Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Kampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya Akmenite Limited Lithuania, inatarajia kutumia dola za Marekani milioni 15 (Sh 38.9 bilioni) kujenga viwanda vitatu vya uchenjuaji wa madini ya metali katika mikoa ya Ruvuma, Dodoma na Lindi. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Arunas Sermuksnis

Hayo yamebainishwa leo Jumanne na Mkurugenzi wa Kampuni ya MAST, Georgefrey Kente ambaye ameonesha utayari wa kampuni yake kujenga viwanda hivyo vitatu mwaka huu.

Katika mazungumzo yake na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde Kente pamoja na Mwekezaji kutoka Lithuania, Arunas Sermuksnis ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni ya Akmenite Limited, amesema mazingira rafiki ya uwekezaji yaliyojengwa na Rais Samia Suluhu Hassan ndio siri ya wawekezaji hao kuja nchini.

Wawekezaji wote wameonesha nia kuanzisha ujenzi wa viwanda vya uchenjuaji wa madini ya metali kuunga mkono jitihada za serikali za kuongeza thamani madini nchini.

Aidha, Mkurugenzi wa kampuni ya Akmenite Limited Arunas Sermuksnis naye ameihakikishia serikali kwamba wataleta nchini teknolojia ya kisasa ya uchenjuaji wa metali ili shughuli za uongezaji madini ufanyike ndani ya nchi kwani hatua za awali za uanzishwaji wa kiwanda hicho zimeanza tayari.

Naye Mavunde amezipongeza Kampuni hizo kwa uamuzi huo wa kuwekeza viwanda vya uchenjuaji madini ndani ya nchi na kuhimiza ukamilishaji wake uwe ndani ya muda mfupi ili wachimbaji wa Tanzania wanufaike na fursa hiyo.

Amesema hivi sasa moja ya changamoto kubwa inayowakabili wachimbaji wa madini ya metali ni kukosekana kwa teknolojia ya uchenjuaji ili kutosafirisha madini ghafi nje ya nchi.

Mavunde pia amewahakikishia wawekezaji hao kwamba serikali kupitia Wizara ya Madini itatoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha kwamba uwekezaji huu unafanyika kwa manufaa ya maendeleo ya sekta ya madini Tanzania.

Aidha, wadau hao wameishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji  na kuwajali wachimbaji wadogo.

Related Posts