WANAFUNZI KATIKA SHULE ZILIKUMBWA NA MAFURIKO WATAENDELEA NA MASOMO – WAZIRI MKENDA

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema Serikali imejipanga na itahakikisha wanafunzi ambao shule zao zimefungwa kutokana na mafuriko Nchini kote wanaendelea na masomo.

Mkenda amebainisha hayo April 22, 2024 wakati akizungumza na wahanga wa mafuriko katika kijiji cha Muhoro na Chumbi B Wilayani Rufiji mkoani Pwani, ambapo amewasisitiza Wazazi kuwaruhusu Watoto wote kwenda Shule zilizo karibu na maeneo waliyopo kuendelea na masomo.

Amesema kuwa mafuriko yasiwe sababu ya mtoto yeyote kukosa Elimu, na kwamba Shule zilizo karibu ziendelee kuwapokea Wanafunzi kutoka Shule zilizoathirika na kufungwa kuendelea na masomo huku Serikali ikiendelea na mikakati mingine ya muda mrefu ya kukabiliana na changamoto hiyo.

“Mwanafunzi yeyote anaepelekwa katika shule iliyo jirani na zile zilizoathirika apokelewe aendelee na masomob huku taratibu zingine zikiendelea , ikiwemo uhamisho iwapo mzazi ataridhia abaki hapo. Kikubwa apokele kwanza bila vikwazo” amesema Mkenda.

Prof. Mkenda amepongeza juhudi za Mkoa huo kwa kushirikiana na Viongozi mbalimbali kuratibu mahitaji ya kibinadamu pamoja na Elimu kwa wahanga hao, na kuongeza kuwa kwa upande wa elimu Serikali inaongeza nguvu kushughulikia suala hilo la dharura.

Amesema katika eneo hilo na mengine miundombinu ya elimu itajengwa upya ikiwemo madarasa, mabweni, vyoo na nyumba za walimu na kuongeza kuwa shule mpya ya sekondari ya Ufundi itajengwa Rufiji ikiwa ni moja kati ya shule 26 za Sekondari za Amali zinazotarajiwa kuanza kujengwa hivi karibuni.

“Tumekuja na Uongozi wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), niwaombe mpeleke taarifa Bodi kwa udharura ili muweze kufadhili ujenzi wa vyoo katika shule hizi zilizopokea wanafunzi waliotoka katika shule zilizoathirika maana idadi ya wanafunzi imeongezeka hivyo muhimu kulinda hali ya afya”, ameongeza Mkenda.

Mkuu wa mkoa wa Pwani Mhe. Abubakari Kunenge amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna Serikali inavyoshughulikia changamoto ya miundombinu ya Elimu, na ameipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa kuendelea kulipa kipaumbele suala hilo pamoja na kuimarisha ulinzi na malezi kwa wanafunzi wote.

Akizungumza mkazi wa kijiji cha Muhoro Bw. Rajabu Tota ameishukuru Serikali kwa kuwapatia maeneo salama ya kuhamia pamoja na kutoa nafasi watoto wao kupokelewa Shule zilizopo karibu kuendelea na masomo.

Related Posts