Kombe la Muungano lilifia hapa

KLABU ya Yanga ya Dar Es Salaam imegoma kushiriki mashindano mapya ya Kombe la Muungano, yatakayofanyika Aprili 23 hadi 27 mjini Zanzibar.

Rais wa Shirikisho la soka Zanzibar (ZFF), Suleiman Mahmoud amesema kwamba timu za Simba na Azam FC ndizo pekee kati ya zilizopewa mwaliko kutoka Bara zilizothibitisha kushiriki.

Mahmoud ameeleza kuwa walipokea barua ya Yanga SC mapema ambapo klabu hiyo iliomba kutoshiriki mashindano hayo ya maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano kutokana na kuwa na ratiba ngumu.

Mashindano hayo yameandaliwa na Shirikisho la Soka la Zanzibar, ZFF, kwa kushirikiana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), yakiwa na lengo la kuitikia wito wa Rais Samia Suluhu Hassan juu ya kuuenzi Muungano.

Jumamosi Novemba 25, 2023, katika Viwanja vya Ikulu ndogo vilivyopo Tunguu Zanzibar, akiipongeza timu ya Taifa ya Zanzibar ya vijana chini ya miaka 15 iliyochukua Kombe la Cecafa nchini Uganda, Rais Samia alisisitiza kuchezwa kwa mashindano ya Muungano na fainali yake ifanyike wakati wa kilele cha Sherehe za Muungano.

Kwa hiyo ZFF na TFF wakakutana na kupanga kufanyika kwa mashindano hayo kuanzia mwaka huu.

Kuanzia mwaka 1982 hadi 2003, Tanzania kulikuwa na mashindano yaliyoitwa Ligi ya Muungano, iliyokuwa ikiandaliwa na Chama cha Soka cha Tanzania, FAT, na Chama cha Soka cha Zanzibar, ZFA.

Kimsingi hii ndiyo ilikuwa Ligi Kuu ya Tanzania na bingwa wake ndiye aliiwakilisha Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Yalıshirikisha timu bora za juu kutoka ligi zote mbili za pande za Muungano, Bara na Visiwani.

Mwaka wa kwanza kabisa, 1982, zilishiriki timu nne, mbili za Bara na mbili za Zanzibar. İdadi ikawa inabadilika hadi kufika 2003 zikashiriki timu nane, nne za Bara na nne za Zanzibar.

Mwaka wa mwisho wa mashindano hayo, 2003, Yanga hawakuwa na sifa ya kushiriki moja kwa moja. Walipewa nafasi ya upendeleo baadaye sana ili kufanikisha mashindano kutokana na mtafaruku uliotokea awali.

Ligi ya Muungano ilikuwa ikifanyika kuanzia Oktoba, baada ya ligi za Bara na Zanzibar ambazo zilianza Februari kuwa zimemalizika.

Mwaka 2003 Ligi Kuu Bara ilichelewa sana kumalizika kutokana na mgogoro mkubwa ulioikumba FAT. Mwenyekiti Muhidin Ndolanga (marehemu) na katibu Michael Wambura, walisimamishwa na Kamati ya Utendaji ya FAT kutokana na matatizo mbalimbali ya kiutawala.

Nafasi zao zikachukuliwa na kamati ya muda chini ya mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa Mtwara, Yahya Mhata na katibu mkuu wa Chama cha Makocha (TAFCA), Mwina Kaduguda, mtawalia. Kutokana na misukosuko iliyotokea ikasababisha Ligi Kuu Baara ichelewe kuisha kwani viongozi wote walikuwa ‘bize’ kupigania madaraka.

Ligi hiyo ambayo ilitakiwa iishe Septemba, ikaenda hadi Novemba 26. Shirikisho la Soka Afrika, CAF, lilipanga siku ya mwisho ya kupokea majina ya wawakilishi wa kila nchi kwenye mashindano ya Afrika kuwa ni Desemba 24.

Kucheza ligi ya nyumbani na ugenini kama ilivyopangwa awali isingewezekana kutokana na ufinyu wa muda. Kutokana na hilo, waandaaji wa ligi, FAT na ZFA wakakubaliana wabadili mfumo wa mashindano kutoka kucheza kwa mtindo wa kuhesabu alama kwa michezo ya nyumbani na ugenini hadi mfumo wa mtoano utakaoanza na nusu fainali.

Zilitakiwa timu sita, tatu za Bara na tatu za Zanzibar. Lakini idadi hiyo isingefanisha mashindano ya mtoano, hivyo wakakubaliana waongeze timu moja moja kutoka kila upande ile iliyomaliza nafasi ya nne kwenye ligi.

Yanga waliomaliza wa nne kwenye Ligi Kuu Bara wakaangukiwa na embe dodo pamoja na Maendeleo FC ambayo ilimaliza nafasi ya nne Zanzibar. Yanga wakapangwa kucheza na Jamhuri ya Pemba, Desemba 10, 2003, kwenye Uwanja wa Gombani.

Wakatoka Dar es Salaam kwenda Pemba kupitia Unguja. Walipofika hapo wakagoma kwenda Pemba wakisema wamegundua kwamba duniani hakuna ligi ya mtoano kwa hiyo wao hawapo kucheza mechi za mtoano.

Ili mambo yasiwe mengi, waandaaji wa mashindano wakaitoa Yanga na kuipa ushindi wa mezani Jamhuri SC. Yanga wakapinga kutolewa, wakaenda kufungua kesi Mahakama ya Ilala kwa hakimu Agatha Kabuta. Mahakama ikapanga kuisikiliza kesi hiyo Februari 2004.

Ili kuwahi tarehe za mwisho za CAF kupokea majina ya wawakilishi wa mashindano ya Afrika, FAT za ZFA zikateua mabingwa wa kutoka kila upande kwenda kushiriki.

Simba waliokuwa mabingwa wa Bara wakapewa nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa na Jamhuri ya Pemba kama mabingwa wa Zanzibar wakapewa tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho ambalo ndilo lilikuwa linaanza. Lakini Jamhuri wakasema hawana pesa kusafiri Afrika, wakajitoa.

Timu zingine zote za Zanzibar zikasema haziwezi ndipo nafasi ikahamia Bara na kuangukia kwa Mtibwa Sugar ambao walikuwa wa pili nyuma ya Simba. Lakini walipewa nafasi hiyo kwa masharti kwamba mechi zao za CAF wacheze Zanzibar.

Huo ndiyo mwaka ambao Mtibwa Sugar waliitwa watoto wa kambo wa Zanzibar. Lakini hata hivyo, walipopata nafasi wakagoma kwenda kuchezea mechi zao Zanzibar. Baada ya kushindikana kwa Ligi ya Muungano mwaka huo, ndiyo haikurudi tena hadi leo.

Wakati sasa yanakuja mashindano mengine yenye sura ya Muungano, tunakumbuka zama za Ligi ya Muungano. Yanga wanapokataa kwenda kushiriki, pia inatukumbusha namna ilivyovuruga hali ya hewa hadi kukoma kwa Ligi ya Muungano.

Hata hivyo, sababu kubwa kabisa ya Ligi ya Muungano kutofanyika tena ni kitendo cha Zanzibar kupata uanachama kivuli wa CAF. Uanachama huo ulimaanisha klabu zake zitashiriki moja kwa moja mashindano ya CAF bila kusubiri nafasi za MUUNGANO.

Kama siyo Yanga kufungua kesi, yawezekana Ligi ya Muungano ingeisha vizuri tofauti na ilivyoisha kwa hisani ya Yanga mahakamani.

Related Posts