Mbeya. Siku moja baada ya mgombea uenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, Mchungaji Peter Msigwa kumtaka mpinzani wake, Joseph Mbilinyi “Sugu” kwenye meza ya mdahalo, mpinzani wake huyo amesema yupo tayari wakati wowote.
Jana, Jumapili Aprili 21, 2024 akirejesha fomu ya kutetea nafasi yake, Mchungaji Msigwa alimtumia salamu Sugu akimtaka kwenye mdahalo mmoja ili kuulizwa maswali ya msingi akisema licha ya kuwa na urafiki, lakini hajamuelewa katika mchakato huo utakaofanyika mwezi ujao.
“Nimuombe Katibu Mkuu (Chadema- John Mnyika) atupe mdahalo mmoja na Sugu ili tushindanishe sera zetu, tuone nani mwenye uwezo. Chama kinahitaji watu wenye uwezo wa kukitangaza kama ambavyo tumeisimamisha Mbeya kwa muda,” amesema Mchungaji Msigwa ambaye ni mbunge wa zamani wa Iringa Mjini.
Alichokisema Sugu
Hata hivyo, Sugu ambaye ni mbunge wa zamani wa Mbeya Mjini, amejibu mapigo hayo kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X zamani Twitter akisema: “Nasikia kuna mtu anataka mdahalo na mimi…well (vizuri) niko tayari any time (wakati wowote).
Mmoja wa wananchi waliochangia andiko hilo, Eric Michael alimwambia Sugu kuwa anamheshimu lakini mdahalo sio mistari na katika hilo Msigwa yupo juu, ni bora ajikite katika mikutano ya hadhara.
Akijibu ujumbe wa Michael, Sugu amesema: “Hunijui vizuri wewe, mwaka 1998 nikiwa nina umri wa miaka 26, nilitoa mada katika mdahalo wa Chuo Kikuu cha Amsterdam (Uholanzi), sijui wewe ulikuwa wapi.
Kanda ya Nyasa inayoundwa na mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe, Songwe na Rukwa, uchaguzi wake unatajwa kuwa na ushindani mkali kutokana na kila mgombea kuwa na nguvu kwa namna walivyojipanga kuelekea katika mchakato huo.
Leo Jumatatu Aprili 22, 2024, Mwananchi Digital limemtafuta Sugu ambaye ni mjumbe wa zamani wa kamati kuu ambapo amesisitiza yupo tayari kwa mdahalo muda wowote na mahali popote atashiriki.
“Kama kutakuwa na tatizo maandalizi, nipo tayari kugharamia, kwa sababu najiamini,” amesema Sugu.
Mchuano wa uchaguzi wa Kanda ya Nyasa unanogeshwa zaidi na hatua ya Mchungaji Msigwa kuchukuliwa fomu ya kutetea nafasi hiyo na makada wanaomuunga mkono waliomsafirishia hadi Iringa anakoishi. Vivyo hivyo kwa Sugu aliyechukuliwa fomu na watu wanaomuunga mkono waliompelekea nyumbani kwake jijini Mbeya.
Hatua ya Sugu na Msigwa kuwania kiti hicho kumewagawa baadhi ya makada wa chama hicho wakiwemo wabunge na viongozi wa zamani wa Chadema, waliojipambanua wazi bila kificho kutangaza kumuunga mkono mgombea fulani kwa sababu mbalimbali.
Makada wanaomuunga mkono Mchungaji Msigwa, wanasema bado na wana imani na mjumbe huyo wa kamati kuu ya Chadema. Wakati wanachama wanaomuunga mkono Sugu wanasema ni wakati mwafaka kwa Nyasa kufanya mabadiliko na kuwa na mwenyekiti mpya.
Hata hivyo, Mwananchi inazo taarifa pia kuwa wapo wajumbe wa kamati kuu na baraza kuu waliojigawa pande mbili za Sugu na Msigwa, ingawa wao hawataki kuonekana hadharani kwa hatua ya sasa.
Mwenyekiti anayemaliza muda wake, Mchungaji Msigwa alishinda nafasi hiyo mwaka 2019, baada ya kumshinda wakili maarufu Boniface Mwambukusi kwa kura 67 sawa asilimia 62.3, dhidi ya 26 sawa na asilimia 24 alizopata mshindani wake, Sadick Malila aliambulia kura 14 sawa asilimia 13.2.
Awamu ya kwanza ya mwaka 2016, Mchungaji Msigwa alimshinda Patrick Ole Sosopi aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha) na mjumbe wa kamati kuu ya chama hicho kwa sasa.
Victoria moto
Mchuano mwingine utakuwa katika Kanda ya Victoria inayounda mikoa ya Mwanza, Kagera na Geita ambapo itakuwatanisha vigogo Ezekiah Wenje anayetetea nafasi hiyo, akichuana na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), John Pambalu.
Wenje aliyewahi kuwa mbunge wa Nyamaga mkoani Mwanza 2010-2015 anawania nafasi hiyo kwa muhula wa pili, wakati Pambalu aliyegombea jimbo hilo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, anajitosa kwa mara kwanza kuwani ubosi wa kanda.
Magharibi, Serengeti kimya kimya
Wakati wagombea kanda za Nyasa na Victoria wakipambana hadharani, hali ni tofauti katika kanda za Magharibi na Serengeti, wanaowania uenyekiti wamekuwa na staili ya kuchukua fomu kwa kuviziana au kimya kimya kwa njia ya mtandao wakihofia kuhujumiana na kuchezewa rafu.
Hata hivyo, ikiwa leo Aprili 22, 2024 ndio dirisha la kuchukua na kurejesha fomu za uenyekiti wa kanda na nafasi zingine linafungwa.
Kanda za Serengeti na Magharibi zinaunda mikoa ya Katavi, Tabora, Shinyanga, Kigoma, Mara, Simiyu.
Kwa mujibu wa Chadema, baada ya mchakato wa kurejesha fomu kukamilika hatua inayofuata ni uteuzi utakaofanywa na kamati kuu.