Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, Leo Aprili 23, 2024 amekutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe kutoka Shirika la Kimataifa lisilo la Kiserikali, linalojihusisha na Afya ya Macho Jumuishi na Watu Wenye Ulemavu, ‘ Christian Blind Mission’ (CBM).
CBM lenye Makao yake Makuu Nchini Ujeruman, ambalo limejikita zaidi katika Mpango wa Kuwasaidia Wenye Ulemavu wa Macho, Ujumbe wake umewasili Ofisini kwa Mheshimiwa Makamu wa Kwanza, ili kueleza mafanikio na changamoto mbali mbali walizokutana nazo, katika Harakati zao.
Shirika hilo ambalo lilianza Kazi hapa Visiwani mnamo Mwaka 2022, linatarajia kukamilisha Harakati zake mwishoni mwa Mwaka huu wa 2024.
Viongozi na Waratibu mbali mbali wamehudhuria katika Kikao hicho wakiwemo; Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Harusi Said Suleiman; Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Dkt. Omar Dadi Shajak; Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya Zanzibar, Dr. Salim Slim; na Mratibu wa Shirika hilo hapa Nchini, Bi. Nesia Mahenge.
Wajumbe wengine waliohudhuria hapo ni kutoka katika Mataifa ya Kenya, Ethiopia, Ujerumani, na wenyeji Tanzania.
Kitengo cha Habari
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
Aprili 23, 2024.