MWENYEKITI wa Wazazi CCM Mkoa wa Morogoro, Dk. Rose Rwakatare ametoa msaada wa tani tano za mchele kwa waathirika wa mafuriko wa jimbo la Mlimba mkoani humo. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea)
Alikabidhi msaada huo leo kwa Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Dunstan Kyoba katika hafla ambayo imefanyika ofisini kwake mkoani Morogoro.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada huo, Dk. Rose amesema amezaliwa Mlimba hivyo ameguswa sana kuona wananchi wenzake wanaishi maisha ya shida.
“Mimi ni mzaliwa wa Mlimba, kwa hiyo hapa ni nyumbani kwangu ndiyo maana nimeamua kuja kulia na wanaolia, tufarijiane wakati huu mgumu, sijaja bure nimekuja na mifuko 1,000 ya mchele angalau wapate chakula,” alisema
Amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutuma ujumbe kupeleka msaada wa vitu mbalimbali na kuwaomba wadau mbalimbaali waendelee kupeleka msaada.
“Hata ukiwa na mfuko mmoja wa mchele, unga unakaaribishwa kuja kusaidia watanzania wenzako, sisi ni watanzania na tunajulikana dunia nzima kwa upendo,” amesema.
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Dunstan Kyoba amemshukuru Dk. Rose Rwakare kwa upendo aliouonyesha kwa wakazi wa Mlimba na kuwaomba wadau wengine kuiga mfano huo na kwenda kusaidia.
Amesema msaada huo umekuja wakati mwafaka kwani wananchi wa maeneo yaliyoathirika na mafuriko wanahitaji nfaraja na kushikwa mkono wakati huu.
“Napenda kutoa wito kwa viongozi wengine na wafanyabiashara waige mfano wa Dk. Rwakatare waje kusaidia wananchi ambao wako kwenye wakati mgumu wakati huu,” amesema
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kilombero Mohamed Msuya, amempongeza Dk Rose kwa msaada alioutoa kwa wananchi hao.
Alisema msaada huo ni wa kuigwa na wa mfano kwa wananchi wa wilaya yaa Kilombero bila kujali itikadi za kisiasa.
“Tumpongeze sana Dk. Rose kwa kuwa na maono ya kuwasaidia wananchi wa Kilombero, kutoa ni moyo wala skiyo utajiri kwasababu kuna watu wana vingi lakini hawana moyo wa kutoa,” amesema
“Nawaomba sana watanzania wote bila kujali itikadi kujitokeza kuwasaidia wananchi wa Jimbo la Mlimba waliopata shida ya mafuriko na tutampa ushirikiano wa kutosha yeyote atakayeleta msaada,” amesema
“Dk Rose Rwakatare ni mfano wa kuigwa kwa wananchi wa Wilaya ya Kilombero, huyu anamoyo wa kipekee kwasababu kila linapotokea tatizo amekuwa msaada mkubwa kwenye Wilaya ya Kilombero,” amesema Msuya
Alisema kuna watu wanataka kutoa msaada lakini wanaogopa kutokana na sababu za kisiasa hivyo amewatoa hofu kwamba wajitokeze kusaidia kwani CCM na Serikali zitawalinda kwa kuwa siasa ni mpaka 2025.
“Kwa sasa hakuna siasa hapa tunaamini tunamadiwani na wabunge lakini tuko kwenye utendaji hatuko kwenye siasa kwa hiyo Dr. Rose najua una marafiki huko mjini, wewe ni Mwenyekiti wa Wazazi CCM mkoa wa Morogoro, unawadau wengi tunajua unauwezo wa kuhamasisha wananchi wakaja kuleta misaada,” alisema