Ushindi wa mabao 2-1 ambao Yanga iliupata dhidi ya Simba katika dabi ya Kariakoo, Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, yanaweza kuwa matokeo yaliyorahisishwa kwa kiasi kikubwa na timu iliyopoteza mchezo huo.
Hakikuwa kibarua kigumu kwa Yanga kupata ushindi katika mechi hiyo tofauti na uhalisia unaotakiwa wa timu kupaswa kufanya kazi ngumu kupata ushindi kwenye dabi kama ambavyo tumeshuhudia miaka ya nyuma kwenye mechi baina ya timu hizo.
Muendelezo wa makosa yanayojirudia rudia kwenye safu ya ulinzi ya Simba, lakini pia kwenye ushambuliaji kulipunguza kazi ya benchi la ufundi la Yanga katika maandalizi ya mchezo huo kwani isingekuwa rahisi kwa wapinzani wao kubadilika ndani ya muda mfupi na kuja na kitu cha tofauti Jumamosi.
Ni mechi ambayo Simba itapaswa ijilaumu yenyewe kutokana na nafasi nzuri za mabao ilizopata kwenye mchezo huo hasa katika kipindi cha kwanza na ikashindwa kuzitumia tofauti na wapinzani wao ambao walipata chache na wakazitumia.
Katika dakika 10 za mwanzo, Clatous Chama alipiga shuti kali lililotemwa na kipa Djigui Diarra lakini akakosekana mmaliziaji, baadaye Kibu Denis alipata nafasi nzuri ya kuifungia bao timu yake akapiga shuti lililotoka nje lakini pia Sadio Kanoute alipata nafasi ya kufunga kwa kichwa lakini aliuelekeza mpira mikononi mwa kipa wa Yanga.
Na hata kipindi cha pili, zipo nafasi zilizopatikana ambazo zingeweza kuinufaisha Simba lakini bado tatizo likawa katika kutumika kwake hadi pale Freddy Michael Koublan alipowafungia bao pekee kwenye mchezo huo.
Haikuwa suala la bahati mbaya kwa Simba kupoteza nafasi katika mchezo huo kwani limeonekana kuisumbua msimu huu mzima katika mashindano ya ndani na yale ya kimataifa.
Kabla ya mechi dhidi ya Yanga juzi, Simba ilikuwa imefunga mabao mawili tu katika mechi nne mfululizo ambazo ilicheza ikiwa ni wastani wa bao 0.5 kwa mchezo, takwimu ambazo sio nzuri kwa timu kama Simba.
Kana kwamba haitoshi unaweza kujiridhisha katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu ambapo hadi Simba inatolewa katika hatua ya robo fainali, ilikuwa inashika nafasi ya nne katika chati ya timu zilizopoteza nafasi nyingi ambapo ilipoteza nafasi 11.
Ulinzi wa lango katika soka ni sanaa lakini pia ni tabia ambayo ni vigumu kubadilika haraka ndani ya muda mfupi na hiki kinaweza kujidhihirisha kwa Simba katika mechi ya juzi dhidi ya Yanga.
Kabla ya kukabiliana na Yanga juzi, Simba haikuwa na mwenendo mzuri katika namna inavyojilinda na mara kwa mara ilikuwa ikifanya makosa ambayo hayakuonyesha kama ilikuwa na sanaa nzuri ya kulinda lango lake lakini pia ilikuwa na muendelezo wa kufanya makosa binafsi ambayo mara kadhaa yaliigharimu timu.
Makosa sugu ambayo Simba ilikuwa inayaonyesha hasa yalikuwa ni kuchelewa kujipanga na kuwepo kwenye maeneo sahihi pindi timu inapopoteza mpira lakini kosa la pili ni kosa la kutotimiza au kutofanya majukumu ya msingi wanayohitajika kufanya ndani ya uwanja pale wapinzani wanapokuwa na mpira.
Ni makosa ambayo juzi yaliendelea na kuinufaisha Yanga katika mabao yote mawili ambayo ilipata yakipachikwa na Stephane Aziz Ki na Joseph Guede katika kipindi cha kwanza.
Bao la kwanza la Yanga ambalo lilikuwa la penalti lilikuja baada ya Hussein Kazi kufanya kosa binafsi la kupoteza mpira kwa Aziz Ki huku akiwa katika mazingira ambayo angeweza kurahisisha kwa kuutoa mpira nje huku kuifanya timu ijipange au kucheza faulo ya kimbinu nje ya eneo la hatari ili kutosababisha kutokea mazingira ya bao au penalti kama ilivyotokea.
Ndani ya eneo la hatari,Hussein Kazi akacheza faulo kwa Aziz Ki katika eneo ambalo tayari beki mwenzako, Che Fondoh Malone alikuwa ameshajiandaa kumpa sapoti huku akimchelewesha Aziz Ki kufanya uamuzi.
Lakini ukiachana na makosa ya Kazi, kwenye bao hilo baadhi ya wachezaji wa Simba hasa wa safu ya ulinzi hawakutimiza jukumu la kuziba nafasi kwa haraka baada ya mpira kunaswa na wapinzani .
Stephane Aziz Ki wakati anafanya shambulizi lililozaa penalti, alikuwa na uwezekano wa kuwapasia Joseph Guede na Clement Mzize ambao walikimbia kwa kasi kwenye eneo la hatari la Simba baada ya Yanga kupora mpira kutoka kwa Kazi.
Bao la pili la Yanga lililofungwa na Joseph Guede lilitokana na beki wa kushoto wa Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ kujisahau na kuvunja mtego wa kuotea ambao walinzi wenzake waliuweka wakati Yanga ilipokuwa inatengeneza shambulizi.
Timu inapotengeneza mtego wa kuotea, mabeki wote wanapaswa kuwa katika mstari mmoja na mlinzi kiongozi wa kati jambo ambalo Tshabalala hakulifanya na kujikuta akiigharimu Simba kwa kufungwa bao la pili.
Makosa ya aina hiyo hayakuwa mageni kwa Simba kwani yamejitokeza katika idadi kubwa ya mechi msimu huu na kuonyesha kuwa yalikuwa yakielekea kuigharimu kwenye mechi dhidi ya Yanga.
Kabla ya kuikabili Yanga, mechi nne nyuma zilizopita za mashindano tofauti, Simba ilikuwa imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara tano na katika kila mchezo kati ya hiyo minne iliruhusu bao.
MAREFA WAMEIHESHIMISHA DABI
Refa wa kati, Ahmed Arajiga na wasaidizi wake Mohammed Mkono na Kassim Mpanga walionyesha kiwango kizuri katika mechi ya juzi kilichochangia dabi imalizike salama pasipo malalamiko yoyote kwa upande wao.
Walifika kwenye maeneo waliyopaswa kuwepo kwa wakati na walitafsiri vyema na kwa haraka matukio tofauti yaliyojitokeza kwenye mchezo huo kwa mujibu wa sheria 17 za mchezo wa mpira wa miguu.
Bao la Joseph Guede linaweza kuwa mfano bora wa namna marefa walivyotimiza vyema majukumu yao kwani kama msaidizi Mohammed Mkono asingekuwepo katika sehemu sahihi na kufuatilia pasipo uhakika shambulizi lililozaa bao hilo, angeweza kuonyesha kibendera cha kuashiria Guede ameotea lakini aling’amua kwa haraka kuwa mshambuliaji huyo hakuotea japo tukio lilifanyika kwa haraka mno.
Lakini pia mwamuzi Arajiga alijitahidi kuwa rafiki wa wachezaji ndani ya uwanja jambo lililochangia kuufanya mchezo usiwe umetawaliwa na jazba na vurugu.
Kulikuwa na wachezaji kutoka mataifa 11 tofauti walioanza katika vikosi vya timu hizo juzi ambapo kati ya hao, nyota wa Kitanzania walikuwa sita huku 16 wengine wakitoka mataifa 10 tofauti.
Hata hivyo, walikuwa ni nyota wa kigeni ambao waliiamua mechi hiyo kwa mara nyingine kama ilivyokuwa katika mchezo wa mzunguko wa kwanza kutokana na kuhusika na mabao yote matatu yaliyopachikwa juzi.
Mabao mawili ya Yanga yalifungwa na wageni na pasi iliyozaa bao moja ilitoka kwa mgeni ambaye ni kiungo Khalid Aucho.
Bao pekee la Simba lilipachikwa na mgeni na aliyepiga pasi ya mwisho ni Clatous Chama kutoka Zambia.
Dabi za hivi karibuni kwenye Ligi Kuu zimeendelea kuwa chungu kwa makipa kutokana na nyavu zao kutikiswa ambapo katika mechi nne mfululizo, imeshuhudiwa kila timu ikiruhusu bao na hivyo makipa kushindwa kumaliza wakiwa hawajaruhusu bao (clean sheet).
Tofauti na mechi ya mzunguko wa kwanza ambayo viungo walitamba kwa kufunga mabao manne kati ya sita yaliyopachikwa kwenye mchezo huo, juzi waliomaliza kibabe walikuwa ni washambuliaji ambao walipachika mabao mawili kati ya matatu ambayo yalipatikana.
Kiungo Jonas Mkude hajapoteza mechi sita mfululizo za dabi ya Kariakoo kwenye Ligi Kuu ambapo nne alikuwa kwenye kikosi cha Simba na mbili hajapoteza akiwa anaitumikia Yanga.
Kwa mara ya kwanza, wachezaji kutoka Ivory Coast wamefunga mabao katika mechi ya Kariakoo Dabi kupitia mabao ya Joseph Guede na Freddy Michael.