GGML yasisitiza kuendelea kuimarisha afya za wafanyakazi

KAMPUNI ya Geita Gold Mining Limited kwa kushirikiana na kampuni mbalimbali imeahidi kuendelea kusimamia mipango ya kuimarisha na kusimamia afya za wafanyakazi dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Hayo yamebinishwa katika kongamano la kwanza la mashirika na kampuni hizo (CWC) lililofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam. Kongamano hilo liliandaliwa na taasisi ya Umoja wa Kimataifa ya Global Compact, Global Compact Network Tanzania (GCNT), kwa kushirikiana na ImpactAfya Limited ili kujenga uelewa kuhusu umuhimu wa afya miongoni mwa makampuni.

Mganga mkuu wa GGML, Dk Aalen Mtemi, alisema kampuni hiyo imejitolea kikamilifu kwa ustawi wa wafanyakazi wake na jamii kwa ujumla.

“Mtazamo wa GGML kuhusu ustawi wa wafanyakazi unaenea zaidi ya usalama wa kimwili,” alisema Dk Mtemi wakati wa mjadala katika mkutano huo.

Marsha Macatta-Yambi, Mkurugenzi Mtendaji, Global Compact Network Tanzania (kushoto) na Bhakti Shah, Mwanzilishi na Mkurugenzi Mkuu wa ImpactAfya Ltd, ambao ni waandaaji wenza wa Kongamano la kwanza la Ustawi wa Biashara lililofanyika Hyatt jijini Dar es Salaam.

Aliangazia mipango ya ustawi wa kampuni iliyopo, huku kampuni ikitoa rasilimali nyingi katika kuimarisha afya ya akili na kuanzisha programu za afya ili kusaidia ustawi wa jumla wa wafanyakazi wake.

CWC ilileta pamoja viongozi wa sekta hiyo ili kujadili jukumu muhimu la programu za ustawi wa shirika katika kupunguza athari za magonjwa yasiyo ya kuambukiza (NCDs) na kukuza hulka ya kufanya mazoezi endelevu.

Baadhi ya programu za kampuni ni pamoja na vituo vya matibabu vilivyo kwenye maeneo yao ya kazi pamoja na kuanzisha program zinazotunza siri za wagonjwa ili kuimarisha utoaji wa elimu ya akili.

“Mipango hii inaonyesha dhamira ya kina kwa usalama wa wafanyakazi, afya ya mwili na uwajibikaji wetu katika mazingira,” aliongeza Dk Mtemi.

Mwanzilishi na mkurugenzi mkuu wa ImpactAfya Ltd, Bhakti Shah alisema; “Ilikuwa muhimu kwetu kuja na jukwaa ambalo tunaweza kujenga ufahamu, ambapo tunaweza kujadili masuala ya afya na magonjwa yasiyo ya kuambukiza. Tunaweza kupata suluhisho kwa sababu ustawi wa wa afya ya binadamu ndio taaluma yenyewe,’ alisema.

Mkutano huo uligusia pia mada kadhaa muhimu kwa ustawi wa wafanyakazi ambapo katika majadiliano hayo ambayo yalilenga kuzungumza kuongezeka kwa magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) kama vile magonjwa ya moyo, kisukari na saratani, watalaam mbalimbali walieleza jinsi hali hizi zinavyoweza kuwa na athari kubwa kwa afya ya mfanyakazi na kuzorotesha tija na mafanikio ya biashara kwa ujumla.

Mkutano huo pia uliangazia umuhimu wa mipango ya kutoa elimu ya afya ya akili mahali pa kazi, kwa kutambua jukumu muhimu ambalo mfadhaiko na wasiwasi vinaweza kuzorotesha utendaji wa mfanyakazi.

Related Posts