Ajali yaua 13 Kilwa | Mwananchi

Kilwa. Watu 13 wamefariki dunia na wengine sita kujeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea eneo la Somanga Wilayani Kilwa Mkoa wa Lindi.

Akizungumzia ajali hiyo leo Jumatatu Aprili 22, 2024  kwenye eneo la tukio, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, John Imori, amesema ajali hiyo imetokea saa 1:30 asubuhi.

Amesema gari dogo la abiria aina ya Mazda lililokuwa likitokea Somanga kuelekea Nangurukuru, limegongana uso kwa uso na lori la mafuta katika barabara kuu ya Lindi – Kibiti.

Kamanda Imori amesema gari lenye namba za usajili T224 DZT lililokuwa likiendeshwa na Abdalla Hamisi (37) mkazi wa Mbagala, Dar es Salaam akitokea Lindi kuelekea jijini Dar es Saalam, liligongana uso kwa uso na gari lenye namba za usajili T707DSX aina ya Mazda lililokuwa likiendeshwa na Saidi Issa (29), mkazi wa Somanga aliyekuwa anatokea Somanga kuelekea Nangurukuru na kusababisha vifo vya watu hao 13.

“Huyu dereva wa lori alihama upande wake na kulifuata gari la abiria bila kuwa na tahadhari yoyote na kusababisha vifo vya watu 13,” amesema Kamanda Imori.

Amesema miili ya marehemu imefanyiwa uchunguzi na kukabidhiwa kwa ndugu zao kwa ajili ya utaratibu wa maziko na majeruhi sita wanaendelea kupatiwa mjatibabu.

“Miili tisa ilichukuliwa pale pale kwenye tukio na ndugu zao, lakini miili minne tuliipeleka hospitalini Tingi lakini nayo tayari ndugu wameshaichukua,” amesema.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kilwa, Jordan Maliga, amesema wamepokea maiti nne za wanaume na zote zimeshachukuliwa na ndugu zao.

Amesema majeruhi waliofikishwa hospitalini hapo watano wamepelekwa hospitali ya Wilaya ya kinyonga kwa ajili ya matibabu zaidi na mmoja wamebaki naye.

“Hapa hospitalini zilikuja maiti nne na majeruhi sita, maiti tisa zilichukuliwa na ndugu zao eneo la tukio, na hii miili minne iliyoletwa hapa hospitali nayo tayari imeshachukuliwa. Majeruhi sita tuliowapokea, watano wamepelekwa hospitali ya Wilaya ya Kinyonga kwa matibabu zaidi,” amesema Dk Jordan.

Akizungumzia hali za madereva, Kamanda Imori amesema wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano zaidi.

Kamanda huyo ametoa wito kwa madereva kuwa makini wawapo barabarani, ili kuepuka ajali ambazo zinapoteza uhai wa watu wengi.

Related Posts