Watu 50 pekee kushiriki mazishi ya CDF Ogolla

Kenya. Watu 50 pekee watashiriki kumzika aliyekuwa Mkuu wa majeshi ya Kenya, Jenerali Francis Ogolla, tovuti ya Nation nchini humo imeripoti.

Miongoni mwa watu hao atakuwemo Rais wa Kenya, William Ruto, maofisa wa ngazi za juu wa jeshi, maofisa waandamizi wa Serikali na wanafamilia.

Hata, hivyo mazishi hayo yameibua gumzo kutokana na kuwa si kawaida kwa mtu mwenye cheo kama chake, kuzikwa na watu wachache na bila jeneza kama alivyoagiza akiwa hai.

Jenerali Ogolla aliacha wosia tangu akiwa hai kuwa akifariki azikwe bila jeneza ndani ya saa 72, kama alivyoeleza Mratibu wa familia, Joel Rabuku Ogolla.

“Kwa heshima ya tabia yake ya unyenyekevu, Jenerali Ogolla alitaja kwamba mazishi yake yatafanyika ndani ya saa 72 baada ya kufariki dunia, akirejea ukweli kwamba tulitoka mavumbini na mavumbini tutarejea.”

Jenerali Ogolla anazikwa leo Jumapili Aprili 21 nyumbani kwao Kaunti ya Siaya baada ya kufariki dunia katika ajali ya helikopta Aprili 18, 2024 wakati akitekeleza agizo la Ruto.

Wakati anapata ajali ya helikopta Alhamisi, Jenerali Ogolla alikuwa katika ziara ya kutekeleza agizo la Rais Ruto, kwamba wanajeshi wafike katika shule ambazo zimeathirika na ujangili ili kuzikarabati.

Rais alitoa agizo hilo alipofungua moja ya viwanda katika Kaunti ya Pokot Magharibi Aprili 8, 2024.

Tovuti ya Taifa Leo imeripoti kuwa Jenerali Ogolla alikuwa anaharakisha kazi hiyo imalizike kwa wakati kama ilivyopangwa na kikosi cha wanajeshi kilifika katika shule hizo kwa muda uliotakiwa.

Hata hivyo, Mkuu wa Majeshi na wanajeshi wengine tisa walifariki wakiwa katika kazi hiyo eneo la Sindar, Kaben, Kaunti ya Elgeyo Marakwet dakika chache baada ya kuondoka kwenye Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Cheptulel katika Kaunti ya Pokot Magharibi.

Kabla ya kukutana na mauti Jenerali Ogolla alizuru Shule ya upili ya Wavulana ya Cheptulel, iliyopo Chesegon kwenye mpaka wa Kaunti za Pokot Magharibi na Elgeyo Marakwet, ambayo haina wanafunzi.

Wanafunzi wa shule hiyo wako katika Shule ya Msingi ya Surumben Wadi ya Masol, umbali wa kilomita 50 kutoka eneo hilo.

Related Posts