezo huo ambapo amekuwa na mwendeleza mzuri wa kushinda katika michezo ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali Tanzania (SHIMIWI) kwa miaka mitatu mfululizo, Michezo ya Mashirika ya Umma na Binafsi (SHIMMUTA) pamoja na masndano mengine.

Nafasi ya pili kwa wanaume imechukuliwa na Thomas Lemunge kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na nafasi ya tatu kwenda kwa Jerome Ndibalema kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Kwa upande wa wanawake nafasi ya pili imechukuliwa na Rehema Abdallah kutoka Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilfu Tanzania (TPHPA) na nafasi ya tatu imekwenda kwa Elizaberth Luwanda kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC).

Aidha, mchezo wa Netiboli umezikutanisha timu za Shirika la Viwango Tanzania (TBS) wamewafunga timu ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa magoli 34-31; nao TAMISEMI wamewachapa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) magoli 42-12.

Katika mchezo wa Kamba wanaume Idara ya Mahakama Tanzania imewavuta Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa mivuto 2-0, Ofisi ya Rais Ikulu wamewavuta Chuo cha Mipango kwa mivuto 2-0; kwa upande wa wanawake Wizara ya Afya wamewavuta Wizara ya UTamaduni kwa mivuto 2-0, Wizara ya Maji wamewavuta Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa mivuto 2-0, Wizara ya Uchukuzi wamewavuta Wizara ya Fedha kwa mivuto 2-0 na Wizara Mambo ya Ndani ya Nchi imewavuta Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilfu Tanzania (TPHPA) kwa mivuto 2-0.

Related Posts