Kagera. Wanawake 347 mkoani hapa wamebainika kuwa na maambukizi ya saratani ya mlango wa kizazi baada ya kufanyiwa uchunguzi.
Jumla ya wanawake 4,689 wamefanyiwa uchunguzi wa saratani hiyo mkoani Kagera.
Akizungumza leo Jumatatu Aprili 22, 2024, katika maadhimisho ya chanjo Afrika yaliyofanyika Manispaa ya Bukoba, Mganga Mkuu wa Mkoa Kagera, Samwel Raizar amesema mkoa huo unafanya kampeni ya kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi kwa wasichana walio chini ya miaka 14.
Amesema Kagera ni miongoni mwa mikoa inayoathiriwa na magonjwa yanayodhibitika kwa chanjo ikiwamo wa saratani ya mlango wa kizazi.
Dk Raizar amesema takwimu za mwaka jana na mwaka huu kwa Mkoa wa Kagera zinaonesha kuna kiwango kikubwa cha ongezeko la wagonjwa wa saratani hiyo.
“Takwimu za mwaka 2023, zinaonesha wanawake waliofanyiwa uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi ni 17,668 na wanawake 469 walibainika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo,” amesema.
Amesema kwa Januari pekee mwaka huu, wanawake 4,689 wamefanyiwa uchunguzi na 347 wamekutwa na maambukizi.
Hivyo, Dk Raizar amewaomba wazazi na wanawake wawaruhusu mabinti zao kwenda kupatiwa chanjo ya HPV ili kuwanusuru na saratani hiyo.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Abdoni Kawha ambaye ni Mwakilishi wa Ofisa Elimu Mkoa Kagera, amesema jumla ya wanafunzi 17,600 kutoka shule 362 watapatiwa chanjo na wamejipanga kuhakikisha walengwa wote kutoka shule hizo wanafikiwa.
Mratibu wa Chanjo Mkoa wa Kagera, Salimu Kimbao amesema wamepokea dozi 299,040 na tayari zimesambazwa kwenye vituo vyote vya Mkoa wa Kagera.
“Tumelenga kuwakinga walengwa wote kwa kila halmashaur na uzinduzi unaendelea na huduma ya kutoa chanjo pia inaendelea kila mahali,” amesema Kimbao.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Erasto Sima amewataka wanaosimamia kazi hiyo ya chanjo, kuhakikisha wanawafikia walengwa wote kwa wakati.
“Hatutarajii kuona eneo fulani limeachwa, vifaa na chanjo visimamiwe na kutumika ipasavyo, fedha zote zinazotolewa na Serikali zitumike kwa kuzingatia kanuni na taratibu za nchi,” amesema.