WAZIRI MAVUNDE  ASIKILIZA CHANGAMOTO ZA WADAU WA MADINI NCHINI

Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde leo Aprili 22, 2024 jijini Dodoma amekutana na wafanyabiashara wa madini na wachimbaji wa madini kwa lengo la kusikiliza changamoto zinazowakabili kwenye shughuli zao ikiwemo changamoto ya ukosekanaji wa teknolojia ya uchenjuaji wa baadhi ya madini na hivyo kuielekeza Tume kuandaa utaratibu sahihi wa usafirishaji wa madini yaliyongezwa thamani kwa kiwango cha teknolojia inayopatikana hapa nchini.

Ametoa maelekezo hayo, mara baada ya kusikiliza changamoto za wafanyabiashara wa madini na wachimbaji wa madini ikiwemo zuio la kusafirisha madini ghafi lililotolewa na Serikali mapema mwaka 2017 ambapo wameomba Serikali kuwapa muda wa kusafirisha madini yaliyoongezwa thamani kwa kiwango cha teknolojia inayopatikana nchini kwa sasa kutokana na kutokuwepo kwa viwanda vya kuchenjua madini hayo hali iliyowasababishia kuendesha shughuli zao kwa hasara.

“Naielekeza Tume ya Madini kuweka utaratibu maalum wa usafirishaji wa madini hayo kwa kipindi cha mpito cha mwaka mmoja wakati mkijipanga kuhakikisha madini yanachenjuliwa ndani ya nchi kwa kiwango kikubwa” amesema Mavunde.

Amesema kuwa, lengo la Serikali la kuweka mkazo wa kuyaongezea thamani madini yote nchini ni kuongeza faida kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini huku Serikali ikipata kodi zaidi, hivyo Sekta ya Madini kuendelea kuwa na mchango kwenye Pato la Taifa.

Aidha, amewataka wadau wa madini kuwekeza kwenye viwanda vya uchenjuaji wa madini sambamba na kuwakaribisha wawekezaji kutoka nje ya nchi kwenye ujenzi wa viwanda hivyo na kuongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini ipo tayari kutoa ushirikiano kwa wawekezaji wenye nia ya kuwekeza kwenye viwanda vya kuchenjua madini nchini.

“Muda wote milango ya ofisi yangu ipo wazi kwa mwekezaji yeyote mwenye nia ya kuwekeza kwenye kiwanda cha kuongeza thamani madini nchini, tunataka kuhakikisha Serikali inapata kodi zaidi fedha ambazo zinatumika kwenye uboreshaji wa huduma za jamii kama vile barabara, maji, vituo vya afya sambamba na kufungua fursa za ajira huku wadau wa madini wakiendelea kutajirika,” amesisitiza Waziri Mavunde.

Katika hatua nyingine amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini itaendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji nchini ikiwa ni pamoja na sheria na kanuni bora za madini, miongozo mbalimbali, kodi na tozo rafiki ili kuvutia wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi.

Ameongeza mikakati mingine kuwa ni pamoja na kuendelea kufanya tafiti mbalimbali kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na uanzishaji wa maabara ya kisasa ili kuhakikisha wachimbaji wa madini wanaendesha shughuli zao kwa uhakika na kutajirika.

“Kama Wizara ya Madini kupitia Vision 2030 ya Madini ni Maisha na Utajiri tumeweka lengo la kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 utafiti wa kina wa madini nchini (high resolution) uwe umefikia asilimia 50 kutoka asilimia 16 ya sasa; mpaka sasa tumeshafanya tafiti katika maeneo ya Dodoma, Geita, Kahama, Mirerani, Lindi na Mtwara,” amesema Mavunde.

Awali akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, *Kheri Mahimbali* amesema kuwa lengo la kikao hicho lilikuwa ni kusikiliza kero za wafanyabiashara na wachimbaji wa madini na kuzitatua sambamba na kutoa ufafanuzi katika maeneo mbalimbali yahusiyo Sekta ya Madini.

Kikao hicho pia kimehudhuriwa na Kamishna wa Madini Nchini, Dkt. Abdulrahman Mwanga, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba na menejimenti na watumishi kutoka Wizara ya Madini na Tume ya Madini.

Related Posts