Veneranda: Mchezaji Fountain Gate Princess anayefuata nyayo za Opah Clement

Dodoma. Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo, msemo huu unashabihiana na maisha ya Veneranda Kasimiri (17), mcheza soka katika timu ya Fountain Gate Princess.

Mbali ya soka, Venaranda ni mwanafunzi anayetarajia kufanya mtihani wa kuhitimu kidato cha sita Mei 6, 2024.

Akizungumza katika mahafali ya kidato cha sita katika Shule ya Fountain Gate jijini Dodoma, Aprili 20, 2024, Veneranda anasema alianza kucheza mpira wa miguu akiwa mdogo.

Veneranda anayesoma masomo ya mchepuo wa Sanaa (Historia, Jiografia na Kiswahili), anasema alipoanza soka alipata ukinzani kutoka kwa wazazi.

“Walikuwa wanasema mtoto mdogo akicheza mpira ataharibikiwa, lakini nilipoibuliwa na shule hii wazazi walielewa hakuna ubaya kucheza soka kwa mwanamke, wakaanza kuniunga mkono,” anasema.

Veneranda anasema hata jamii, awali ilimwona anafanya jambo lisilostahili kutendwa na mtoto wa kike.

Sasa anasema mambo yamebadilika, jamii inaona na kudhamini soka la wanawake.

Veneranda aliyesoma Shule ya Msingi ya Mlimwa A, alichaguliwa kujiunga Shule ya Sekondari ya K/Ndege zote za jijini Dodoma.

Anaeleza alipokuwa kidato cha tatu, timu ya Fountain Gate Princess iliona kipaji chake na kuamua kumpa ufadhili.

Kwa mujibu wa Veneranda, shauku yake ni kucheza soka nje ya nchi huku akiendelea na masomo, kama ilivyo kwa mwezake anayemtaja kwa jina la Mary Aron.

Veneranda aliyepata daraja la pili katika mtihani wa Taifa wa kidato cha nne, anasema kwa kawaida wanaingia darasani saa 12.00 asubuhi hadi saa 10.00 jioni.

Baada ya masomo darasani huingia kwenye mazoezi kwa saa moja na nusu. Huko hufundishwa na walimu wa soka.

Veneranda anayecheza nafasi ya winga, anasema mchezaji wa timu ya Simba Queens, Opah Clement ndiye ayemvutia katika soka la wanawake, na angependa kufikia viwango vya juu zaidi yake.

Opah ni mchezaji wa zamaji wa Simba Queens ambaye kwa sasa anacheza soka la kulipwa nchini Uturuki katika klabu ya Besktas.

Mbali na kucheza soka, anasema lengo lake ni kuwa mwanasheria, awasaidie wachezaji wenzake wanapoingia katika mgongano kisheria.

“Kila mmoja asimame katika mchezo, azidi kupambana na kujiamini aweze kufikia malengo yake. Kwa sasa michezo ni ajira,” ni ushauri wa Veneranda kwa mabinti wenzake.

Msimamizi Mkuu wa Shule za Fountain Gate, Joseph Mjingo amesema Veneranda ni miongoni mwa wanafunzi 22 wenye vipaji ambao wanafadhiliwa na Mfuko wa Fountain Gate.

Mjingo amesema wapo wanafunzi wenye vipaji na ambao shule zao huwaibua baada ya kuwaona.

Amesema wanafunzi hao si wenye vipaji katika soka pekee, bali hata kwenye kudansi, utangazaji na elimu kwa maana ya kuwa na uwezo mzuri darasani.

Ni nini kiliwasukuma kukuza vipaji katika soka la wanawake? Mjingo amesema ni kuhamasisha soka hilo nchini.

Amesema wameona mafanikio katika kuibua na kuviendeleza vipaji vya watoto wa kike kutokana na baadhi yao kunufaika na ufadhili katika vyuo vya michezo kwenye mataifa kadhaa, kama Hispania, Mali na Marekani.

Amemtaja Mary Aron, akieleza baada ya kumaliza kidato cha sita mwaka 2023 alipata ufadhili wa Euro 60,000 (Sh165.07 milioni) kwa mwaka.

Mjingo amesema baada ya Serikali kuanzisha tahasusi mpya, kuanzia Julai, 2024 nao watazianzisha zote zinazohusu michezo kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita.

Amesema wataanza na shule iliyoko Mwanza kwa sababu mazingira yake yanaruhusu, wakati wakiendelea na matayarisho kwa shule ya Dodoma.

Tahasusi za michezo zipo saba ambazo ni  Biolojia, Chakula na Lishe kwa Binadamu na Michezo (BNS); Kiingereza, Muziki na Michezo (LMS); Kiswahili, Muziki na Michezo (KMS) pamoja na Fasihili ya Kiswahili, Muziki na Michezo (FaMS),

Fasihi ya Kiingereza, Muziki na Michezo (LiMS); Kifaransa, Muziki na Michezo (FMS) na Kiarabu na Muziki na Michezo (ArMS).

Ahmed Kamugisha, mzazi wa mmoja wa wanafunzi shuleni hapo, amesema ni vyema mkazo ukawekwa katika tahasusi mpya ili kumjenga mwanafunzi kufahamu anapenda kufanya nini baadaye.

“Kijana wangu anayemaliza kidato cha sita ni miongoni mwa waliopata fursa ya kusafiri nchi za Norway na Uholanzi kwa sababu tu ya michezo. Napenda Serikali na wadau wa elimu kuongeza bidii kwenye hili,” amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dk Suleiman Jafo, aliyekuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo amesema baadhi ya tahasusi zilizoanzishwa, mbali na michezo,  zinagusa moja kwa moja suala la mazingira.

“Tunajua changamoto ya mazingira ndiyo kubwa duniani, hivi sasa tunaona hata katika nchi yetu ipo. Ukienda kule Rufiji, Ifakara, Malinyi na Arusha changamoto ni mabadiliko ya tabianchi,” amesema.

Amesema tahasusi mpya zitawajenga vijana vizuri kufahamu athari za mazingira kwa sababu ndani yake kuna baadhi ya masomo yatakayohusiana na mazingira.

Machi 20, 2024 Serikali kupitia Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ilitangaza kuanza kwa tahasusi mpya 65 kwa wanafunzi wa kidato cha tano kuanzia Julai, mwaka huu.

Uamuzi huo umefikiwa baada ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kufanya marekebisho katika mitalaa, na Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014.

Sera hiyo kwa sasa inajulikana kama Sera ya Elimu na Mafunzo ya Amali ya mwaka 2023, ambayo pamoja na mambo mengine elimu ya lazima inaishia kidato cha nne badala ya darasa la saba.

Kwa mujibu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, jumla ya shule 96 za sekondari teule ndizo zitaanza utekelezaji wa kutoa masomo ya amali.

Related Posts