Tanzania nafasi ya 3 kwa tembo wengi barani Afrika

Imeelezwa kuwa Tanzania inaongoza kwa idadi kubwa ya simba, nyati, na chui huku ikishika nafasi ya tatu kwa kuwa na tembo wengi barani Afrika hivyo itachochea ongezeko la watalii na kufikia malengo ya serikali ya kufikisha idadi ya watalii milioni tano ifikapo 2025.

Takwimu hizo zimetolewa na mkurugenzi wa taasisi ya utafiti wa wanyamapori Tanzania TAWIRI Dkt. Eblate Mjingo wakati wa hafla ya kutangaza matokeo ya sensa ya wanyamapori na uzinduzi wa ripoti na taarifa ya watalii waliotembelea nchini Tanzania mwaka 2023

Akiwasilisha ripoti ya idadi ya watalii waliotembelea Tanzania kwa mwaka 2023 Dkt. Edward Kohi mkurugenenzi wa utafiti na mafunzo wizara ya maliasili na utalii amesema kuna ongezeko la asilimia 118 ukilinganisha na ukuaji wa asilimia 96.2 barani Afrika

Akitoa maelekezo ya serikali mara baada ya kuzindua ripoti ya idadi ya watalii na kupokea matokeo ya sensa waziri wa maliasili na utalii Anjela Kairuki ameelekeza taasisi za uhifadhi kuweka jitihada kuongeza wanyama ambao wanapungua na kuhakikisha tembo wanaoongezeka hawaleti madhara kwa binaadamu.

Sensa ya wanyamapori nchini Tanzania imefanyika katika mifumo mitatu ya ikolojia kati ya 11 iliyopo nchini na inalengo la kukuza, kuendeleza utalii, Kupunguza migogoro kati ya binaadamu na wanyamapori, sanjari na kusaidia utekelezaji wa mikataba ya uhifadhi.

Related Posts